• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wito wanafunzi wa vyuo vikuu wasitengwe na serikali, wafadhili

Wito wanafunzi wa vyuo vikuu wasitengwe na serikali, wafadhili

NA ALEX KALAMA

WADAU katika sekta ya elimu kaunti ya Kilifi, wameitaka serikali na mashirika ya kijamii kutenga na kuelekeza fedha zaidi masomoni, wakitakiwa pia kuweka zingatio kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Aidha wadau hao wamekosoa mashirika na serikali kwa kuweka ufadhili zaidi kwa wanafunzi wanaotoka shule za msingi na kujiunga sekondari, huku asilimia ndogo ya mashirika hayo ikijitokeza kufadhili wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu.

Akizungumza wakati wa kupeana hundi ya Sh855,000 kwa wanafunzi 30 wanaojiunga na shule za sekondari, mkurugenzi mkuu wa wakfu wa Imarika Peter Angore ametoa wito kwa wadau kuweka ufadhili zaidi kwa wanafunzi wanaotoka shule za upili na kujiunga na vyuo vikuu.

Alisema kuna visa vingi vya wanafunzi wanaomaliza shule za msingi kufadhiliwa wanapoingia katika shule za upili, lakini masomo yao kukwama pindi wanapokamilisha elimu ya sekondari.

“Kwa hivyo nataka kuomba serikali za kaunti na serikali kuu kwamba katika hali hiyo ya kusaidia, basi mgao zaidi uweze kuletwa ili wanapopita hawa wanafunzi vizuri wa Kidato cha Kwanza mpaka Kidato cha Nne, bado tuweze kuwasaidia kuendelea na elimu katika vyuo vikuu,” alisema Bw Angore.

Mzee Boniface Yaa, mkazi wa Kilifi kwa upande wake ameyataka mashirika na wafadhili wote kuangazia wale waliopata alama za wastani badala ya wadau wote kuwaangazia waliofanya vyema na kuwatenga wale ambao hawakufanya vyema sana katika mitihani yao ya kitaifa.

“Sababu kubwa ya mtu kupatiwa ufadhili ni sababu ya kukosa uwezo. Kwa hivyo, wakati wanaangalia hawa ambao wamefanya vizuri pia kuna wale ambao hawakufanya vizuri sana japo nao wamefanya vizuri. Nao kwa sababu wana haki ya kusoma wangefikiriwa pia wapate ufadhili ili nao wasikose kusoma,” alisema Bw Yaa.

  • Tags

You can share this post!

Hali ngumu ya maisha yalazimu mama kufanya kazi ya tuktuk...

Safari ya barobaro singo aliyeanza ufugaji na kuku 3, sasa...

T L