• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Mafuriko yalemaza shughuli katika baadhi ya maeneo Nakuru

Mafuriko yalemaza shughuli katika baadhi ya maeneo Nakuru

Na PHYLLIS MUSASIA na KEVIN ROTICH

WAKAZI wa Kiamunyi na baadhi ya sehemu za Bahati, Kaunti ya Nakuru, wameendelea kukadiria hasara kubwa baada ya maeneo hayo kukumbwa na mafuriko kufuatia mvua inayoendelea kunyesha.

Katika eneo la Kiamunyi, mvua ilioanza kunyesha mwendo wa saa kumi na moja jioni Jumatano ilisababisha mafuriko ambapo maji yaliingia katika nyumba za wakazi na hata katika maduka ya kufanyia biashara.

Shughuli nyingi zilikwama baada ya maji kujaa ndani ya nyumba hizo huku nguo, malazi na mali nyinginezo zikiloa maji.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo wamesema mafuriko hayo yamesababishwa na ukosefu wa mitaro maalumu ya majitaka huku wengine wakikashifu mradi wa kilimo unaoendeshwa na raia mmoja wa kigeni katika Madrugada Garden kwa kutumia njia mbovu ya unyunyuzaji maji mimea bila kuzingitia mbinu kamili inayohitajika.

“Licha ya maeneo haya kukosa mitaro ya kupitisha maji ya mvua, kunaye raia mmoja wa kigeni ambaye anaishi upande wa juu wa sehemu hii. Anafanya kilimo lakini mbinu anayotumia si inayofaa,” amedai Bi Grace Mwanda, mmoja wa wakazi wa Kiamunyi.

Kulingana na Bi Mwanda, kila wakati kunaponyesha kuna mitaro ya maji ambayo imetengezwa kutoka kwa shamba la raiya huyo ambayo huelekeza maji kwenye sehemu ya chini wakoishi mamia ya wakazi wengine.

“Bila kujali kuwa kuna watu wengi ambao wanaishi sehemu ya chini na unapata kwamba maji hayo yanakosa kufuata mkondo mmoja na kuingia ndani ya nyumba zetu na hata sehemu za maduka ambayo tunafanyia biashara,” ameongeza Bi Mwanda wa kughadhabika.

Mkazi mwingine Jeremy Lang’at amesema maji hayo ni hatari sana kwa afya ya wakazi hasa watoto ambao mara nyingi hulazimika kulala kwenye nyumba zilizojaa maji na baridi kali.

“Tumezidi kusikitika jinsi hali hii imeendelea kwa muda sasa bila serikali ya kaunti kufanya lolote. Ni wajimu wa viongozi tuliowachagua kuhakikisha kuwa hali afya zetu pamoja na usalama kwa jumla unatiliwa maanani,” amesema Bw Langa’t.

Ongezeko la mvua kubwa katika Kaunti ya Nakuru pia imesababisha maeneo ya mabanda kwenye sehemu ya chini ya Nakuru Magharibi kama vile Kaptembwa, Kwa Ronda, Ponda Mali na sehemu nyinginezo kushuhudia mafuriko.

Katika maeneo ya All Nation kule Bahati, wakazi walishuhudia mafuriko kufuatia mvua ya Jumatatu, Jumanne na Jumatano.

Barabara zilizojaa maji husababisha msongamano mkubwa wa magari huku wanabodaboda pamoja na wale waliotumia njia ya miguu kutatizika pakubwa.

Wengi walionekana kutumia njia mbadala kama vile mikokoteni ili kuvuka ng’ambo ya pili.

Katika pitapita zetu, tunapata kina mama waliobeba watoto wakionekana pia kuyaweka maisha yao hatarini kwa kukalia mikokoteni isiyokuwa na vyuma vya kushikilia.

“Wanafunzi wengi wamekosa kufika shuleni kwa kuhofia kusombwa na maji barabarani. Biashara pia imekwama na hatujia jinsi hali itakavyokuwa kufikia hapo kesho iwapo tatizo hili litazidi kushuhudiwa. Serikali yetu ya kaunti inapaswa kushughulika na kuhakikisha kuwa mitaro kamili inachimbwa sehemu hii yote ili kuzuia mafuriko zaidi,” ameeleza Bw Ng’ethe Mutai ambaye ni mkazi wa Bahati.

