Makala

MABADILIKO: Mike Tyson mkulima hodari wa bangi baada ya kustaafu ndondi

May 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MIKE Tyson alikuwa bondia shupavu enzi zake katika uzani mzito.

Baada ya kuangika glavu zake mwaka 2005, Mwamerika huyu bado anakumbukwa kwa mchango huo wake kwenye masumbwi. Amejishughulisha pia na uigizaji wa filamu na usemaji.

Alitangaza majuzi kuwa huenda akarejea ulingoni hivi karibuni kwa pigano la maonyesho ya kuchangisha fedha kusaidia wenye shida.

Kwa sasa, hata hivyo, Tyson, 53, ameamua kuwa shughuli inayompendeza ni ukulima wa bangi katika jimbo la California.

Tangu mwaka 2016 mmea huo ulipohalalishwa katika jimbo hilo, Tyson anayefahamika kwa jina la utani kama “Baddest Man on the Planet”, amezamia ukulima wa mmea huo katika ekari 40.

Tyson, ambaye anashikilia rekodi ya kuwa bondia aliyepata ubingwa wa dunia wa uzani mzito akiwa na umri mdogo zaidi (alishinda taji la WBC mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 20), ana jumla ya ekari 418 ya shamba analoliita Tyson Ranch.

Vyombo vya habari nchini Marekani vimeripoti kuwa anajenga mahali maalum pa watalii katika ranchi hiyo ya bangi. Anatumai pia jumba hilo litatumika kuandaa tamasha za muziki. Litakuwa na bwawa la kuogelea la aina ya mto (lazy river).

Mbali na hoteli hiyo ya kifahari, Tyson analenga kuwa na Chuo Kikuu katika eneo hilo kitakachotoa mafunzo kwa wakulima wa bangi na watu wanaotaka kuingilia upanzi wa mmea huo.

Tyson, ambaye enzi zake kama bondia hakukosa utata ikiwemo kumuuma Evander Holyfield masikio katika pigano la mwaka 1997 na pia kufungwa jela kwa ubakaji mwaka 1992, anasemekana anavuna Sh53.6 milioni kila mwezi kwa kuuza mmea huo, ambao ni haramu nchini Kenya. Tyson mwenyewe huvuta bangi ya Sh4.3 milioni kila mwezi akiwa na marafiki na mashabiki anapowaalika katika kipindi chake cha Hotboxin’ With Mike Tyson. Anapata mapato pia kutokana na kipindi hicho cha intaneti.

Licha ya kujipata katika upande mbaya wa sheria mara si haba, Tyson anasalia kuwa mmoja wa mabondia maarufu duniani.

Tyson, ambaye alishinda mapigano 50 (44 kwa njia ya kuwalambisha sakafu wapinzani) na kupoteza manne, alivuna fedha nyingi akishiriki ndondi za malipo.

Inaaminika alivuna Sh73.4 bilioni akiwa bondia. Hata hivyo, kama wanamichezo wengi, Tyson alipoteza mali yake nyingi. Mwaka 2003, alitangaza kufilisika akijilaumu kwa kuharibu mali hiyo kwa kuishi maisha ya anasa.

Mashabiki 18, 187 walihudhuria pigano la marudiano kati ya Tyson na Holyfield mwaka 1997 katika ukumbi wa MGM Grand. Fedha zilizokusanywa langoni kuingia katika ukumbi huo, ni Sh1.8 bilioni. Tyson alituzwa Sh3.2 bilioni naye Holyfield aliyeibuka mshindi akatia mfukoni Sh3.7 bilioni. Itakumbukwa Tyson alipigwa marufuku ya mwaka mmoja na kutozwa faini ya Sh321.7 milioni kwa kuuma masikio ya Holyfield.

Tyson alipata watoto saba kutoka ndoa zake tatu. Mmoja wa watoto hao kwa jina Exodus Tyson aliaga dunia mwaka 2009 katika ajali ya tredimili.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wealthy Gorilla, Tyson amesalia na mali ya Sh321.7 milioni pekee baada ya kupoteza nyingi kwa anasa ikiwemo kucheza kamari.

Itakumbukwa akiwa bondia alimiliki kasri lenye vyumba 52 mjini Connecticut, ambalo aliuzia mwanamuziki 50 Cent kwa Sh353.9 milioni mwaka 2003. Wakati huo, Tyson alikuwa na madeni ya Sh1.8 bilioni.