Lugha, Fasihi na Elimu

Viongozi wapamba mikutano ya basari kwa burudani wakiishia kuwapa wanufaika Sh3,000

January 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

VISA vya wanasiasa kutumia pesa nyingi kurembesha mikutano ya kusambaza basari halafu kuishia kuwagawia watoto wanufaika pesa ambazo hazisaidii vinafaa kuorodheshwa kama ufisadi, mwenyekiti wa wazazi wa Murang’a Bw David Njau amesema.

Bw Njau amelalamika kwamba wanasiasa kwa mfano hutumia zaidi ya Sh5 milioni kupanga mikutano ya ugavi basari kisha mwanafunzi anayefaa kulipiwa karo ya Sh40,000 anapewa Sh3,000 pekee.

“Tuchukue mfano wa hapa Murang’a mnamo Jumapili iliyopita ambapo Gavana Irungu Kang’ata aliandaa mkutano mkubwa wa kugawa basari kwa wanafunzi maskini,” akasema Bw Njau.

Alisema kwamba majukwaa yalipambwa kwa kiasi anachokadiria ni mamilioni. Hapo pia kulikuwa na mazulia ya kifahari.

“Nilihesabu zaidi ya magari 100 ya kuwekwa mafuta na walipa ushuru yaliyofika katika uwanja wa Mumbi. Mawaziri Moses Kuria (Utumishi wa Umma) na Ezekiel Machogu wa Elimu pia walifika,” akasema.

Bw Njau aliongeza kwamba mkutano huo ulikuwa na watumbuizaji wa kulipwa huku vifaa vya muziki na sauti vikiwa vya kukodishwa.

Aidha, Bw Njau alisema kwamba wengi wa wazazi waliofika katika mkutano huo walikuwa wamelipa nauli halafu serikali ya Kaunti ikagharimia vitu kama maji na chakula.

La mno, hafla hiyo ikawa imelipiwa katika vyombo vya habari ipeperushwe moja kwa moja kwa muda wa saa tano na kile kilisheheni zaidi ni siasa za 2027 na 2032.

“Swali ninalojiuliza ni hili. Hizo pesa zote zilizotumika kwa maandalizi haziwezi zikapungua Sh20 milioni. Si bora zingetumika kuzidisha kiwango cha basari kwa watoto?” akahoji.

Labda ni katika busara hiyo ambapo mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua naye alilalamika kwamba Serikali ya Kaunti inafaa kutoa kati ya Sh40,000 na Sh50,000 kama basari kwa kila mnufaika.

“Unapotuita katika kikao kama hiki unafaa kutoa pesa ambazo zitamsaidia mtoto kubakia shuleni ndipo nasi wanasiasa wengine ambao tuko na vitita vidogo vya basari tushikilie hawa watoto wasome,” akasema Bi Wa Maua.

Bi wa Maua aliteta kwamba “tunaweka sherehe za kutoa basari lakini vile viwango tunagawa vinaishia watoto kufukuzwa shuleni ilihali tunaweza kutia bidii hawa watoto wabakie darasani hadi wawe kile wanachotamani kuwa”.

Katika visa vingine, wanasiasa hufika katika mikutano wakitumia usafiri wa ndege lakini basari wanazotoa ni za bajeti ya chini kuliko gharama ya mafuta ya usafiri huo.

Hivi majuzi kulichipuka tetesi katika eneobunge la Gatanga baada ya kuibuka kwamba mtoto aliyekuwa amefukuzwa kwa kukosa karo ya Sh35,000 katika Shule ya Upili ya Murang’a alipewa basari ya Sh3,000 pekee.

Bw Njau alisema kwamba “ili kutufumba macho, wao husema serikali haigawi fedha kwa mujibu wa idadi ya watu”.

“Hizo kidogo walizo nazo wanazitumia kuandaa mikakati ya kisiasa,” akadai.