Maeneo haya ni hatari kwa mizozo ya ardhi
KISA cha hivi karibuni katika Angata Barrikoi, Trans Mara Kusini, Kaunti ya Narok, ambapo wakazi sita walipigwa risasi na kuuawa na polisi, kimeangazia maeneo ambayo huathiriwa mara kwa mara na ghasia zinazotokana na mizozo ya ardhi ya muda mrefu.
Kisa hicho kilitokea baada ya maafisa wa serikali kwenda kugawa kwa nguvu ardhi inayozozaniwa, huku kukiwa na madai kwamba wanasiasa wenye ushawishi walikuwa wamenyakua sehemu ya ardhi hiyo.
Mbunge wa Emurua Dikirr, Johana Ng’eno, alinaswa kwenye video akiunga mkono wakazi na kuwalaumu maafisa wa serikali kwa kupuuza agizo la mahakama lililositisha mipango ya kuwafurusha wakazi.
Mizozo ya aina hii haipo tu Angata Barrikoi. Hapa chini ni baadhi ya mifano mingi nchini Kenya:Mnamo Mei 6, Rais William Ruto aligawa ekari 6,000 zaidi za Ranchi ya Kedong kwa jamii ya Wamaasai katika Kaunti ya Narok.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa serikali kupanua umiliki wa ardhi kwa wenyeji.Ranchi hiyo kubwa ambayo pia inahifadhi miundombinu muhimu kama Bandari Kavu ya Naivasha imekuwa ikizozaniwa kwa muda mrefu.
Rais Ruto aliahidi kuwa walengwa wa ardhi hiyo watapokea hatimiliki ndani ya wiki moja.Wiki hii, Rais Ruto alitangaza kuwa serikali imeanza mazungumzo ya kununua ardhi hiyo ili kupatia makazi familia 600 zilizopo Sogoo na 13,500 waliotimuliwa Mau.
Familia ya aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Nyanza, Isaiah Cheluget, imekuwa ikishinda kesi mbalimbali mahakamani kuthibitisha inamiliki ardhi hiyo.
Katika Murang’a, maeneo hatari ni pamoja na Mbo-I-Kamiti, Samuru Gituto, Kagaa, Muthanga, Nanga Kihoto, Mwireri Mukia, Mithini, na Kihiu Mwiri.
Kuna kundi la watu wenye ushawishi wanaoshirikiana na maafisa wa serikali, mawakili na mabroka kulaghai wenyehisa wa ardhi za makundi haya. Zaidi ya watu 100 wameuawa Kihiu Mwiri kwa miaka 20 iliyopita.
Aprili 23, 2023 watu wawili walipigwa risasi katika mzozo wa ardhi ya ekari 1,500 huko Kampi Ways, Chepchoina. Mwaka 2014, watu sita waliuawa walipojaribu kuwafurusha wakazi wa shamba la Mengo.
Aprili 2024, wengine watatu walijeruhiwa katika Mowlem, Endebess.Ekari 54,000 za ardhi ya Mwea Trust zimekuwa kwenye mzozo wa muda mrefu baina ya jamii za Mbeere, Embu, Kamba, na Kirinyaga. Mwaka 2019 mtu mmoja aliuawa na wengine sita kujeruhiwa.Mpaka wa Nkararo-Enoosoen umekuwa chanzo cha umwagikaji wa damu kati ya koo mbili tangu 1974.
Serikali ililazimika kuingilia kati mwaka jana kwa kupima na kuweka mipaka rasmi.Kamishna wa Bonde la Ufa, Abdi Hassan, alishtumiwa kwa kuingilia mzozo wa ekari 2,600 katika Njoro kati ya Mosem Enterprises na Chuo Kikuu cha Egerton.Watu walikamatwa, mmoja akapigwa risasi, na jamii ikalalamikia upendeleo wa maafisa wa serikali kwa chuo kikuu.
Kanisa Katoliki la Voi lilipewa kibali cha kuwatimua wanyakuzi waliokuwa wamevamia ekari 40 za ardhi. Mahakama ya Ardhi na Mazingira iliamuru walipwe fidia ya Sh500,000 kwa uharibifu wa mali.
Katika mpaka wa Kisumu na Nandi, familia ya mwanamuziki marehemu Achieng Abura ilishinda kesi dhidi ya kampuni ya Usonik Farm Purchase. Mahakama iliamuru kampuni hiyo lipe fidia ya Sh30 milioni na kuondoka kwenye ardhi hiyo.
Huko Taita Taveta, Jaji Edward Wabwoto alikataa kubatilisha uamuzi wa awali ulioipa kampuni ya Teita Estate Sisal Ltd umiliki halali wa zaidi ya ekari 16,930, jambo lililowaacha wananchi bila matumaini ya kurejeshewa ardhi.
Na huku Kisauni, kaunti ya Mombasa, wakazi zaidi ya 1,200 walioko kwenye ekari 341 wamo hatarini kufukuzwa baada ya serikali kukataa kulipa fidia ya Sh1.7 bilioni kwa kampuni ya Mainland Properties Ltd. Mahakama iliagiza serikali na wakazi kujadiliana na kampuni hiyo kupata suluhu ya kudumu.