• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Maina Njenga: Gachagua ajue mimi ndiye kusema Mlima Kenya

Maina Njenga: Gachagua ajue mimi ndiye kusema Mlima Kenya

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA kinara wa kundi haramu la Mungiki Bw Maina Njenga ameshikilia kwamba yeye ndiye kinara wa siasa za Mlima Kenya, akimuonya Naibu wa Rais Rigathi Gachagua akome kumharibia jina.

Bw Njenga anadunisha vita vya kiubabe ambavyo vimechipuka kati ya Gachagua na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, akisema “mimi ndio kusema”.

Aidha, Njenga alifichua kwamba wakati shamba la rais mstaafu lililoko Mjini Ruiru lilivamiwa Machi 27, 2023 na genge lililosemwa kusajiliwa na serikali na likaiba mbuzi na kukata miti, “mimi nilitoa vijana wa kuweka usalama eneo hilo na pia nikatoa miti 2, 000 na tukaipanda katika shamba hilo kama fidia ya iliyokatwa”.

Alikana madai kwamba anarejesha tena kundi haramu la Mungiki.

“Unawasikia wakisema kwamba eti sisi tumerejea ili tuanze harakati za kutahirisha wanawake. Hebu wakuje watuonyeshe mmoja tu ambaye tumetahirisha,” akaambia Taifa Leo Dijitali.

Bw Njenga alikuwa akimjibu Bw Gachagua ambaye mnamo Januari 2, 2024 akiwa katika Kaunti ya Nyandarua aliteta kwamba “kuna vijana ambao wanakusanywa upya ili warejeshe matukio ya kukeketa wanawake wetu na pia kututoza ushuru katika biashara zetu”.

Bw Gachagua alikuwa akirejelea hatua ya serikali ya kuharamisha mkutano wa kisiasa wa Bw Njenga aliokuwa ameitana uwanjani Kabiru-ini Kaunti ya Nyeri.

“Hilo halitafanyika na ikiwa ndio mwisho wa umaarufu wangu wa kisiasa, na uwe. Niko tayari kupoteza kura nikilinda kina mama wetu dhidi ya genge hilo na uhasi walo,” akasema Bw Gachagua.

Kwa upande wake, Bw Njenga amesema kwamba “mimi ndiye nilikuwa mwanzilishi wa kundi la Mungiki lakini pia nilitangaza hadharani na waziwazi hatua ya kulizima… kwa hivyo tuache kukumbushwa mambo yetu ya kale ambayo tuliyakoma”.

Alihoji itakuwaje “mimi ambaye ndiye nilikuwa mkubwa wa kundi hilo na nimesema nililimaliza kuwe na mwingine ambaye bado anashikilia kwamba liko”.

Alifananisha harakati za ukandamizaji anaotwikwa Mlima Kenya pamoja na wafuasi wake na kisa cha mfalme fulani ambaye kila mara akiugua alikuwa akidai lishe ya nyama ya nyani.

“Ulifika wakati ambapo hakukuwa na nyani mchanga wa kuchinjwa na ndipo mfalme huyo alitangaza kuwa hata wale nyani wakubwa na wakongwe waliokuwa wakitumwa kuchinja wale wadogo bado walikuwa ni nyani tu waliokuwa na nyama,” akasema.

Alisema kwamba hiyo ndiyo mbinu ambayo imekuwa ikitumika Mlima Kenya “ya kuchinja vijana na baada ya wao kuisha, wameelekeza ulafi wao kwa wale nyani wakubwa na wakongwe”.

Aliwataka wenyeji Mlima Kenya wakae kwa umoja, upendo na amani “ili kujipa afueni za kimaisha katika hali zetu zote”.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wamalwa: Ruto alikerwa nilipopeleka Wetangula, Musalia kwa...

Jinsi Tanzania imejipanga AFCON mara hii kuepuka fedheha ya...

T L