• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Mahangaiko ya mama kulea mtoto aliyepooza ubongo

Mahangaiko ya mama kulea mtoto aliyepooza ubongo

NA FRIDAH OKACHI 

MAMA Bahati, mkazi wa Kawangware, Nairobi hana budi ila kumfanyia kila kitu mwanawe mwenye umri wa miaka 10 sawa na atunzavyo mtoto mchanga kwa sababu ya maradhi ya kupooza ubongo.

Carol Josephs Emoyo, 38, anasema kila unapowadia wakati wa kula hulazimika kumtafunia chakula ili aweze kutafuna.

Kulingana na nina, Bahati alianza kuugua maradhi hayo pindi tuu alipofikisha miezi sita baada ya kuzaliwa.

Kwa sasa hali yake imekuwa ni kumtegemewa mama yake kwa kila jambo.

Mwanawe huyu hawezi kufanya chochote.

Hawezi kujilisha mwenyewe; hawezi kutembea; hawezi kukaa, wala kuskia, mahangaiko haya yakiwa machache kuyaorodhesha, Mama Bahati akisalia kubeba mzigo wake mwenyewe.

Emoyo, mama wa watoto watatu ambaye anatatizika kulea mtoto huyo, kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Dijitali alielezea jinsi hufahamu mwanawe anahitaji kula.

“Kama mzazi Mwenyezi Mungu anakupa ufahamu kujua anahitaji kula. Kulingana na hali yake ya maumivu na dawa anazotumia, namtengea muda wake wa kula kama watoto wengine nyumbani,” akasema.

Kutokana na hali ya mwanawe, Emoyo, humtafunia chakula kiwe mwororo na laini ili aweze kumeza bila matatizo.

“Kutumia mashine ya kusaga pia huwa changamoto. Inabidi nitamfunie kuhakikisha anapata madini ya kutosha,” alisimulia Emoyo.

Kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa, mama huyu anasema haijakuwa rahisi kuwasiliana na mwanawe.

“Mawasiliano kati yangu naye yamekuwa ngumu kwa takriban miaka kumi na moja sasa. Ili kujua amefurahi hutoa sauti fulani, haswa wakati namkutanisha na watu,” aliongeza.

Mtoto aliyepooza ubongo, mzazi anapaswa kuwa karibu naye kila wakati.

“Kuwa mama wa mtoto kama huyu kunashirikisha mengi. Mzazi anapaswa kuwa na moyo wa kupenda,” Emoyo anahimiza wazazi wenye watoto wenye changamoto za aina hiyo.

Kulea mtoto wake mwenye mahitaji maalum nay a kipekee, anasema haijakuwa rahisi.

Mumewe alipofariki, mambo yaligeuka – kila saa ikawa ni kuwaza na kuwazua.

“Babake alijiingiza kwenye ulevi baada ya kugundua mtoto wake alipooza ubongo,” alisimulia, akionekana kusononeka.

Kabla kufariki, alijukumika kulipa kodi ya nyumba pekee, mahitaji mengine yakimwangukia.

Emoyo hutegemea vibarua vya kijungu jiko kukithi familia yake mahitaji muhimu ya kimsingi.

“Pesa kusaka matibabu hospitalini, ilibidi nifanye vibarua. Kwa sasa, mambo si rahisi,” alisema Emoyo.

Hana budi ila kuvalia njuga kiatu cha mama na baba.

Bahati anavyoendelea kukua, ndivyo mambo yanazidi kuwa mlima kukwea.

  • Tags

You can share this post!

Jackie Matubia: Wanawake Wakenya wanapenda wanaume wakorofi

Mwalimu mwanablogu Kisii alinyongwa – Upasuaji

T L