• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Magwiji kuzalisha maharagwe ya jadi

Magwiji kuzalisha maharagwe ya jadi

NA SAMMY WAWERU 

LIKIWA na miaka mitano tangu lianzishwe, kundi la Neema Farmers Community Garden linajivunia kuwa na mchango mkubwa katika sekta ya kilimo. 

Wadau wakiendelea kuhamasisha wakulima kukumbatia teknolojia na mbinu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (climate change), kundi hilo la kina mama linajituma kuhamasisha ukuzaji wa maharagwe asilia.

Florence Mutugi, mwenyekiti, anadokeza kwamba wanafanya kampeni ya kilimo cha maharagwe kama vile Mwitemania – maarufu kama Sura Mbaya, Noe – Jina lenye asili ya tabaka la Agikuyu (maharagwe ya rangi nyeupe na mengine yenye madoadoa meusi), na yale ya kukwea.

“Kimsingi, ni maharagwe yanayostahimili mikumbo ya kiangazi na ukame. Yanahitaji maji kiasi tu kuyanawirisha,” Florence anasema.

Neema Farmers Community Garden, ina makao yake Kirinyaga, na kando na orodha hiyo, pia inahamasisha ukuzaji wa Kawairimu – maharagwe mekundu, nyota, na pia yale ya manjano.

Wambui Nyaga, mwanachama, anasema mbali na uhamasisho wa urejeleo wa chakula cha jadi, wanahimiza tija za ukuzaji wa mazao pasi kutumia kemikali.

Florence Mutugi (kulia) na mkulima mwenza, ambao ni wanachama wa kundi la Neema Farmers Community Garden, wakitoa maharagwe kwenye makaka (pods). PICHA|SAMMY WAWERU

Wanajaribu kila wawezavyo kuhakikisha uhalisia wa maharagwe hayo unasalia, kwa kutumia dawa za kienyeji kukabiliana na kero ya wadudu na magonjwa.

“Aghalabu, tunatoa mafunzo kwa wanamemba kuhusu mbinu za kukabiliana na kero ya mimea, matumizi ya jivu na pia tunajiundia dawa asilia dhidi ya wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea,” Wambui anaelezea, japo anakiri mfumo huo si rahisi kwani una gharama zake.

Florence Murugi, anasikitika kwamba asilimia kubwa ya shughuli za kilimo nchini zinaegemea matumizi ya pembejeo, hasa mbolea na dawa zenye kemikali.

Hatua hiyo ni hatari, ikizingatiwa kuwa dawa zenye kemikali zinahusishwa na maradhi ya siha (lifestyle diseases).

“Tunapozungumza kuhusu afya bora, wengi wanadhania ni mjadala wa virutubisho faafu pekee. Ni muhimu kuwa makini jinsi chakula kinachotufikia mezani kinavyozalishwa, la sivyo tutaendelea kuwa mateka wa maradhi yanayohusishwa na afya,” asisisitiza.

Mseto wa maharagwe yaliyokuzwa na kundi la Neema Farmers Community Garden, Kaunti ya Kirinyaga. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, kundi hilo lina wanachama wasiopungua 30, Esther Mugure akiungama amefaidika pakubwa kulea familia yake changa.

Tunashibisha familia zetu na pia kujiendeleza kimapato na kimaisha, Esther anasema.

Shabaha ikiwa kufufua kilimo cha maharagwe asilia, Neema Farmers Community Garden imesaidia pakubwa katika uzalishaji wa mbegu kuendeleza kilimo chake.

“Kilo haipungui Sh350, tukilenga wakulima wenza,” Esther anaelezea.

Ikitegemea spishi, maharagwe huchukua kati ya siku 70 hadi 120, sawa na miezi mitatu, kukomaa.

Ni kutokana na mchango wa kundi hilo la kina mama katika sekta ya kilimo, lilipata fursa kushiriki Maonyesho ya Mbegu za Kiasili na Chakula cha Tamaduni za Kiafrika 2023, Makala ya Pili, yaliyoandaliwa na muungano wa Inter-Sectoral Forum on Agrobiodiversity and Agroecology (ISFAA).

Baadhi ya wanachama wa Neema Farmers Community Garden, Kirinyaga wakati wa Maonyesho ya Mbegu za Kiasili na Chakula cha Tamaduni za Kiafrika. PICHA|SAMMY WAWERU

ISFAA inaleta pamoja sekta za serikali na za kibinafsi katika kilimo, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, ya utafiti, na makundi ya wakulima kwa lengo la kilimo endelevu na kuboresha mazingira.

Kauli mbiu ya maonyesho hayo yaliyofanyika katika Makavazi ya Kitaifa – Kenya, Nairobi ilikuwa ‘Kuadhimisha Uhuru wa Chakula na Mbegu Nchini Kenya – Kufufua na kulinda Mfumo wetu wa Chakula na Kilimo huku tukikita Mizizi yetu, Kudumisha Mustakabali Wetu wa Kwanza’.

Mbali na maharagwe, Neema Farmers Community Garden pia inazalisha mseto wa mboga kuanzia za kienyeji kama vile murenda, managu (mnavu), saga, terere ndio mchicha, sukuma wiki, na spinachi.

Hali kadhalika, hulima mahindi ya rangi; manjano na mekundu, kilo moja ya mbegu za mboga Florence akisema inaanzia Sh600 nayo mahindi Sh500.

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Kindiki aonya magenge ya ujambazi Magharibi mwa Kenya

Trekta ndogo kivutio cha vijana kushiriki kilimo 

T L