• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
Shule mwanga wa matumaini kwa wanafunzi kutoka Boni

Shule mwanga wa matumaini kwa wanafunzi kutoka Boni

NA KALUME KAZUNGU

KWA zaidi ya miaka 30 sasa, Shule ya Msingi ya Mokowe Arid Zone, Kaunti ya Lamu imekuwa kichocheo kikuu cha watoto kutoka jamii za wachache na wasiobahatika katika jamii kupata elimu.

Shule hiyo iko katika eneobunge la Lamu Magharibi.

Ni taasisi ya umma iliyoanzishwa tangu 1992, dhamira kuu ikiwa ni kuhudumia kielimu watoto kutoka jamii za wachache, ikiwemo Orma, Sanye, Boni na wengineo.

Shule hiyo ya mseto inatoa huduma za bweni, ambapo kuna wanafunzi, hasa wale wa kutoka sehemu za mbali ya Lamu ambao hulala na kuishi hapo wakati muhula wa masomo unapoendelea.

Sehemu ya kuingia kwa bweni la wasichana katika Shule ya Msingi ya Mokowe Arid Zone. PICHA | KALUME KAZUNGU

Shule hiyo pia inahudumia wanafunzi wa kuhudhuria masomo asubuhi, kushinda mchana kutwa na kisha kurudi nyumbani jioni.

Tangu kuanzishwa kwake, shule hiyo imekuwa kiungo muhimu kwani imeleta mwanga wa matumaini kwa wanafunzi ambao walikuwa wamekatiza kabisa matumaini kwamba ndoto yao ya elimu ingefaulu.

Itakumbukwa kwamba miaka ya hivi karibuni, Shule ya Msingi ya Mokowe Arid Zone imeibuka kuwa kiokozi cha pekee, hasa kwa wanafunzi wa jamii ya Waboni kutoka vijiji vya Msitu wa Boni, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Kati ya mwaka 2014 hadi sasa, eneo la Msitu wa Boni limekumbwa na changamoto tele za utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Hali hiyo ilisukuma shule tano za Msitu wa Boni, ikiwemo Milimani, Basuba, Mararani, Mangai, na Kiangwe kufungwa.

Licha ya juhudi za serikali kuu kudhibiti usalama wa msitu wa Boni na hata kuamuru shule hizo kufunguliwa, sio zote ambazo zilifaulu kufunguliwa.

Ila zile chache zinazohudumu kama vile Kiangwe, Mangai na Mararani zikihudumia wanafunzi wa madarasa ya chini, ambapo ni chekechea (ECDE) hadi Gredi ya Nne pekee.

Wanafunzi wa madarasa ya juu, kuanzia Gredi ya Tano hadi Gredi ya Nane, wamelazimika kuhamishwa vijijini mwao na kupelekwa Mokowe Arid Zone kuendeleza masomo yao.

Takwimu kutoka kwa utawala wa Shule ya Mokowe Arid Zone zinaonyesha kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 8,88, ambapo kati yao takriban 196 ni Waboni kutoka vijiji vya msitu wa Boni.

Licha ya shule hiyo kutoa mwanga wa matumaini kwa wanafunzi wa jamii za wachache, changamoto bado zimekuwa zikiiandama shule hiyo na hata wanafunzi wenyewe, hasa wale wa kutoka vijiji vya msitu wa Boni.

Kwa mfano, Mei 2023, shule hiyo ililazimika kufungwa kwa zaidi ya wiki mbili pale mafuriko yalipokumba taasisi hiyo, ambapo maji yalizagaa kila mahali kwenye uwanja wa shule hiyo.

Ukosefu wa chakula cha kutosha kuwakimu wanafunzi Mokowe Arid Zone pia umekuwa ukishuhudiwa mara kwa mara, ambapo utawala wa shule hiyo umekuwa ukijitokeza kuomba usaidizi kutoka kwa serikali ya kaunti, ile ya kitaifa na wahisani ili masomo yasiathiriwe.

Kila muhula wa elimu unapoanza, wanafunzi wa kutoka vijiji vya msitu wa Boni wamekuwa wakibebwa, iwe ni kupitia kwa helikopta ya kijeshi, pikipiki au mashua kutoka vijijini mwao hadi shuleni, ambapo hupiga kambi kwenye taasisi hiyo kwa muda wote wa muhula.

Mpangilio huo pia kwa mara kadhaa umeshuhudia changamoto, ambapo wanafunzi Waboni kila mara wamekuwa wakichelewa kufika shule kusoma wakati mihula inapofunguliwa.

Je, wakati huu ambapo shule zinatazamiwa kufunguliwa kwa muhula wa pili kote nchini kuanzia Jumatatu, Mokowe Arid Zone imejipanga vipi?

Katika mahojiano na Taifa Leo, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bw Charles Joseph Mzee, alisema wako tayari kuanza muhula wa pili Jumatatu.

Baadhi ya madarasa katika Shule ya Msingi ya Mokowe Arid Zone. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Mzee aidha alitaja baadhi ya changamoto, ikiwemo ukosefu wa vyoo vya kutosha kukimu idadi kubwa ya wanafunzi shuleni humo.

Shule ya Mokowe Arid Zone ina jumla ya vyoo 16 ambapo baadhi yake vinavuja na kufura wakati mvua inaponyesha.

Aliiomba serikali na wahisani kujitokeza kuwajengea vyoo Zaidi ili masomo shuleni humo yaendelee vyema.

“Twatarajia kufungua shule yetu Jumatatu pia kama wengine nchini. Wanafunzi kutoka msitu wa Boni huwa wanasafirishwa kufika hapa kupitia boti, pikipiki au helikopta ya kijeshi. Ni matumaini yangu kwamba wahusika wanaendeleza mikakati ili wanafunzi wetu wafike hapa mapema muhula huu kuendelea na masomo,” akasema Bw Mzee.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Lamu, Bw Zachary Mutuiri, anasema kamati mbalimbali za usimamizi wa shule za Lamu (BOM) zinakutana Alhamisi (leo) ili kujadili hali ilivyo shuleni, ambapo changamoto zozote zitakazojitokeza zitasuluhishwa haraka kupisha muhula wa pili kuendelea Jumatatu.

Bw Mutuiri alisema shule nyingi za Lamu ziko hali shwari kwani mafuriko hayajaathiri sana eneo hilo.

“Pengine shule zinazokaribiana na mto Tana kama vile Chalaluma ndizo ambazo tuko na wasiwasi nazo. Ila tunaamini shule zote Lamu zitafunguliwa kufikia Jumatatu. Changamoto zilizopo zitajadiliwa na kushugulikiwa leo,” akasema Bw Mutuiri.

Kaunti ya Lamu ina jumla ya shule za msingi 134, ikiwemo za umma na zile za kibinafsi.

Idadi ya shule za sekondari zilizoko kaunti hiyo pia ni karibu 100.

  • Tags

You can share this post!

‘Obado alikuwa kwa Raila usiku ule Sharon aliuawa’

Tunazima kabisa uhasama wa kikabila Sondu – Kindiki

T L