Makala

Madai mapya yafichuka kuhusu ulanguzi wa figo katika Hospitali ya Mediheal

Na LEON LIDIGU April 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANACHAMA mmoja wa jopo la serikali lililochunguza upandikizaji wa figo wenye utata katika Hospitali ya Mediheal, amedai kuwa ripoti yao ilifanyiwa marekebisho makubwa ili kuficha ushahidi wa ukiukaji wa sheria, na hivyo kuzua maswali mapya kuhusu ulanguzi wa viungo vya binadamu nchini.

Ripoti hiyo, iliyoandaliwa na jopo la watu 12, ilibaini kuwepo kwa mienendo ya kutiliwa shaka kuhusu ulanguzi wa figo, likiwemo jina moja lililoonekana mara kwa mara kama jamaa wa wahisani na wapokeaji wa figo — wote wakiwa raia wa kigeni.

Hata hivyo, licha ya ushahidi huo, ripoti hiyo ilihitimisha kuwa “hakukuwa na ushahidi wa kutosha” na badala yake ikapendekeza uchunguzi zaidi.

Lakini kwa mujibu wa Dkt Philip Cheptinga, daktari mtaalamu wa figo na mwanachama wa jopo hilo, wao watatu walijiondoa katika hatua za mwisho za maandalizi ya ripoti hiyo baada ya kuamriwa kufuta baadhi ya matokeo ya msingi.

“Tuliambiwa kutoka juu, kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Afya kwamba tunapaswa kufuata maagizo na kuficha baadhi ya mapendekezo. Hatukukubaliana na hilo, hivyo tukajitoa,” alisema Dkt Cheptinga.

Kwa mujibu wa Dkt Jonathan Walla, Rais wa Chama cha Madaktari wa Figo (KRA), jopo hilo lilikuwa limegundua kuwa Waisraeli watatu walipokea figo ambazo tayari zilikuwa hazifanyi kazi. Pia, aliunga mkono madai kuwa baadhi ya wahisani walikuwa vijana maskini wa Kenya waliolaghaiwa kuuza figo zao kwa kati ya Sh200,000 hadi Sh700,000.

Katika kipindi cha miezi mitatu ya mwaka huu pekee, hospitali hiyo imeripotiwa kufanya zaidi ya upasuaji 18 wa figo, wengi wa wapokeaji wakiwa kutoka mataifa ya Mashariki ya Kati, Ulaya ya Mashariki na Asia.

Ripoti ya runinga ya kimataifa ya DW TV pia ilieleza jinsi kampuni moja ya kimataifa ya Israeli inavyoshirikiana na Mediheal kuchukua figo kutoka vijana wa Kenya na kuwauzia wagonjwa Ulaya kwa zaidi ya Sh3 milioni, huku mhisani akilipwa chini ya Sh300,000.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Hospitali ya Mediheal, Dkt Swarup Mishra, alikanusha vikali madai hayo, akisema, “Kwa jina la Mungu, hatujawahi kuchagua mhisani wala kumlipa yeyote kwa figo. Hizi ni siasa na fitina.”

Lakini KRA na mashirika mengine kama Renal Patients Society of Kenya (RPSK) yanasema hatua za dharura zinahitajika. “Tunaangamiza mfumo mzima wa uchangiaji wa viungo kwa uhalifu huu. Tunahitaji mjadala wa kitaifa kuhusu mchango wa figo kutoka kwa watu waliokufa kutokana na ajali au kwa njia ya kisheria,” alisema Bw John Gikonyo, rais wa RPSK.

Huku Waziri wa Afya, Aden Duale, akiapa kuanzisha uchunguzi mpya, wadau wengi wanahofia kuwa kashfa hii inaweza kuathiri vibaya imani ya umma kwa sekta ya afya, huku baadhi ya wagonjwa wa figo wakihofia kuchangia viungo vyao kwa sababu ya hofu ya kufanyiwa ulaghai.