‘Taifa Leo’ linaendana na wakati tangu kuzinduliwa kwake – Wazee
NA KALUME KAZUNGU
“Kumekucha! Ninapolisoma gazeti la Taifa Leo mimi binafsi huhisi kumepambazuka.”
Hiyo ni kauli ya mzee na babu wa kisiwa cha Lamu, Bw Athman Ahmed Umar.
Licha ya mzee Umar kutinga umri wa miaka zaidi ya 70, kila ukimuona huwa amejibanza kibarazani kwake katika mtaa wa Langoni kwenye Mji wa Kale wa Lamu huku akilidurusu gazeti la Taifa Leo.
Bw Umar ni mmoja tu kati ya mamia ya wazee wa kisiwa cha Lamu na mwambao wa Pwani kwa jumla ambao hupendelea sana kulisoma gazeti la Taifa Leo.
Katika ulimwengu wa leo, tunajua fika kuwa magazeti ni muhimu kwani ni mojawapo ya mifumo sufufu ya kuwapasha watu habari na kuwaelimisha pia.
Taifa Leo, aidha, ilizama ndani kutaka kujua hasa ni nini sababu za mababu wengi Lamu na Pwani kupenda sana kulisoma hili gazeti la Taifa Leo.
Kwa upande wake, Bw Umar anasisitiza kuwa Taifa Leo ni gazeti la kipekee ikilinganishwa na magazeti mengine nchini Kenya na ulimwenguni.
Hili linatokana na kile anachokitaja kuwa ‘lugha rahisi na nyepesi’ kueleweka.
Ikumbukwe kuwa Taifa Leo ndilo gazeti la kwanza nchini Kenya kuwahi kuchapishwa kwa lugha ya Kiswahili.
Ni gazeti linalomilikiwa na Shirika la Habari la Nation Media Group.
Gazeti hili lilizinduliwa rasmi mwaka 1958.
“Gazeti la Taifa Leo hunitoa nta masikioni kwa kunihabarisha au kunijulisha matukio mengi, iwe ni ya papa hapa nchini au ulimwenguni kote. Lugha yake ya Kiswahili ni nyepesi na linaendana kabisa na rika letu sisi mababu,” akasema Bw Umar.
Ramadhani Ali, mkazi wa mtaa wa Mkomani kisiwani Lamu, anasema yeye hafahamu uwepo wa gazeti lingine lolote isipokuwa Taifa Leo.
Bw Ali,75, amedumu akilisoma Taifa Leo kwa karibu miaka 50 sasa.
Anasema baada ya kuzinduliwa rasmi miaka ya hamsini (1950s), yeye tayari alikuwa akifanya kazi ya kuuza dukani mjini Mombasa.
Anasema dukani kila siku alikuwa akipata fursa ya kusoma Taifa Leo.
“Tangu hapo hadi wa leo imekuwa kawaida yangu kama ibada kudurusu Taifa Leo karibu kila siku. Sioni sababu ya kunizuia kulisoma hili gazeti, ikizingatiwa kuwa ndilo la kwanza la lugha ya Kiswahili kuchapishwa nchini Kenya. Hunivutia kwa lugha yake ya kueleweka. Hunipa fahari nikilisoma,” akasema Bw Ali.
Alexander Mutua, mzee na mpenzi wa Taifa Leo mjini Mpeketoni, anakiri kuvutiwa na nembo ya mnazi kwenye kurasa za nje za gazeti hilo.
Bw Mutua anasema kuwepo kwa nembo hiyo ya mnazi kwenye Taifa Leo mahususi kwa eneo la Pwani hulifanya gazeti hilo kuwa na mwonekano unaoshabihiana kikamilifu na uhalisia wa eneo la Pwani.
Anasema sababu nyingine inayomfanya kukimbilia kununua na kusoma Taifa Leo ni vichekesho vilivyomo, hasa kurasa za Dondoo za Hapa na Pale.
“Taifa Leo ina muonekano wa Kipwani. Mimi hufurahia sana kuvunjwa mbavu na taarifa cheshi kwenye kurasa za Dondoo za Hapa na Pale. Furaha, hasa kwetu sisi wazee, ni jambo la maana. Taifa Leo hutusahaulisha au kutuondolea kabisa msongo wa mawazo, kutuliwaza, hivyo kuwa na maisha marefu ya uzeeni,” akasema Bw Mutua.
Bi Doris Karembo,60, mkazi wa Malindi, anasema yeye pia hupendelea kusoma Gazeti la Taifa Leo miaka nenda miaka rudi.
Sababu zake ni kuwa Pwani ni Uswahilini, hivyo Taifa Leo, ambalo huchapishwa kwa lugha ya Kiswahili, huendeleza hadhi ya Pwani, ikiwemo kuhifadhi mila, desturi na tamaduni za eneo hilo.
“Nisiposoma Taifa Leo hapa Pwani nitasoma nini. Mojawapo ya majukumu ya lugha ni kuhifadhi na kuendeleza tamaduni. Twajivunia Taifa Leo kwa lugha yake ya Kiswahili tunayohisi ni ya muktadha kindakindaki wa Pwani. Yaani sera za Pwani zauzwa au kutangazwa kupitia usomaji wa Taifa Leo,” akasema Bi Karembo.
Mababu na akina nyanya wengine waliohojiwa pia walitaja maandalizi ya taarifa za Taifa Leo kuwa yenye kuvutia.
Bw Abubakar Hussein alisema taarifa nyingi kwenye gazeti hilo hugusia masuala ya mashinani au mashambani kabisa.
“Twaona fahari tukisoma taarifa zinazotuhusu au kutugusa kwa njia moja au nyingine kupitia Taifa Leo. Nikiona kijiji chetu kimetajwa kwa habari mimi hujiweka au kujishirikisha katika mazingira hayo kwenye usomaji wangu,” akasema Bw Hussein.
Naye Bw Kahindi Tsofa,78, mkazi wa Kilifi Mjini, anasema yeye hupendelea taarifa fupifupi zilizoko pembezoni mwa kurasa za Taifa Leo.
“Macho yangu huwa hayaoni vizuri, hivyo hupenda sana hizi taarifa fupifupi. Nikiona Lamu, Kilifi, Mombasa, Nairobi, Embu na kaunti zingine zikiwa zimeangaziwa kwa ufupi mimi hukimbilia kujifahamisha kwa muda mfupi bila kutapatapa,” akasema Bw Tsofa.
Wazee pia walitaja mawaidha au wosia ambao hutolewa kwenye baadhi ya kurasa za Taifa Leo kuwa mwafaka, wakisema huwaongezea busara katika kuishi kwao.