Makala

Maina Njenga aahidi kupanga mkutano mwingine ‘akisaidiana na Uhuru’

January 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Bw Maina Njenga, amesisitiza kwamba harakati za kuandaa mkutano mkubwa wa viongozi wa Mlima Kenya wakiongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta bado zingalipo.

Hii ni licha ya mkutano aliokuwa amepanga mnamo Desemba 31, 2023 katika uwanja wa Kabiru-ini ndani ya Kaunti ya Nyeri kutibuliwa na serikali na washirika wa Bw Kenyatta kumtaka akome kutumia jina la rais huyo mtaafu.

“Uhuru atahudhuria kama kiongozi wa Mlima Kenya na atakuja kutupa mawaidha na maono ya kuelekea mbele katika mustakabali wa kijamii na kisiasa,” akasema Jumatatu alipotoa taarifa kuhusu sokomoko la Kabiru-ini.

Bw Njenga alikuwa ameupigia debe mkutano huo kama uliokuwa wake wa kukabidhiwa majukumu ya kuwa msemaji wa jamii za Mlima Kenya na Bw Kenyatta na hatimaye atoe hotuba yake ya kukubali na pia viongozi wengine wahutubu.

Serikali kupitia kamishna wa Kaunti ya Nyeri Bw Peter Murugu alisema kwamba mkutano huo ulikuwa wa kufufua kundi haramu la Mungiki na ndipo serikali ikaupiga marufuku.

Aidha, Bw Njenga amemtahadharisha Naibu wa Rais Rigathi Gachagua dhidi ya mtindo wa vitengo vya kiusalama kukandamiza vijana wa Mlima Kenya kwa kuwahusisha na kundi haramu la Mungiki.

Bw Njenga alisisitiza kwamba hajaenda mafichoni kama ilivyokuwa ikienezwa kutokana na mkutano huo wake kuishia kuwa misako mikali katika Kaunti ya Nyeri, Murang’a, Nyandarua, Laikipia, Kirinyaga, Nairobi, Nakuru, Machakos na Kajiado.

Ripoti ya polisi kuhusu misako hiyo ya Januari 1, 2024 ilionyesha kwamba jumla ya vijana 704 walinaswa, 250 wakiwa wa Nyeri.

Bw Njenga hakuonekana katika eneo la Nyeri licha ya msako mkali kuandaliwa katika barabara zote za kuingia Kaunti hiyo, sasa akisema kwamba “hata hakukuwa na mkutano kwa kuwa ulikuwa umeahirishwa”.

“Nilipata kumtafuta Bw Kenyatta na viongozi wengine wa nchi na tukakubaliana kwamba mkutano huo wa Nyeri kwanza tuachane nao. Lakini kwa kuwa hatukuwa na nia ya kuwaacha wafuasi wetu kwa mataa ikizingatiwa tulikuwa tumeandaa mkutano huo kwa muda, tukaamua tujipange tena polepole,” akasema.

Tayari, wandani wa Uhuru wakiwemo aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Bw Jeremiah Kioni na mwanablogu Pauline Njoroge wamemuonya Njenga dhidi ya kutumia jina la rais huyo mstaafu katika hotuba na mikutano yake wakisema kwamba “anajua kujieleza kila wakati akiwa na suala la kuwaambia Wakenya.

Alisema hakuwa amechapisha tangazo rasmi la kuwaita vijana wajitokeze Kabiru-ini wala kutuma ilani kwa maafisa wa polisi kama ilivyo sheria “kwa hivyo wale waliokamatwa walikuwa katika harakati zao za kibinafsi”.

Hii ni licha ya vijana walioponyoka kunaswa kukiri kwa vyombo vya habari kwamba walikuwa wakitii “mwaliko wa Bw Njenga wa kuandaa maombi na mkutano wa kisiasa”.

Bw Njenga aliongeza kwamba hangejitokeza katika Kaunti ya Nyeri au kwingineko kuwasaidia wafuasi wake waliokuwa wakikamatwa na maafisa wa polisi akiongeza kuwa kwa sasa anaomboleza kifo cha mjomba wake.

“Tunapanga mazishi na hata tulimpeleka Mochari siku hiyo ya mkutano wa Kabiru-ini,” akasema.

Aliitaka serikali ielewe kwamba “kwa sasa hakuna kundi linaloitwa Mungiki na hao vijana sasa ni wale baada ya kutumiwa na viongozi wa Mlima Kenya kuingiza utawala wa William Ruto mamlakani wamegeukwa na kubandikwa kuwa wanachama wa kundi haramu”.