• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Unesco mbioni kutambua Mwazindika, ngoma ya jadi Taita Taveta

Unesco mbioni kutambua Mwazindika, ngoma ya jadi Taita Taveta

NA LUCY MKANYIKA

JUHUDI zinaendelezwa ili ngoma ya kitamaduni ya jadi Taita Taveta inayojulikana kama Mwazindika itambuliwe na kulindwa kimataifa kupitia kwa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Ngoma hiyo iko katika mchakato wa kuorodheshwa kama ‘Urithi wa Utamaduni Usioonekana’ na shirika hilo.

Iwapo itaorodheshwa, ngoma hiyo italindwa na kukuzwa na shirika hilo.

Kwa sasa, wataalamu wa Unesco, wakiongozwa na mshauri wa utamaduni wa ukanda wa Afrika Mashariki Masanori Nagaoka na Mkurugenzi wa Utamaduni wa Tume ya Kitaifa Julius Mwahunga, wanazuru kaunti hiyo ili kushirikiana na wadau mbalimbali kuhusu mchakato wa kuandikisha ngoma hiyo.

Watafanya vikao na maafisa wa serikali na wale wa taasisi mbalimbali, wachezaji wa Mwazindika kutoka makundi tofauti, na baraza la wazee kutoka sehemu mbalimbali za kaunti.

Vilevile, unesco itahifadhi na kurekodi ngoma hiyo, pamoja na kukusanya maoni kutoka kwa wadau.

Ngoma hiyo inajumuisha upigaji ngoma, uimbaji na unenguaji wa viuno, ikionyesha utamaduni wa Wataita.

Kundi la Gonda ya Bara Isanga la Densi ya Kitamaduni ya Mwazindika latumbuiza wataalamu wa Unesco katika eneo la Bura, Kaunti ya Taita Taveta. PICHA | LUCY MKANYIKA

Wakati wa kucheza nyimbo za Mwazindika, wanaoshiriki hutumia ngoma kubwa zilizotengenezwa na shina za miti zilizochimbwa, zikipambwa na ngozi ya ng’ombe na shanga na vilevile kupiga firimbi na vigelegele. Wachezaji huvaa kofia za aina yake vichwani, mikufu, bangili, na vikuku vya miguu.

Ngoma hiyo huchezwa na wanaume na wanawake, haswa wakati wa sherehe kama harusi, mazishi, na tamasha zinginezo. Aidha huonyesha utamaduni wa jamii hiyo, pamoja na historia yao, maadili, na kanuni za kijamii.

Wakati wa kucheza ngoma hiyo, wanaoshiriki husisimuka kiasi kwamba wakati mwingine hupagawa, haswa wakati ngoma inapopigwa.

Kundi la Gonda ya Bara Isanga la Densi ya Kitamaduni ya Mwazindika latumbuiza wataalamu wa Unesco katika eneo la Bura, Kaunti ya Taita Taveta. PICHA | LUCY MKANYIKA

Mwazindika ni ngoma ambayo imepitishwa kutoka kizazi hadi kizazi na pia imetumika kama chombo cha mabadiliko ya kijamii, na vilevile kukuza na kutetea masuala yanayoathiri watu wa eneo hilo.

“Ziara hii ina lengo la kuhifadhi utamaduni huu kwa kizazi kijacho. Tunafanya hivi kwa ajili ya siku zijazo,” alisema Dkt Nagaoka.

Kwa upande wake, Bw Mwahunga alisema kuwa kuorodheshwa kwa Mwazindika kwa kitengo hicho kutaboresha utalii wa kaunti hiyo.

“Wakati wa ziara hii, pia tutafanya mkutano wa siku mbili na wadau ili kupata maoni yao na ridhaa ya kuendelea na mchakato huu. Hatutalinda tu ngoma bali pia utamaduni unaokuja nayo kama vile chakula, mavazi na mengine,” alisema.

Gavana Andrew Mwadime alisema kuwa kuorodheshwa kwa ngoma ya Mwazindika kutasaidia kuitambua ulimwenguni, na hivyo kuboresha utalii wa eneo hilo kupitia utamaduni.

“Vilevile itaongeza fahari na itatambulisha jamii yetu ya Wataita ulimwenguni. Ni jukwaa nzuri la kuonyesha uwezo wetu wa utalii na hivyo kuwanufaisha watu wetu kiuchumi,” alisema gavana Mwadime.

Timu hiyo inatarajiwa kuwasilisha ripoti kwa kamati ya Unesco ambayo itafanya uamuzi wa mwisho kuhusu kuorodheshwa kwa ngoma hiyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Utalii katika kaunti hiyo Bw Wallace Mwaluma alisema kuwa mchakato huo ulianza mwaka jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Utamaduni nchini baada ya ngoma hiyo kusisimua waliohudhuria sherehe hizo katika ukumbi wa makavazi ya Bomas of Kenya.

“Tumefanya vikao kadhaa na hivi sasa tuko katika hatua ya mwisho kabla ya maamuzi hayo muhimu kufanywa na shirika la Unesco,” alisema.

Mwanachama wa Kundi la Gonda ya Bara Isanga la Densi ya Kitamaduni ya Mwazindika akitumbuiza wataalamu wa Unesco katika eneo la Bura, Kaunti ya Taita Taveta. PICHA | LUCY MKANYIKA
  • Tags

You can share this post!

Wachuuzi wanne washtakiwa kuuza dawa ‘feki’ ya...

Juhudi za mwanamke kusimamisha mazishi ya Kiptum zagonga...

T L