Siri ya kumudu ‘Karatasi ya Pili’ ya KCSE Kiswahili
KARATASI ya Pili katika KCSE Kiswahili huwa na sehemu nne – Ufahamu, Muhtasari/Ufupisho, Sarufi na Matumizi ya Lugha na Isimujamii.
SEHEMU A. UFAHAMU (ALAMA 15)
Ufahamu aghalabu hulenga kutathmini uwezo wa mtahiniwa kujifasiria ujumbe katika kifungu na kuwasilisha ufasiri huo kwa usahihi kupitia maandishi.
Taarifa ya ufahamu inaweza kuwa ndefu au fupi; sahili au changamano kutegemea uzito wa ujumbe uliomo.
Mtahiniwa asome kifungu kwa zaidi ya mara tatu. Kusoma kwa mara ya kwanza kuwe kwa haraka tu ili kujua yaliyomo.
Afanye hivyo kwa kunakili au kupigia mstari hoja muhimu zinazojitokeza katika kifungu. Asome kwa mara nyingine kisha arejelee maswali chini ya kifungu. Atagundua kwamba mara nyingi majibu kwa swali la kwanza na pili hupatikana katika aya ya kwanza, ya pili, n.k.
Mtahiniwa atambue kwamba “maneno elekezi” ndiyo mtihani wenyewe. Azingatie anachohitajika kufanya anapoulizwa ‘fafanua’, ‘taja’, ‘eleza’, ‘toa’, ‘dondoa’, ‘andika’, ‘nakili’ n.k.
Mtahiniwa aepuke ‘ukasuku’. Asiradidi swali kabla ya kutoa jibu lake. Kwa mfano: “Kulingana na taarifa uliyoisoma, toa sababu tatu zilizomfanya Almasi aadhibiwe na mwalimu wake (Alama 3)”.
Mtahimiwa atoe jibu lake moja kwa moja badala ya kusema: “Kulingana na taarifa niliyoisoma, sababu tatu zilizomfanya…”
Huko kutamfanya mtahiniwa atumie vibaya nafasi aliyotengewa kutolea jibu lake. Majibu yoyote yanayoandikwa nje ya nafasi iliyotengewa huwa hayasahihishwi.
Mtahiniwa azingatie muktadha wa maneno aliyoulizwa kutolea maana yake. Mara nyingi maana ya neno hubainika kutokana na jinsi lilivyotumiwa katika kifungu na mtahiniwa asijikite katika kamusi tu.
Azingatie pia nafsi iliyotumiwa katika neno asilia na asiibadilishe au kuidondosha anapoandika jibu. Kwa mfano, maana ya ‘kuyahofia’ ni ‘kuyaogopa’ – si ‘kuogopa’.
SEHEMU B. MUHTASARI (ALAMA 15)
Mtahiniwa asome kifungu zaidi ya mara tatu akifasiri maana na ujumbe unaojitokeza. Chini ya kifungu, huwepo nafasi ya ‘Matayarisho’ au ‘Nakala Chafu’ kwa mtahiniwa kuandaa vidokezo vya jibu lake kabla ya kulihamisha kwa usahihi katika nafasi ya ‘Jibu’ au ‘Nakala Safi’.
Mtahiniwa asitangulize jibu kwa kupendekeza kichwa au anwani ya kifungu alichokisoma.
Jibu sharti liwasilishwe katika aya moja tu ambayo itahifadhi kiini cha taarifa ya kifungu.
Idadi kamili ya maneno iandikwe kwenye mabano chini ya jibu. Mtahiniwa ana uhuru wa kuzidisha jibu lake kwa maneno tisa pekee ya yale aliyoagizwa kutumia.
Ni muhimu kuzingatia kanuni za sarufi na kuepuka makosa ya hijai. Mtahiniwa apigie mstari mmoja wa mahazari/mchinjo kati vidokezo vyake katika ‘Nakala Chafu’.
SEHEMU C. SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
Baadhi ya vitahiniwa ni sauti; silabi; mofimu, mzizi na viambishi; aina za maneno; aina za sentensi; virai na vishazi; miundo ya sentensi; upatanisho wa ngeli za nomino; nyakati na hali (njeo); uakifishaji; mnyambuliko wa vitenzi; usemi halisi na usemi taarifa; umoja na wingi wa nomino; ukubwa na udogo wa nomino; na uundaji wa maneno.
Ukanushaji na uyakinishaji; mwingiliano wa maneno; matumizi ya viambishi na maneno maalumu; vinyume vya vitenzi; visawe, vitate na vitawe; na uchanganuzi wa sentensi pia hutahiniwa katika sehemu hii.
Majibu ya mtanihiwa yaanze kwa herufi kubwa na yaishie kwa kitone au alama ya nukta.
Majibu yawasilishwe kwa hati nzuri inayosomeka kwa urahisi
Majibu yasitangulizwe kwa vinyota, vistari, vitone vizito au mishale.
Mtahiniwa atumie ama nambari, herufi za alfabeti au nambari za Kirumi pekee kutanguliza jibu lake.
SEHEMU D. ISIMUJAMII (ALAMA 10)
Mtahiniwa anatarajiwa kuelewa maana na dhima ya Isimujamii; maana, sifa na dhima ya lugha; sifa za mawasiliano; hadhi na sifa za lugha ya taifa na rasmi; chimbuko na asili ya Kiswahili; Usanifishaji wa Kiswahili, sababu za maenezi ya Kiswahili; dhima ya Kiswahili kama lugha ya taifa, rasmi na ya kimataifa; na matatizo na suluhu kwa changamoto zinazokabili Kiswahili.
Afahamu pia sera na taratibu za kudhibiti matumizi ya lugha; lahaja za Kiswahili; sifa na dhima ya lugha katika sajili mbalimbali; makosa katika mazungumzo au mawasiliano na dhana kama vile lakabu, misimu, lafudhi, krioli, pijini, msimbo, lingua franka; n.k.
Mtahiniwa atakosa alama zote iwapo atashindwa kutambua sajili husika hata kama atataja sifa sahihi za lugha katika sajili aliyoulizwa kubainisha.
Majibu yaambatanishwe na mifano kwa hoja iliyozuliwa kutoka kwenye tungo au kifungu husika.
Idadi sawa ya hoja itolewe kwa idadi sawa ya alama kwa kila swali.
USHAURI
Mtahiniwa atangulie kujibu maswali katika Sehemu za C na D. Kwa kufanya hivyo, muda mwingi utatengewa maswali ya Sehemu za A na B ambazo aghalabu huhitaji uchanganuzi mwingi na akili tulivu mno.