Mahubiri: Usizoee kutazama nyuma kwa masikitiko, kuna nuru mbele
GIZA lililoko nyuma, usilitazame mbele ni kweupe. Kutazama nyuma kwa masikitiko, hakulipi. Kutazama nyuma kwa tamaa, hakulipi. Yaliyopita si ndwele, ganga yajayo. Kama nyuma panatokota mabaya, usitazame nyuma.
Kubainisha hatari ya kutazama nyuma, tunakumbushwa kumtazama mke wa Lutu.
“Mkumbukeni mkewe Lutu” (Luka 17:32). Jina lake halitajwi katika Biblia. Ila mume wake Lutu alikuwa mwadilifu na mcha-Mungu.Miji ya Sodoma na Gomora ilipindukia katika maisha ya raha. Ilipitiliza bila kufanya toba.
Mungu aliadhibu miji ya Sodoma na Gomora. Familia ya Lutu iliokolewa katika hasira takatifu ya Mungu. Waliambiwa wasitazame nyuma. Mke wa Lutu alipotazama nyuma, aligeuka nguzo ya chumvi.
Kutazama nyuma huku kuna hatari zifuatazo:Kwanza, kutohamishika. Mtu hayuko tayari kuhama kutoka mazingira hatarishi na mabaya.Pili, kupoteza uhai wa kiroho. Palipo na dhambi ya mauti kuna kupoteza uhai wa kiroho.
Mke wa Lutu alikufa “amesimama kama gari.”Tatu, ni kutosonga mbele. Husongi mbele kwa kusitasita.
Ukitazama nyuma unakwamisha safari ya wokovu.Mke wa Lutu alizongwa na mambo matano: kutotii, uzembe, masikitiko, tamaa, na kutoachia. Kuna mtu mmoja aliyezongwa na ulevi si “kunywa divai kidogo” ya Mtume Paulo kwa Timotheo.
Yeye aliamua kuvunja chupa tupu za kileo kikali. Alivunja chupa ya kwanza na kusema: “wewe unanifanya nikose karo ya watoto.” Alivunja chupa ya pili na kusema:
‘Wewe unanifanya niuze simu zangu.” Alipofikia ya tatu na kuona bado ina kileo kikali, aliambia chupa: ‘Wewe kaa pembeni, sina ugomvi na wewe.’ Utamaliza kiu yangu baada ya zoezi hili.” Huyu alitazama nyuma.