Makala

Mafuriko: Mtambo unaofungua mikondo ya maji iliyozibwa

May 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SAMMY WAWERU Na LABAAN SHABAAN

HUKU sehemu nyingi nchini zikiendelea kushuhudia athari za mvua kubwa, mifumo kupitisha maji imezibwa na taka zilizosombwa.

Mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa barabara na makazi.

Uvumbuzi wenye ubunifu unahitajika ili kukabili hatari hii.

Kampuni ya ujenzi, Bainridge Construction Company, ambayo ina utaalamu katika nyanja za ujenzi na uhandisi wa majengo inaongoza katika kukabili changamoto za mfumo wa kupitisha maji na unyunyizaji maji mashambani.

Paul Kairigi, mwasisi Bainridge Construction, kampuni yenye mtambo wa Watermaster unaoweza kufungua mikondo ya maji iliyozibika. PICHA|SAMMY WAWERU

Kwa kutilia mkazo usimamizi wa rasilimali na uboreshaji wa miundombinu, kampuni hii hutumia teknolojia ya kisasa kukabili matatizo kama vile mkusanyiko wa udongo mwingi kwenye mikondo ya maji.

“Tuna mtambo wa kuzibua mifumo ya mifereji ya maji iliyozibwa,” anaeleza mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni hiyo Paul Karigi.

Vile vile, Bainridge iko katika mstari wa mbele kuvumbua suluhu ya kibunifu kwa wakulima.

Kwa mfano, mtambo wa Watermaster husaidia katika uondoaji wa mkusanyiko wa udongo kwenye maji.

Kwa hivyo teknolojia hii ni kimbilio kwa wanaoathiriwa na mvua kubwa inayosababisha mafuriko.

Vifaa vilivyobuniwa husaidia kupunguza athari katika mito iliyofurika, barabara na miundomsingi ya uchukuzi.

Nchini Kenya na kwingineko, miradi ya umwagiliaji maji mashambani hukabiliwa na vizingiti vikubwa kutokana udongo mwingi kuziba mifereji ya maji.

Daraja linalounganisha mtaa wa Zimmerman na Githurai 44, ambalo limefurika kufuatia mikondo kadha kuzibika. PICHA|SAMMY WAWERU

Udongo huu husombwa na maji yanayotiririka na kusafirishwa kupitia mikondo ya maji kama vile mito na mitaro.

Kukwama kwa mifumo ya kupitisha maji katika miji mingi ni changamoto kubwa katika msimu wa mvua kubwa inayosababisha mafuriko nchini.

Mafuriko ambayo nchi inakabiliana nayo, aghalabu hushuhudiwa katika maeneo ya miji na kuvuruga shughuli za maisha.

Kulingana na Bw Karigi, kubuniwa kwa mitambo ya kuzibua mikondo ya maji iliyokwama kutasaidia kukabili matatizo haya.

Mkondo wa majitaka eneo la Zimmerman, Nairobi uliokaribia makao ya watu ambao umeathirika na mafuriko yanayoendelea. PICHA|SAMMY WAWERU

“Endapo hali hii haitadhibitiwa, mfumo wa kilimo utaathirika pakubwa,” anaonya.

Na kadri muda utakavyozidi kupita bila hatua kuchukuliwa, shughuli za uzalishaji chakula zitasambaratishwa na athari za mafuriko.

Utegemezi wa kilimo kinachostawi kwa kutumia mvua, pamoja na athari za mabadiliko ya hali ya hewa (mabadiliko ya tabianchi), ni kichochea kutafuta suluhu endelevu.

“Bainridge inashughulikia changamoto hizi kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu. Vifaa hivi hufanya kazi pale ambapo mashine za kawaida zimeshindwa kuondoa udongo na uchafu katika vyanzo na mikondo ya maji kama vile mabwawa na mito,” anafafanua Karigi.

Nyumba iliyofurika eneo la Zimmerman, kufuatia mkondo wa maji kuzibika kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa nchini. PICHA|SAMMY WAWERU