Madiwani waepuka mijadala ya aibu, wakazi wengi wakihudhuria vikao
NA KALUME KAZUNGU
BUNGE la Kaunti ya Lamu miaka ya hivi karibuni limeshuhudia idadi kubwa ya wananchi wanaojitokeza kuhudhuria na kufuatilia vikao vya mijadala ya madiwani ndani ya majengo hayo ya bunge.
Kinyume na awali ambapo ni wananchi wasiozidi 10 pekee ambao wangefika kufuatilia mijadala ya madiwani, kumeshuhudiwa ongezeko la umma unaofika bungeni, hasa tangu majengo mapya ya bunge la Kaunti ya Lamu kukamilika mjini Mokowe.
Majengo hayo ya bunge yalijengwa kwa kima cha Sh214 milioni.
Awali, Bunge la Kaunti ya Lamu lilikuwa likifanya vikao vyake kwenye ukumbi wa kijamii wa Manispaa ya Kaunti ulioko kisiwani Lamu.
Ukumbi huo haukuwa na nafasi ya kutosha kuuwezesha umma kuhudhuria kwa wingi vikao vya mijadala ya madiwani bungeni.
Majengo ya sasa ya bunge mjini Mokowe aidha yako na nafasi tele za wananchi kufika kufuatilia vikao vya bunge.
Kulingana na Afisa wa Itifaki na Uhusiano Mwema wa Umma Katika Bunge la Kaunti ya Lamu, Bw Hussein Miji, Bunge la sasa la kaunti hiyo liko na nafasi chungu nzima kwani lina uwezo wa kupokea kati ya wananchi 150 na 200 kwa awamu moja.
Hiki ni kinyume kabisa na majengo ya awali ya bunge la kaunti ya Lamu yaliyoko kisiwani Lamu kwani nafasi iliyotengewa umma ilitosheleza kati ya wananchi 25 hadi 30 pekee.
Ni kutokana na hilo ambapo kila kunapofanyika mijadala bungeni, wananchi wengi zaidi wamekuwa wakihudhuria na kufuatilia vikao vya madiwani wao, wakijua fika kuwa kuna nafasi ya kuwatosha wao kuketi kufuatilia vikao husika.
Jengo hilo la kifahari mjini Mokowe pia limekuwa likiwavutia wengi kuingia ndani ilmuradi angalau waonje utamu wake wakati mijadala ikiendelea.
“Twashukuru kwamba bunge la sasa lina nafasi chungu nzima iliyotengewa umma. Isitoshe, tumetundika skrini kila mahali ili kuwawezesha hata wale ambao wako maeneo wasikoweza kuwaona madiwani wetu moja kwa moja wakijadili miswada pia wafuatilia kwenye skrini hizo. Hali ni shwari bungeni,” akasema Bw Miji.
Mbali na kuwepo kwa nafasi tele na ufahari wa jengo, kigezo kingine kikuu kinachowachochea wananchi kuhudhuria vikao bungeni ni madiwani wa kaunti ya Lamu kuepuka mijadala ya aibu na kuweka zingatio kwa mijadala ya kuisogeza kaunti mbele.
Utapata kwamba baadhi ya vikao vya siku za nyuma, hasa vile vya kati ya mwaka 2013 na 2017, mara nyingi vilikuwa vikijadili mambo madogomadogo.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa na Taifa Leo walisema wao hupendezwa na jinsi madiwani wa Lamu wa miaka ya sasa wanavyojikita sana katika kuangazia mijadala ya maendeleo na yenye uzito.
Bw Athman Salim, alisema kinyume na miaka ya awali ambapo hoja zilizojadiliwa bungeni zilikuwa za kimzahamzaha, kwa sasa inafurahisha na kuridhisha kuona madiwani wakijikaza kujadili masuala yanayomnufaisha mwananchi au jamii, hasa kimaendeleo.
“Zamani hatukupendelea jinsi mijadala ya kimzahamzaha ilivyosheheni bungeni. Unafika bungeni na kupata madiwani eti wakijadili hoja kuhusu kupiga marufuku minisketi (vimini) au hoja ya kumuondoa gavana mamlakani au kiongozi huyu na yule. Hili halikuturidhisha kamwe. Na ndio sababu mara nyingi ungepata umma bungeni ukiwa ni watu watatu au 10 pekee wakifuatilia mijadala hiyo ya kivivihivi tu,” akasema Bw Salim.
Baadhi ya miswada na sheria zinazonuia kuleta maendeleo ya kupigiwa mfano ambazo zimepitishwa miaka ya hivi punde bungeni Lamu ni pamoja na ule wa kutengwa kwa mfuko wa hazina ya maendeleo kwa vijana katika kaunti ya Lamu. Mswada huo ulipitishwa mwaka 2022.
Bunge la Lamu pia tayari limepitisha au kuidhinisha mswada wa Masuala ya Kukabiliana na Majanga ya Dharura, ule wa leseni za kibiashara kwa wafanyabiashara wa Lamu, Sheria ya Masuala ya Maradhi ya Saratani na Jinsi ya Kukabiliana nayo, na Mswada wa Masuala ya Elimu ya Chekechea (ECDE) miongoni mwa mingine.
Bunge la Kaunti ya Lamu linaongozwa na Spika Azhar Ali Mbarak akisaidiwa na Diwani wa Wadi ya Mkunumbi Bw Paul Kimani Njuguna ambaye ndiye Naibu Spika.
Bunge hilo linajumuisha madiwani waliochaguliwa 10 na wale wa maalum wanane (8).