Maana ya Jowi! Jowi! zilizotanda kufuatia kifo cha Raila
PUNDE tu baada ya habari kuhusu kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kauli za “Jowi! Jowi! Jowi! zilitolewa na wakazi wa mtaa wa Kibra, Nairobi, nyumbani kwake Bondo na maeneo kadhaa ya Luo Nyanza wakiomboleza kifo chake.
Nyakati za uhai wake, ilikuwa ni ada kwa mwendazake kuomboleza watu mashuhuri kwa kutoa kauli ya “Jowi! Jowi! huku akipeperusha mgwisho (fly whisk); “orengo” kwa dholuo.
Kwa mfano, Februari 12, 2020, wakati wa mazishi ya rais wa pili nchini Hayati Daniel Arap Moi nyumbani kwake Kabarak, Nakuru, Odinga alizua kioja alipowasili kwa kishindo akiimba Jowi! Jowi! Jowi! akielekea kwenye jeneza la Moi kabla ya kutoa heshima zake akipeperusha mgwisho.
Katika mila na tamaduni za jamii ya Waluo, neno “Jowi” linarejelea Nyati, mnyama anayefahamika kwa sifa zake za ujasiri na nguvu na ukakamavu.
Ndiposa, katika jamii hii, nyati hunasibishwa na mjasiri, mwenye nguvu na ushawishi mkubwa kijamii na kisiasa; sifa ambazo Odinga alikuwa nazo wakati wa uhai wake.
Nyimbo za “Jowi! Jowi!” zinatarajiwa kuendelea kutanda nyumbani kwa Odinga, Opoda Farm, Bondo, na maeneo mengine ya Luo Nyanza wakati huu wa waombolezo na siku ya mazishi.