Maana halisi ya ‘AirBnBs’ na kwa nini jina hilo limejikuta katika utata wa mauaji
NA WANDERI KAMAU
KWA wengi, huenda neno ‘AirBnB’ likawa geni.
Ni mfumo mpya wa kibiashara, ambapo wamiliki wa nyumba huwa wanakodisha watu kwa siku moja ama siku kadhaa.
AirBnB, ikiwa ni jina lenye asili ya kampuni ya Amerika iliyo na makao yake makuu San Francisco na inayofanya kazi kwa njia ya kimitandao kutoa huduma za makazi ya muda mfupi, ni biashara inayoanza kuvutia umaarufu nchini Kenya.
Ingawa ni mfumo wa kibiashara unaolingana na ule wa watu kukodisha chumba cha kawaida cha malazi, huu ni tofauti.
Licha ya biashara ya nyumba hizi maalum kuanza kushika kasi nchini, kuna uwezekano mkubwa kwamba wengi wa wawekezaji hawajajisajili kupitia kampuni asilia iliyoko Amerika.
Tofauti yake ni kuwa, AirBnB huwa na vifaa vyote ambavyo nyumba ya kawaida huwa navyo—kama vile jikoni, viti, runinga na kitanda.
Hivyo, mtu hujihisi kuwa kama yuko kwenye nyumba ya kawaida, badala ya chumba cha malazi au ‘lodging’, ambacho huwa na mahali pa kulala tu.
Ikizingatiwa ni mfumo mpya wa kibiashara duniani, umeibukia kuwa wenye mvuto Kenya.
Watu wengi, ambao awali walikuwa wakikodisha vyumba vya kawaida vya malazi kulala wanapozuru maeneo tofauti kwa shughuli za kikazi ama matembezi, sasa wameamua kutumia AirBnBs.
Ijapokuwa bei ya kukodisha nyumba hizo ni ghali, ikilinganishwa na vyumba vya kawaida vya malazi, watu wengi wamekuwa wakizipendelea, kwani zinampa mtu uhuru hata wa kujipikia.
Katika kile kimeonyesha umaarufu wake, biashara hiyo imechangamkiwa na wafanyabiashara wengi wa vyumba vya malazi katika maeneo ya mijini kama Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru kati ya mingineyo.
Jijini Nairobi, biashara hiyo imeibukia maarufu sana katika mitaa ya kifahari kama vile Kilimani, Kileleshwa, Lavington kati ya mingine.
Licha ya majumba hayo kuibukia kuwa maarufu, yameanza kugeuka kuwa majukwaa ya uasherati, uzinzi, matumizi ya mihadarati na hata madai ya mauaji.
Hili linafuatia mauaji tata ya mwanadada Starlet Wahu anayesemekana alikumbana na mauti katika chumba kilichodaiwa kuwa Airbnb mnamo Januari 3 mwaka huu, 2024 katika mtaa wa South B, jijini Nairobi.
Hata hivyo, kampuni ya AirBnB ya Amerika imekanusha kwamba chumba hicho hakikuwa kimesajiliwa chini yake.
Kwenye kisa hicho, ripoti zilieleza kuwa marehemu aliandamana kwenye chumba hicho na mwanamume aliyetambuliwa kama John Matara.
Polisi bado wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo, mshukiwa akingoja kufikishwa mahakamani.
Tukio la pili lilitokea Jumapili alfajiri, Januari 14, 2024 ambapo mwanamke wa umri wa miaka 24 alipatikana ameuawa katika hali tatanishi kwenye chumba aina hiyo eneo la Roysambu, Kaunti ya Nairobi.
Polisi waliofika katika eneo la mauaji hayo walitoa tahadhari kwamba lazima wale wote wanaoendesha biashara hiyo waweke kamera za siri – CCTV, ili kuhakikisha kuwa zinanasa na kurekodi shughuli zote zinazoendelea.
Kulingana na polisi, hilo litawasaidia kunasa mtu yeyote anayejihusisha kwenye maovu ya aina yoyote ile.
Kutokana na visa hivyo viwili, baadhi ya Wakenya wameeleza hofu yao kwamba kuna uwezekano mkubwa wa maovu mengi ambayo yamekuwa yakiendelea kwenye nyumba hizo bila kubainika.
Kulingana na Bi Mary Mungai, ni wakati serikali ichukue hatua za kutosha kulainisha uendeshaji wa biashara hiyo, la sivyo maovu mengi yataendelea bila kubainika.
“Mimi nilikuwa nikiendesha biashara hiyo katika mtaa mmoja jijini Nairobi. Hata hivyo, niliisimamisha kutokana na maovu niliyokuwa nikiyaona yakiendeshwa katika nyumba hizo na watu tuliowakodisha. Wengi walikuwa raia wa kigeni. Baadhi yao walitumia nyumba hizo kuendesha uasherati na wanawake tofauti kutoka humu nchini,” akasema Bi Mungai.
Kauli kama hiyo ilitolewa na Bw James Matagaro, ambaye pia aliwahi kuendesha biashara hiyo.
“Ina mapato mazuri, ila lazima serikali iweke mikakati ya kutosha kuilainisha,” akasema.