• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Watanzania walemea Wakenya katika tuzo za Fasihi

Watanzania walemea Wakenya katika tuzo za Fasihi

NA WANDERI KAMAU

WATANZANIA waling’aa kwenye mashindano ya 2023 ya Tuzo ya Fasihi ya Safal-Cornell, kwa kuibuka washindi kwenye vitengo vyote.

Kwenye mashindano hayo, yaliyofanyika katika hoteli moja, Ijumaa, jijini Nairobi, hakuna Mkenya hata mmoja aliyeibuka mshindi, licha ya baadhi ya waandishi nchini kuwasilisha kazi zao.

Mwandalizi mkuu wa mashindano hayo huwa ni Profesa Mukoma wa Ngugi, aliye mwanawe mwandishi maarufu wa vitabu, Prof Ngugi wa Thiong’o, kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Cornell, nchini Marekani, anakosomesha Fasihi.

Mashindano hayo huwa yanaandaliwa kila mwaka, chini ya ufadhili wa shirika la Safal Group, kupitia kampuni yake ya Mabati Rolling Mills, inayotengeneza mabati nchini Kenya.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na majaji mnamo Ijumaa, waandishi Philipo Oyaro na Ahmad Simba kutoka Tanzania waliibuka washindi kwenye kitengo cha riwaya.

Wawili hao walishinda kupitia vitabu vyao ‘Dunia Duara’ na ‘Safari ya Maisha’ mtawalia. Wawili hao ndio walikuwa wakiwania tuzo katika kitengo hicho, pamoja na mwandishi Nicholas Ogal kutoka Kenya, kupitia kitabu chake ‘Salome Anaishi’.

Watanzania pia waling’aa katika kitengo cha ushairi, baada ya waandishi Fatuma Salim na Lenard Mtesigwa kuibuka washindi. Walishinda kupitia madiwani yao ‘Changa la Macho’ na ‘Ndani ya Subira Kichwangomba’. Mkenya wa pekee aliyekuwa akiwania tuzo katika kitengo hicho ni John Karithi kupitia diwani yake ‘Ushairi wa Maisha ya Kesho.’

Akiwatangaza washindi, Profesa Kyallo Wamitila—aliyekuwa Jaji Mkuu—alisema kuwa jumla ya miswada 196 iliwasilishwa kwa jopo la majaji.

Alisema kuwa kila mmoja ni mshindi, kwani miswada yote ilikuwa na ubora wake.

“Miswada yote ilikuwa na ubora wake, japo lazima tungeiteua miswada bora zaidi,” akasema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Simamizi ya Tuzo hizo, mshairi na mkeretekwa wa Kiswahili, Abdilatif Abdallah, alisema kuwa msukumo mkuu wa tuzo hizo ni kuwapa nafasi Waafrika kuandaa tuzo zao wenyewe ili kuendeleza lugha asilia.

Mshindi katika vitengo vyote viwili (riwaya na ushairi) hutuzwa Sh750,000  huku mshindi wa pili akituzwa Sh375,000 katika kitengo chochote kile.

  • Tags

You can share this post!

Matrekta yageuzwa mabasi ya shule Lamu

Kibarua cha kukabiliana na janga la ulevi Mlima Kenya

T L