• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Maiti za Shakahola: Mung’aro amtuma Jumwa kwa Kindiki

Maiti za Shakahola: Mung’aro amtuma Jumwa kwa Kindiki

NA ALEX KALAMA

GAVANA wa Kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro amemsihi Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa kuzungumza na mwenzake wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ili kuhakikisha kwamba miili iliyotambuliwa inaondolewa katika mochari ya Hospitali Kuu ya Malindi kuenda kuzikwa.

Akizungumza Jumamosi katika kijiji cha Muyeye, eneobunge la Malindi, gavana Mung’aro alisema kuna haja ya miili ambayo tayari chembechembe za DNA zimelinganishwa na kufafana, kukabidhiwa kwa wanafamilia wakazike ili kupunguza msongamano.

Kiongozi huyo wa kaunti alikuwa amehudhuria hafla ya mazishi ya aliyekuwa gwiji wa nyimbo za Kimijikenda Mzee Masha wa Iha.

“Nataka nikwambie Waziri wa Jinsia kwamba imekuwa vizuri siku ya leo uko hapa. Nakutuma ufikishe salamu kwa waziri mwenzako wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ya kwamba afanye mpango ile miili ambayo ilifukuliwa kule msituni Shakahola na ambayo ilitambuliwa, ikabidhiwe wenyewe wakaizike.

Alisema maiti za wahanga wa Shakahola walioangamia katika kinachodaiwa ni kupotoshwa na mahubiri ya Paul Mackenzie wa Good News International, zimekwamisha mambo mengi sana kufanyika.

“Tunataka kurekebisha ile mochari lakini kwa kuwa ile miili haijaondolewa pale, imekuwa vigumu kufanya kazi hiyo,” akasema Bw Mung’aro.

Alisema haoni haja ya miili iliyokwisha kufanyiwa mlinganisho wa DNA kuendelea kuhifadhiwa mochari.

“Kwa nini zile familia ambazo zilipewa majibu ya mlinganisho wa DNA zisipewe miili kuenda kuizika?” akauliza.

Gavana huyo alisema kuwa serikali yake iko na mipango ya kuboresha Hospitali Kuu ya Malindi ili kuhakikisha huduma zote za matibabu zinazohitajika zinapatikana pale kama zile zinazopatikana katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) jijini Nairobi.

Alisema hospitali hiyo ya Malindi inafaa kuwa na hudumu kwa wagonjwa mahututi.

“Hivi karibuni tutajenga wodi mbili mpya za kisasa katika Hospitali Kuu ya Malindi. Pia tutajenga chumba kingine kipya cha kina mama wajawazito kujifungulia na kufikia mwisho wa mwaka huu 2024 tutakuwa tuko na chumba cha kuhudumia wagonjwa mahututi ambacho kitakuwa na vitanda 10,” akaahidi.

Aidha gavana huyo alidokeza kuwa serikali yake imetenga jumla ya Sh250 milioni ili kuboresha sekta ya afya katika hospitali hiyo ya Malindi na mipango hiyo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Machi 2024.

Mbali na hayo, gavana Mung’aro aliahidi kujenga barabara moja mjini Malindi ambayo itaitwa jina la Masha wa Iha kama njia mojawapo ya kumuenzi na kumukumbuka gwiji huyo wa muziki wa kitamaduni aliyetangulia mbele ya haki. Barabara yenyewe itakuwa ya kutoka Kasufini kuelekea Thalatha Meli.

Katika hafla hiyo ya mazishi Bw Mung’aro alikuwa ameandamana na mbunge wa Malindi Amina Mnyazi pamoja na waziri Jumwa.

Jumla ya miili 429 ya waliokuwa waumini katika kanisa tata la Good News International imekuwa ikilala katika mochari.

Soma Pia: Jinsi mauaji chakani Shakahola yalivyoshtua ulimwengu

Wengi wao walifariki wakifunga msituni Shakahola ili wakakutane na Yesu jinsi walivyoelezwa na viongozi wao wa kidini.

Sakata hiyo ilipofichuka, serikali kwa ushirikiano na wadau wengine ilianzisha msako mkali msituni na ufukuaji wa makaburi ya halaiki kuondoa maiti ambazo ziliishia mochari ya Hospitali Kuu ya Malindi.

Hadi sasa bado haijazikwa na ingali imehifadhiwa kwenye makontena mawili katika mandhari ya mochari hiyo ya Malindi.

Soma Pia: Kontena kutumika kuhifadhi miili baada ya mochari kujaa

  • Tags

You can share this post!

Shule yatoa hamasisho kuepusha watoto kuuawa mtaani

Migogoro ya ardhi yapungua tangu kitabu kuanika makateli

T L