• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Shule mama lao kwa idadi kubwa na baba lao kwa matokeo Lamu

Shule mama lao kwa idadi kubwa na baba lao kwa matokeo Lamu

NA KALUME KAZUNGU

SHULE ya Lake Kenyatta, Kaunti ya Lamu ni yenye fahari tele sio tu kutokana na kwamba inabeba hadhi au jina la Rais mwanzilishi, Hayati Mzee Jomo Kenyatta bali kwa masuala mengine mengi.

Ndio shule kubwa zaidi kwa idadi ya wanafunzi kote Lamu ikilinganishwa na shule zote 134 za msingi za umma na za kibinafsi zilizoko kaunti hiyo.

Ikipatikana mjini Mpeketoni, Lamu Magharibi, Shule ya Msingi ya Lake Kenyatta ina jumla ya wanafunzi 1,745, ikiwemo wale wa chekechea (ECDE) hadi Gredi ya Nane.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili mnamo Ijumaa, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi na Sekondari ya Msingi (JSS) ya umma ya Lake Kenyatta, Joseph Osio Agutu, alisema mbali na kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi kushinda shule nyingine zote za Lamu, Lake Kenyatta pia ina historia nzuri ya kuandikisha matokeo bora, hasa kwenye mtihani wa kitaifa wa mfumo uliopita wa darasa la nane (KCPE).

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi na Sekondari ya Msingi (JSS) ya umma ya Lake Kenyatta, Joseph Osio Agutu. Anasema licha ya kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi na kuandikisha matokeo bora, Shule ya Lake Kenyatta bado inakumbwa na changamoto tele, ikiwemo ukosefu wa madarasa ya kutosha ya wanafunzi kusomea. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kwa mfano, mnamo 2022, mwanafunzi aliyeongoza katika KCPE kote Lamu ni Ngaruiya Peter Mburu kutoka Shule ya Msingi ya Lake Kenyatta.

Alijizolea alama 413 kati ya 500.

Kwenye KCPE ya 2021, wanafunzi watatu kutoka shule hiyo hiyo ya Lake Kenyatta waliibuka miongoni mwa kumi bora, Kaunti ya Lamu, wakiwa na maksi 400 na zaidi kila mmoja.

Kwenye KCPE ya 2023, shule hiyo ya umma haikuachwa nyuma kwani ilifaulu kutoa msichana bora, Kimani Abigail Wamaitha, aliyepata alama 397 kati ya 500, hivyo kuitwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Alliance.

Bw Agutu alisema hajuti kwamba shule yake ndiyo yenye idadi kubwa ya wanafunzi kote Lamu, akitaja hatua hiyo kuwa miongoni mwa mambo yanayowapa walimu na wanafunzi motisha wa kufanya bidii zaidi masomoni.

Ina walimu wa msingi 31, wale wa sekondari msingi wanane na wa chekechea sita.

Lake Kenyatta pia ni miongoni mwa shule za kwanza kuanzishwa, hasa kwenye taarafa ya Mpeketoni.

Ilianzishwa mwaka 1975, kwa sasa ikiwa na umri wa miaka 49.

“Twajivunia kama wana Lake Kenyatta Primary kwamba sisi ndio mama lao kwa idadi kubwa ya wanafunzi kote Lamu. Isitoshe, sisi ndio baba lao bado likija suala la matokeo ya mtihani wa kitaifa eneo hili,” akasema Bw Agutu.

Ila zipo changamoto zinazoikumba shule hiyo, ambapo utawala wa taasisi hiyo unaamini zikisuluhishwa, Lake Kenyatta itakuwa miongoni mwa shule bora zaidi si Lamu tu bali pia Pwani na nchini kwa jumla.

Miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa madarasa ya kutosha kukimu kikamilifu idadi kubwa ya wanafunzi waliopo.

Bw Agutu anasema wanahitaji karibu madarasa manne ya ziada kuwakimu wanafunzi wa shule ya msingi pekee.

Pia wanahitaji madarasa mengine manne ya ziada ili kuwahifadhi wanafunzi wa sekondari msingi, hasa wale wa Gredi ya Tisa wanaofaa kuingia kuanzia mwaka 2025.

Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 200 wa Gredi ya nne ambao wamegawanywa na kuhifadhiwa katika madarasa matatu badala ya manne.

Gredi ya tano nao ni wanafunzi 191 waliogawanywa na kuhifadhiwa katika madarasa matatu ilhali pia wanahitaji kuwekwa katika madarasa manne.

Katika Gredi ya sita, shule hiyo ina wanafunzi 206 waliogawanywa katika madarasa matatu ilhali moja zaidi likihitajika.

Gredi ya saba kuna wanafunzi 202 waliogawanywa na kuhifadhiwa katika madarasa matatu ilhali wakihitajika kuwa madarasa manne.

Nayo Gredi ya nane, shule hiyo ina wanafunzi 224, ambapo wamegawanywa na kuhifadhiwa katika madarasa matatu pekee badala ya manne.

“Kama uonavyo, tunahitaji madarasa zaidi hapa. Serikali itusaidie ili masomo yaendelee vyema kwani wanafunzi wetu wanafinyana. Tunahitaji angalau madarasa manne zaidi kwa wanafunzi wa msingi na mengine manne zaidi kwa wanafunzi wa sekondari msingi kwenye shule hii yetu ya Lake Kenyatta,” akasema Bw Agutu.

Mbali na kwamba ina idadi kubwa ya wanafunzi kushinda shule zote za Lamu na kuvuma kwa kuandikisha matokeo bora ya mitihani ya kitaifa, Lake Kenyatta pia inajivunia kwa viongozi mashuhuri nchini ambao wamesomea shule hiyo.

Viongozi hao ni pamoja na Mbunge wa sasa wa eneo hilo (Lamu Magharibi), Bw Stanley Muthama Muiruri na aliyekuwa Kamishna wa zamani wa Lamu, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Masuala ya Utawala Katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Bw Njenga Miiri.

Mbunge wa Lamu Magharibi Stanley Muthama. Ni miongoni mwa watu mashuhuri nchini ambao wamesomea katika shule ya Lake Kenyatta mjini Mpeketoni, Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Katika mahojiano ofisini mwake mnamo Ijumaa aidha, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Lamu Zachary Mutuiri aliwasihi walimu, wanafunzi na wazazi wa shule hiyo kubwa ya Lake Kenyatta kuondoa shaka kuhusiana na masuala ya miundomsingi.

Kulingana na Bw Mutuiri, Wizara ya Elimu tayari inaendeleza mikakati kabambe itakayohakikisha madarasa zaidi yanajengwa shuleni humo mwaka huu.

“Tuliwasilisha mapendekezo kuhusiana na mahitaji yaliyoko Lake Kenyatta kwa Wizara ya Elimu. Tunavyoongea ni kwamba wizara imepasisha mapendekezo hayo, ikiwemo madarasa kati ya manne na tano yajengwe na kukamilishwa haraka shuleni Lake Kenyatta kabla ya mwaka ujao ambapo wanafunzi wa Gredi ya Tisa watastahili kuhifadhiwa,” akasema Bw Mutuiri.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wanawake Murang’a vitani kisiasa, kulikoni?

Ukiachia mjakazi shughuli zote nyumbani utakuja kulia...

T L