• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
‘Maeneo kame yanaweza kugeuzwa ya uzalishaji chakula’

‘Maeneo kame yanaweza kugeuzwa ya uzalishaji chakula’

Na SAMMY WAWERU

KATIKA maeneo kame, njaa inaweza ikawa historia serikali ikijitolea kupiga jeki sekta ya kilimo.

Iwapo inamudu kusafirisha mafuta kutoka mjini Mombasa hadi Busia, ni wazi maji yanaweza kuchukua mkondo huo kutoka maziwa yaliyomo nchini na hata Bahari Hindi.

Kilimo

Sekta ya kilimo imegatuliwa chini ya katiba inayotumika kwa sasa, iliyoidhinishwa 2010 na kuanza kutumika 2013.

Katika usomaji wa makadirio ya bajeti kila mwaka serikali kuu hutoa mgao kwa sekta ya kilimo na serikali za kaunti.

Fedha wanazopokea kwa nini zisitumike kusafirisha maji kwa njia ya mifereji hadi maeneo kame?

Magavana wanadai mgao wanaopokea hautoshi kuendesha serikali za ugatuzi, kiasi kikubwa kikielekezwa kwa watumishi wao.

Tume ya kuainisha na kusawazisha mishahara ya watumishi wa umma (SRC), imekuwa ikishauri magavana kupunguza mzigo wa mshahara ikizingatiwa kuwa pesa wanazopata zinatoka mfukoni mwa mlipa ushuru.

Mlipa ushuru huyu ndiye yule yule anayekufa njaa.

Viteka maji

Ingekuwa bora iwapo wangeyapa kipau mbele maslahi ya mwananchi. Maslahi ya mwananchi ni kuimarisha sekta ya kilimo, ambacho ni kapu la lishe ya taifa.

Zaraa ndiyo uti wa mgongo wa nchi hii, na ulimwengu kwa jumla.

Kando na kusafirisha maji maeneo kame kwa mifereji, uchimbaji wa mabwawa na vidimbwi, ni miongoni mwa njia za kutegua kitendawili cha upungufu na ukosefu wa chakula.

Vihifadhi hivyo vitateka maji msimu wa mvua, ambayo yatatumika kufanya kilimo na msimu wa kiangazi.

“Msimu wa mvua, hasa ya masika, maji mengi hupotea. Yangetekwa na mabwawa na vidimbwi ili yatumike kufanya kilimo na matumizi mengine nyumbani wakati wa kiangazi,” anasema Kipruto Arap Kirwa, ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri wa Kilimo serikali ya Rais (mstaafu) Mwai Kibaki.

Kuna baadhi ya wakulima ambao wamefanikiwa kuzalisha chakula wakati wa kiangazi, kwa kutumia mfumo wa kunyunyizia maji mashamba kwa mifereji.

Mwae Malibet, huhifadhi maji kwenye matenki msimu wa mvua na huyatumia kukuza mimea mbalimbali. “Shamba langu wakati wa mvua na kiangazi halikosi mazao. Hutumia mfumo wa mifereji kunyunyizia mimea maji,” asema Bw Mwae ambaye ni mkulima eneo la Gachie, Kiambu.

Baadhi ya maeneo Turkana na Mandera yana viunga vya kilimo kufuatia uhifadhi wa maji kupitia mabwawa na vidimbwi. Yanayoshuhudia ukame yanaweza kufuata mkondo huo serikali ikiitikia kuyapiga jeki kwa kuchimba mabwawa na vidimbwi. “Wanachohitaji ni maji pekee, watatue shida za njaa. Serikali itilie mkazo miradi ya kuchimba mabwawa,” ahimiza Mwae.

Mpango wa kuchimba mabwawa unaonekana kutatizwa na kero la ufisadi. Mradi wa bwawa la Kimwarer na Aror, kaunti ya Elgeyo Marakwet Sh21 bilioni zimeripotiwa kubadhiriwa. Ikiwa serikali itazima suala la ufisadi, huenda mipango ya kufanikisha usalama wa chakula nchini utaafikiwa.

  • Tags

You can share this post!

Mafisadi, ‘hata wawili tu’ watupwe jela liwe...

Waliobwagwa 2017 wasubiri kujaribu bahati 2022 –...

adminleo