Magonjwa na ukatili wa kijinsia unavyowaathiri wanawake kimya kimya
Wanawake wamehimizwa kuinua sauti zao dhidi ya Ukatili wa Kijinsia (GBV), ikiwemo mauaji ya wanawake ambayo yamekithiri kote nchini, na pia kupigania ustawi wa afya yao kwa ujumla.
Katika Kongamano la siku tatu kuhusu Ustawi wa Wanawake, lililoandaliwa na Kanisa la Kitengela Presbyterian Church of East Africa (PCEA), wanawake wapatao 1,300 kutoka mji wa Kitengela na maeneo jirani walishiriki kujadili changamoto nyingi wanazopitia.
Kongamano hilo liliangazia afya ya wanawake kwa ujumla – kimwili, kiakili na kijamii – chini ya mada ” Kuunganisha Imani na Afya katika kumtumikia Mungu, Familia na Jamii.”
Kulingana na Mchungaji John Muhinyia, wa Parokia ya Kitengela, kongamano hilo liliandaliwa kutokana na changamoto nyingi ambazo wanawake wanapitia kimya kimya kote nchini, kuanzia ukatili wa kijinsia hadi magonjwa hatari yasiyo na dalili za wazi.
“Wanawake duniani kote wanapitia changamoto nyingi. Wengine huvumilia maumivu na fedheha kila mwezi wanapokamilisha mzunguko wao wa hedhi. Wengine huishi na wenzi wakatili, huku mamilioni wakikumbwa na unyanyasaji unaohusiana na matatizo ya uzazi,” alisema Mchungaji Muhinyia, akisisitiza umuhimu wa kuwa na jamii yenye afya bora.
Washiriki wa kongamano hilo, waliokuwa na umri wa kati ya miaka 30-50, walipata nafasi ya kuzungumza na washauri wa afya ya akili na wataalamu wa matibabu waliokuwa wameweka kambi ya huduma za afya bila malipo nje ya ukumbi wa Kanisa la PCEA Ebenezer.
Wataalamu wa afya walielimisha washiriki kuhusu magonjwa mbalimbali yakiwemo: Saratani (matiti na mlango wa kizazi) matatizo ya uzazi kwa wanawake na wasichana, afya ya akili, magonjwa ya moyo,magonjwa yanayohusiana na mzunguko wa hedhi na mfumo wa uzazi.
Katika mjadala, ukatili wa kijinsia ulijitokeza kama tatizo linalotesa wanawake wengi ndani ya familia zao. Wanawake walipewa wito wa “kupaza sauti zao – kuzungumza waziwazi” kuhusu ukatili huu.
“Utasa umeharibu ndoa nyingi. Wanaume mara nyingi huwalaumu wake zao. Jamii pia inamhukumu mwanamke katika ndoa. Mimi ni mwathirika wa miaka 10 ya unyanyasaji wa kimwili kutoka kwa mume wangu mlevi,“ alisema Jane (tumebana jina lake halisi ) wakati wa kongamano hilo.
Hata hivyo, Bonface Onsongo kutoka Equity Afya, tawi la Kitengela, alisema kuwa wengi wa wanawake waliopimwa walikuwa wakisumbuliwa na magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha kama vile unene kupita kiasi, kisukari shinikizo la damu, magonjwa ya akili yanayohusiana na msongo wa mawazo na wasiwasi, hasa kutokana na changamoto za gharama ya maisha.
Zaidi ya hayo, asilimia 15 ya wanawake waliopimwa waligundulika kuwa na vidonda vya tumbo pamoja na matatizo ya afya ya akili.

Zaidi ya wanawake 20 waligunduliwa kuwa na saratani ya matiti na ya mlango wa kizazi na walipewa rufaa kwa matibabu maalum. Wakati huo huo, wagonjwa 13 walihamishiwa Hospitali ya Karen kwa uchunguzi zaidi wa matatizo yao ya kiafya.
Dkt Dan Gikonyo, daktari wa magonjwa ya moyo na mwanzilishi wa Hospitali ya Karen, alikuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika kongamano hilo. Alieleza kuwa magonjwa ya moyo ndiyo chanzo kikuu cha vifo vya wanawake kote ulimwenguni.
Alibainisha kuwa kuna dhana potofu kuwa magonjwa ya moyo ni “magonjwa ya wanaume”, akiwahimiza wanawake kutafuta elimu kuhusu maradhi haya na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara hospitalini.
“Ni muhimu kwa kila mtu kuelewa hatari yake ya ugonjwa wa moyo, ikiwa ni pamoja na historia ya familia, shinikizo la damu, kiwango cha mafuta mwilini kisukari na uvutaji wa sigara,” alisema Dkt Gikonyo.
Aliwataka washiriki kuimarisha mshikamano wa kijamii, kushiriki uzoefu wao, kuunda vikundi vya msaada na kusherehekea mafanikio yao.
“Wanawake ndio moyo wa familia zetu, jamii zetu na nchi yetu. Kwa kuweka kipaumbele afya yako, unasaidia si tu maisha yako, bali pia unachangia ustawi wa vizazi vijavyo,” aliongeza.
Kongamano hili la afya na ustawi wa wanawake litakuwa tukio la kila mwaka na litafanyika katika parokia zote za Kanisa la PCEA kote nchini katika siku za usoni.