• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mahangaiko ya miaka 12 akingoja mumewe

Mahangaiko ya miaka 12 akingoja mumewe

Na GEORGE SAYAGIE

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 57 katika Kaunti ya Narok, amekuwa akiishi kwa mahangaiko kufuatia kutoweka kwa mumewe miaka kumi na miwili iliyopita bila kujulikana aliko.

Bi Jane Oluoch, ambaye ni mama wa watoto watano, amekuwa akiishi kwa matumaini akiamini kuwa siku moja yeye na watoto wataungana na mumewe Michael Olouch Onyango.

Wawili hao walikuwa wameoana kwa muda wa miaka 16, kabla ya mumewe kutoweka. Amekuwa akimtafuta kila mahali, lakini hajafanikiwa kumpata kufikia sasa.

Bi Oluoch, anayehudumu kama mtaalamu wa chakula katika Hospitali ya Rufaa ya Narok, alisema kuwa mnamo Oktoba, 6, 2007, alipokea ujumbe wa kuhofisha kutoka kwa mumewe.

“Nimeenda safari. Tafadhali watunze watoto wetu. Wafunze neno la Mungu. Liuze gari letu ikiwa sitakuwa nimerejea kufikia Jumatatu. Nitawasiliana nawe,” ulieleza ujumbe huo.

Tangu hapo, hajawahi kusikia ujumbe wowote kutoka kwake.

Alieleza kwa ghadhabu kwamba mumewe aliondoka ghafla, hata bila kutoa ujumbe wa alikokuwa akienda.

Wawili hao walioana mnamo 1986, kupitia harusi. Bw Onyango alikuwa akihudumu kama mtaalamu wa mashine za matibabu katika hospitali hiyo.

Siku aliyotoweka, Bw Onyango ambaye pia alihudumu kama dereva wa teksi, aliamka kama kawaida na kuelekea kazini mjini Narok.

“Baada ya hapo, aliegesha gari lake katika Kituo cha Petroli cha Kobil. Alizima simu yake na kumpa jirani yangu na kumwambia aniletee. Nilifahamu baadaye kwamba alienda Nairobi kuhudhuria mkutano wa Chama cha ODM akiwa na rafiki yake,” alisema.

Afahamu hali ni mbaya

Akizungumza na Taifa Leo mjini Narok, Bi Oluoch alisema kuwa alifahamu kwamba hali si nzuri, baada ya gari lao kuletwa nyumbani na dereva mwingine. Dereva huyo alisema kuwa alipewa gari hilo na Bw Oluoch, ambaye alimshauri kulipeleka nyumbani kwake kwani hangerejea.

Amesema kuwa amekuwa akimtafuta katika mochari na vituo mbalimbali vya polisi bila mafanikio yoyote.

“Hali yangu ilibadilika sana. Maisha yaligeuka kuwa magumu. Huwa ninahisi vibaya sana tangu mume wangu alipoondoka,” alisema

Alisema kuwa ugumu mkubwa aliopitia ni kuikimu familia yake na kuwasomesha watoto wake watatu katika vyuo vikuu bila usaidizi wa mtu yeyote. Vilevile, amekuwa akishughulikia matibabu ya msichana wake wa miaka 14, ambaye anaugua kifafa.

You can share this post!

Nyota wa Cranes wazidi kujaajaa kambi ya mazoezi

MWANAMKE MWELEDI: Sanaa i mishipani na azidi kuipa uhai

adminleo