Makala

Mahangaiko ya msichana shujaa aliyepigwa na stima akiokoa mbuzi aliyekwama

Na MERCY KOSKEI October 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA moja kutoka Baringo inalalamikia usimamizi wa Kampuni ya Umeme Nchini (KPLC) kwa kumtelekeza mwana wao ambaye alipigwa na stima Aprili 28 mwaka huu.

Sharon Kalalwa, nusura apatwe na mauti baada ya kupigwa na umeme uliokuwa kwenye mti wa stima uliokuwa umeanguka. Kalalwa ni mwanafunzi wa Gredi ya Pili katika Shule ya Msingi ya Cheseret.

Siku hiyo alikuwa akielekea shuleni aliposikiza mlio wa mbuzi ambaye alikuwa amefungwa. Alielekea kufungua mbuzi huyo kutokana na utu ndani yake lakini akakanyaga mti huo wa umeme na akapigwa na stima.

Waliosikia kilio chake walifika kumwokoa wakampata akiwa hali taabani lakini wakahofia kupigwa na umeme pia kisha wakawaita wahudumu wa KPLC.

Kwa mujibu wa walioshuhudia kisa hicho, wafanyakazi wa KPLC walifika saa sita mchana ilhali tukio lenyewe lilifanyika saa tatu asubuhi.

Dogo huyo kisha alikimbizwa hadi Hospitali ya Chemolingot kwa huduma za kwanza kabla ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Nakuru kwa matibabu zaidi.

Mamake Irene Anamale alikuja kusimuliwa matukio haya yote baada ya kuanza kumsaka mwanawe ambaye alikosa kuja nyumbani jioni. Alipashwa habari kuhusu kilichojiri wakati Kalalwa tayari alikuwa hospitalini Nakuru akiwa amelazwa.

Siku iliyofuata aliandamana na shangaziye Kalalwa na jirani na walipofika hospitalini alichokiona kilimshtua. Mwanawe alikuwa katika hali mbaya wala hakuweza kumtambua.

“Alikuwa kitandani akiguguna kwa maumivu na uso wake ulikuwa umevimba wala hangeweza kuona vyema. Ilichukua siku tatu ndipo anitambue wala hata hangeweza kutembea kuenda kujisaidia,” akasema Bi Anamile, mchuuzi wa vyakula.

Kinachosikitisha ni kuwa kwa muda wa miezi mitano iliyopita, Kalalwa amekuwa hospitalini akiangaliwa na kutunzwa na mamake ila usimamizi wa KPLC haujawatembelea au kufanya lolote.

“Sikufikiria mwanangu angeimarika kwa sababu miezi kadhaa imepita imekuwa kipindi kigumu zaidi kwake. Amekuwa akihisi maumivu sana,” akaongeza, mama huyo wa watoto wanne na mlezi wao wa pekee.

Alishangaa kwa nini usimamizi wa KPLC haujamtembelea mwanawe ilhali ni utepetevu wao ndio umechangia masaibu yake.

“Kila mara nikipiga simu kuomba msaada, wananikosea heshima. Wametelekeza mwanangu wala hawajafanya lolote kumsaidia. Nasaka haki kwa mwanangu kwa sababu amekosa shule kwa miezi kadhaa na hata sijui ataanzia wapi baada ya kupona,” akasema.

Alisema kuwa mzigo wa kumtunza na kumwangalia mwanawe umekuwa mkubwa sana kwake huku pia akiwalea watoto wengine watatu.

Hospitalini, Tabitha Akuka, naibu msimamizi wa kitengo kinachowauguza waliochomeka alisema Kalalwa atahitajika kufanyiwa upasuaji mwingine japo kwa sasa wamejaribu sana kumwokoa kutoka hatarini.

“Amepitia upasuaji mara mbili na bado imebakia moja ambao atafanyikwa Jumatatu ijayo au Jumapili. Tutahakikisha kuwa miguu yake inapona vizuri wala hataondoka hospitalini kama hajapona kabisa,” akasema Bi Akuka.

Meneja wa KPLC tawi la Baringo Samuel Boigor alithibitisha kuwa wanafahamu kisa hicho, wamefanya uchunguzi na ripoti imewasilishwa kwa vitengo vya usalama na bima.

Alikiri kuwa walichelewa kufika eneo la tukio kwa sababu walipata habari kuhusu yaliyotokea kwa kuchelewa.

“Akiondoka hospitalini, familia yake itashauriana na idara yetu ya bima kuhusu gharama ya matibabu. Huwa tunashauri familia zisifuatilie gharama hiyo mara moja kwa sababu kuna visa ambavyo huishia mauti,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.