Wakazi hao hata hivyo wamekashifu vikali ahadi zisizokuwa na vitendo ambazo washikadau wakiwemo wanasiasa, maafisa wa Halmashauri ya Barabara kuu nchini (KeNHA) pamoja na maafisa wa kaunti wamekuwa wakitoa kuhusiana na urekebishaji wa mitaro katika maeneo hayo.

“Wao husubiri kila mara tunapopata shida kama hii ndio unawaona wakija kutoa ahadi za uongo badala wafanye kazi inayoonekana,” amesema Bi Rosemary Wesonga huku akiongeza kuwa wakazi wamechoshwa na ahadi hizo duni.

Solai

Wakazi wa Kiamunyi hata hivyo wanalinganisha kile wanachokipitia kwa sasa karibia kuwa mkasa mkasa wa maafa ulioshuhudiwa Solai mwaka mmoja uliopita.

Baadhi yao wanasema wanahofia uhai wao na familia.

“Ikiwa serikali haitaingilia kati kuona kuwa raiya huyu wa kigeni anazungumziwa na kukanywa kuhusu jinsi anavyowachilia maji taka kutoka shambani mwake na kuyaelekeza kwenye makazi yetu, basi hatutakaa kwa amani bali kwa hofu kuwa huenda tukakumbana na maafa wakato wowote,” akaeleza mkazi mwingine John Kimani.

Takribani mwezi mmoja uliopita, maeneo ya Olive Inn na Kimunyi kwa jumla yalishuhudia mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha.

Wakazi wengi walilazimika kuhama makwao baada ya nyumba zao kujaa maji.

Wakulima pia walikadiria hasara yamamilioniya pesa baada ya mimea yao kusombwa na maji.

Mahidi, maharagwe, ngano na mboga zilihabiwa vibaya.

Wakati huo, mbunge wa eneo hilo Bw Rymond Moi alizuru sehemu zilizoathirika akiandamana na maafisa kutoka KeNHA.

Barabara za Kiamunyi zimeliwa na mmomonyoko wa udongo uliosababishwa na kukosekana mfumo mzuri wa kusafirisha majitaka. Picha/ Phyllis Musasia

Waliahidi kuwa serikali ya Nakuru itafanya na inafanya kila juhudi kuhakisha kuwa mafuriko hayo yanadhibitiwa upesi.

“Tunaomba mtulie na muwe pia wavumilivu kwa muda huu ambao serikali inajaribu sana kuhakikisha kuwa kila mmoja wenu anakaa vyema,” Bw Moi akawaeleza wakazi wa Kiamunyi walionekana kukerwa na jinamizi la mafuriko ya mara kwa mara.

Mnamo Aprili, waziri wa kaunti ya Nakuru anayeshughulikia sekta ya barabara na miundombinu Bi Lucy Kariuki alisema kuwa Sh345 milioni zilikuwa zimetengwa ili kurekebisha mitaro yamaji taka.

Hii ni baada ya maafisa  idara ya utabiri wa hali ya hewa kutoa ilani kwa wakazi wa Nakuru pamoja na serikali yake kuwa makini na kujitayarisha kwa mvua kubwa.

Bi Kariuki alisema kuwa sehemu mbalimbali kama vile Murogi, Kipkelion na barabara ya Mombasa zilikuwa zimepewa kipaumbele kwenye marekebisho hayo.

“Sh137 milioni zimetengwa kwa ajili ya kurekebisha mitaro na sehemu zote za kupitisha maji aka hasa katika mji wa Nakuru ili kuzuia mafuriko,’ akaeleza Bi Kariuki.

Aidha, aliongeza kuwa Sh200 milioni zilikuwa zimetengewa maeneo ya Naivasha na viungani mwake.

Sehemu za biashara katika eneo hilo pia ziliratibiwa kunufaika.

Eneo la Salgaa lilitengewa kitita cha Sh4 milioni kwenye mradi huo, pesa ambazo ziliratibiwa kurekebisha mitaro ya maji katika sehemu yenye umbali wa kilomita moja ya barabara hiyo. Maeneo mengine kama vile Mosop pia yaliratibiwa kiasi sawia cha pesa hizo.

  • Tags

You can share this post!

Jaguar kulala seli kwa siku ya pili

Mwangi Kiunjuri asema madai ya uhai wa Ruto kuwa hatarini...

adminleo