Lugha, Fasihi na Elimu

Serikali yamulika shule hewa msituni Baringo

May 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA DAVID MCHUNGUH

WIZARA ya Elimu inachunguza sakata ya shule hewa katika Kaunti ya Baringo ambayo mbunge wa Baringo Kaskazini amehusishwa.

Uchunguzi huo unajiri kufuatia ufichuzi wa Taifa Leo wiki jana.

Ufichuzi huo ulianika sakata ya shule hewa zilizowekwa mabango, lango na ua lakini hakuna majengo, walimu au hata wanafunzi.

Hata hivyo, mbunge wa eneo hilo, Joseph Makilap alikanusha kuhusika katika sakata hiyo inayokiuka taratibu za usajili wa taasisi za elimu.

Haya yameibuka huku Wizara ya Elimu ikianzisha uchunguzi wa ndani kuhusu nia ya uwekaji mabango, lango na ua kutangaza Shule ya Upili ya Wasichana ya Kaptiony, Shule ya Sekondari ya Kampi ya Nyasi na Shule ya Sekondari ya mseto ya Kasaka.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amemwandikia Mkaguzi Mkuu wa Serikali Nancy Gathungu kuchunguza suala hilo.

Aliambia Taifa Leo kwamba ukaguzi wa kitaifa wa shule utafanywa baadaye, ingawa alikanusha kuwa na habari kuhusu shule hizo hewa.

“Katika wiki iliyopita, kumekuwa na ripoti za madai ya shule hewa katika Kaunti ya Baringo. Ripoti hizo ni pamoja na madai kwamba shule hizo hewa ni njia ya kupora fedha za umma,” inasema barua ya Waziri kwa Dkt Gathungu iliyoandikwa Mei 13, 2024.

“Kwa kuwa uchunguzi wetu wa awali umebaini kuwa shule zilizotajwa hazijasajiliwa na hazijapata stakabadhi au ufadhili kutoka kwa Wizara, tunaomba kwa maslahi ya umma na kwa uwajibikaji, pia ufanye ukaguzi maalum ili kubaini ukweli wa madai haya,” asema Bw Machogu kwenye barua hiyo.

Waziri pia amemwandikia Katibu wa Elimu Msingi, Dkt Belio Kipsang akimuagiza kuchunguza hali ya usajili wa shule hizo na iwapo zina bodi za usimamizi.

“Fanya uchunguzi na kutayarisha ripoti kuhusu mtu au watu waliohusika katika uwekaji wa mabango na/au lango kwa shule zinazodaiwa, na kwa kiwango ambacho kinaweza kuthibitishwa, lengo lao hasa,” inasema barua hiyo.

Bw Machogu alisema kuwa kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, uamuzi utafanywa kuhusu iwapo Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) itaombwa kufanya uchunguzi zaidi.

Mkurugenzi wa Elimu, Kaunti-ndogo ya Baringo Kaskazini, Kiprono Langat aliambia Taifa Leo kwamba hajahusika katika usajili wowote wa shule hizo na wala hajaidhinisha kufunguliwa kwa akaunti zozote za benki zinazohusiana nazo.

Bw Makilap alisema kuwa ardhi hiyo ilitolewa na wenyeji kwa madhumuni ya kuanzisha shule na ikawekwa mabango kuepusha wanyakuzi wa ardhi.

“Ilifanyika hata kabla sijawa mbunge. Tatizo ni nini ikiwa wazazi na jamii wameweka mabango ya shule zinazopendekezwa? Hatuwezi kuichafua Wizara ya Elimu kupitia propaganda. Hakuna pesa kutoka kwa CDF au Wizara ambazo zimetengwa kwa shule hizo za upili zilizopendekezwa,” alisema

Kulingana na Sheria ya Elimu ya Msingi (2013), mchakato wa usajili wa shule ya umma huanza kwa kutuma maombi kwa bodi husika ya elimu ya kieneo. Iwapo itaridhika kwamba kuanzishwa kwa taasisi kunazingatia mahitaji yaliyowekwa, bodi ina mamlaka ya kumjulisha muombaji ndani ya siku 30.

“Ikiwa ombi limeidhinishwa, bodi ya elimu ya kaunti itaarifu afisi inayowakilisha Baraza la Elimu, Viwango na Ubora katika kaunti iwapo ni shule ya msingi au sekondari inayoanzishwa,” sheria hiyo inasema.

Ikiwa bodi itakataa ombi, muombaji pia atafahamishwa kuhusu uamuzi huo.

Ili kusajiliwa, taasisi inapaswa kuwa na idadi ya kutosha ya walimu waliosajiliwa na wafanyakazi wasio walimu, vifaa vinavyofaa vya kufundishia, jina, maelezo ya mahali ilipo, anwani ya posta na kielektroniki.

Pia ijumuishe mifumo ya utawala na usimamizi wa taasisi husika.

Zaidi ya hayo, waombaji wanatakiwa kueleza idadi, sifa na uwezo wa walimu na watumishi wasio walimu, miundomsingi inayofaa pamoja na mambo mengine.

“Mtu yeyote atakayekiuka masharti ya kifungu hiki atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyozidi Sh20 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili .”

Mnamo 2017, afisa wa ngazi ya chini katika Wizara ya Elimu ambaye alisimamia uwekaji data kutoka kwa wakurugenzi wa elimu wa kaunti aliingiza shule hewa ya Upili ya Mundeku katika Kaunti-ndogo ya Khwisero, Kaunti ya Kakamega na pia akaunti ya benki.

Alishtakiwa kwa kupokea Sh11,131,305 kutoka kwa Wizara kama malipo ya wanafunzi 1,188 hewa.