• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Majangili Pokot Magharibi sasa wateka nyara watoto

Majangili Pokot Magharibi sasa wateka nyara watoto

NA OSCAR KAKAI

MAJANGILI wanaendelea kutesa vijiji vilivyoko kaunti za Pokot Magharibi na Turkana, mara hii wakiwateka nyara watoto.

Ukatili wa watekaji nyara umewatia hofu wazazi wanaojituma kila siku kuwapeleka wana wao shuleni.

Hii imekuwa tishio kwa amani na kuathiri maisha, maendeleo na uchumi wa maeneo husika.

Wiki jana, msichana wa umri wa miaka 12 alitekwa nyara katika kijiji cha Akulo kilichoko wadi ya Masol, Kaunti ya Pokot Magharibi kisha akapatikana hai katika Kaunti ndogo ya Turkana Mashariki, kaunti jirani ya Turkana.

Mwishoni mwa mwaka 2023, mvulana mdogo wa umri wa miaka 10, John Nangat Lobore, alitekwa nyara na majangili katika kijiji cha Kostei eneo la Turkwel.

Hilo lilitokea baada ya watoto wawili na wanaume wawili kutegwa nyara na kujeruhiwa vibaya. Waathiriwa walikuwa wa kutoka vijiji vya Kamurio na Sarmach mtawalia.

Kwenye kisa kingine, kijana Lonyakomol Lokuri akiwa na wenzake wawili, aliuawa huku wenzake hao wakifanikiwa kutoroka lakini wakiwa na majeraha.

Awali, mvulana mdogo Eliya Lwalenyang alitekwa nyara katika kijiji cha Songok na kupelekwa mbali kwa mwendo wa saa sita kisha akarejeshwa usiku baada ya askari wa akiba na maafisa wa usalama kuwasaka majangili hao.

Kulingana na wakazi, visa hivi vimekuwa vikichochea uhasama zaidi na hatua za ulipizaji kisasi.

Inadaiwa kuwa majangili huwaumiza mateka na hata kuwatoa kama sadaka kwa miungu.

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya usalama wamesema kuwepo kwa makundi kinzani ya ujangili kunasababisha ongezeko la utekaji nyara watoto “ndiposa wale ambao wameiba mifugo yao (ya watekaji nyara) wasikie uchungu na kuirejesha (mifugo)”.

Chifu wa Ombolion Joseph Korkimul anasema kuwa lengo la mashambulio mapya halijabainika sababu majangili wengi huwa hawaibi mifugo bali wanateka nyara watoto peke yao.

“Majangili wameamua kutumia mbinu chafu sababu wanaamini kuwa kuwateka nyara watoto kutakomesha kabisa wale ambao hulipiza kisasi baadaye. Hakuna mzazi anataka kuona mwanawe akiwa mikononi wa majangili. Upendo wa watoto kutoka kwa wazazi ndio majangili hutaka kuondoa,” alisema Bw Korkimul.

Mzazi Linah Kales kutoka kijiji cha Kases anasema kuwa wanawake na watoto wanafaa kuwekwa kando kwenye suala la ujangili.

 “Ni suala la kuvunja moyo kuona maafisa wa usalama wakiwa karibu na shule lakini hawalindi watoto. Kwa sasa tunategemea Mungu tu. Sisi ni kama tumesahaulika kuhusu maisha ya watoto wetu,” alisema Bw Kales.

Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing anasema kuwa majangili wamebadili mbinu na wanafanya mashambulio majira ya mchana.

“Wanalenga watoto na akina mama ambao hawana hatia. Watoto ni watu ambao hawana uwezo wa kujikinga. Hawana nguvu wakati wanavamiwa,” alisema Pkosing.

Bw Pkosing ambaye ameghabishwa na kiwango cha juu cha utekaji nyara, alisema kuwa hali hiyo huenda ikawa mbaya zaidi ikiwa serikali haitachukua hatia.

“Kukiwa na matukio kama haya, tunaharibu matunda ambayo tumepata kuhusu kuwarai wakazi kupeleka watoto shuleni. Sababu kutokana na hali hii ya utekaji nyara, wazazi hawataruhusu wana wao kuenda shule,” alisema.

Alisema kuwa utekaji nyara bado unaendelea licha ya fedha kuwekwa kwenye bajeti ya usalama ambayo inafaa kuwa na upepelezi wa hali juu na kuzuia uhalifu wa aina hiyo.

“Kuna haja ya maafisa wa usalama kuhakikisha kuwa wanabuni mbinu za kuweka usalama shuleni,” alisema Bw Pkosing.

Seneta wa kaunti ya Pokot Magharibi Julius Murgor anashangazwa na kinachofanyika katika jamii.

Kulingana na Bw Murgor, majangili wanaisababishia jamii kilio kikubwa.

“Majangili hao hulenga wasiojiweza. Wao hulenga mtu, eneo ama umma ambao haujalindwa,” alisema Bw Murgor.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Pokot Magharibi Peter Kattam, anasema kuwa maafisa wa usalama wanalenga kuharibu maficho ya majangili ambayo hutumika na wakora kupanga mashambulio katika eneo la Bonde la Kerio.

“Tunalenga vigogo wao na tunapanga kuwakamata. Wanajihusisha kwa kuwapa mafunzo watu wawe majangili, wezi wa mifugo na wauaji,” alisema Bw Kattam.

Kamishina wa kaunti hiyo Khalif Abdulahi anasema anawajibikia kazi yake, lengo likiwa ni kunyamazisha milio ya risasi katika eneo hilo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Tanzania yapata treni za umeme, Kenya ikisukuma maisha na...

Wakeketaji waficha uovu wao kwa muziki wa juu

T L