Makala

Majembeni: Mji wa wapenda kilimo usiopenda wazembe

May 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

“DEREVA tafadhali simamisha gari nishukie hapo kwenye Majembe…”

Hiyo mara nyingi ndio iliyokuwa kauli miongoni mwa abiria waliokuwa wakiabiri matatu au mabasi, iwe ni kutoka Lamu, Mokowe, Hindi na Mpeketoni kuelekea Witu, Malindi na Mombasa au kurudi.

Ni kauli ambayo mwishowe ilizaa mji na eneo nzima liitwalo Majembeni katika Kaunti ya Lamu.

Kulingana na Chifu Mkuu Mstaafu wa eneo la Hongwe ambalo pia linajumuisha Majembeni, Bw Isaac Mkalimani, kulikuweko na majembe yapatayo manne yaliyoachwa na mzungu mmoja baada ya katapila au trekta kubwa zilizokuwa zikitekeleza ujenzi wa barabara kuharibikia eneo hilo miaka ya sabini (1970s).

Ni kutokana na kuwepo kwa majembe hayo ya katapila ambapo wasafiri waliweza kulitambua eneo au stendi hiyo kiurahisi, hivyo kuwaelekeza madereva na makondakta kuwashukishia pahali hapo.

Miaka 50 baadaye, Majembeni imenawiri hadi kuwa mji na kupewa hadhi ya kuwa lokesheni, ikiwa na idadi ya watu wapatao 7,000.

Mji wa Majembeni uko katikati ya barabara ya Lamu-Garsen, ambapo barabara hiyo huugawanya mji huo pande mbili.

Lokesheni ya Majembeni inapatikana kwenye wadi mbili za Lamu ambazo ni Mkunumbi na Hongwe.

Unaposafiri kwenye barabara kuu ya Lamu-Garsen utaupata mji wa Majembeni ukiwa kati ya Kibaoni na Witu.

“Majembeni ni mji ulioanza kama steji ya mabasi na matatu. Ni mahali ambapo magari ya usafiri wa umma yaliteremsha au kupakia abiria na mizigo pale. Kulikuwepo na Majembe makubwa ya katapila iliyoharibika pale wakati ikitekeleza ujenzi wa barabara yetu. Yalikuwa ni ya mzungu. Tulianza kuyaona majembe hayo mwaka 1974,” akasema Bw Mkalimani.

Aliongeza, “Abiria walikuwa wakiwafahamisha madereva na makondakta kwamba washukishiwe kwenye majembe hayo. Hivyo ndivyo jina Majembeni lilichipuka na kunawiri hadi leo ila majembe yenyewe yaliachwa kuoza na kuozeana pale. Pia wananchi walipoanza kubuni makazi pale walikata majembe hayo na kuyauza kipandekipande kama vyuma vikuukuu. Majembe hayapo tena.”

Wazembe hawana nafasi

Ni mji unaotambulika sana kwa kuwa na watu wenye bidii za mchwa na wapenda kilimo.

Hapa, wazembe kamwe hawana nafasi.

Ni kutokana na hilo ambapo mji wa Majembeni unaendelea kuvuma kote Lamu kwa kilimo cha kujikimu majumbani na pia kilimo-biashara.

Ni Majembeni ambapo utapata wakulima wengi kutoka kila upande wa Lamu, iwe ni kisiwani Lamu, Mokowe, Hindi, Witu, Mkunumbi, Mpeketoni, Hongwe, Baharini na viunga vyake, ambao walianzisha makazi Majembeni.

Majembeni sasa imekuwa miongoni mwa miji michache ya Lamu inayotambulika kama jungu kuu la kilimo na kuzalisha mazao yanayotegemewa kote Lamu.

Kwa mujibu wa Naibu wa Chifu wa Majembeni, Bi Eunice Njoroge, mazao mengi, yakiwemo mahindi yanayotumika kwenye miji ya kaunti ya Lamu huzalishwa kutoka Majembeni.

“Lokesheni yetu ya Majembeni iko na vitongoji kama vile Mavuno na Poromoko ambavyo ndivyo kusema kwa masuala ya kilimo na uzalishaji wa chakula kitumiwacho kote Lamu. Hapa utapata mahindi, maharagwe, pojo na hata matunda yakizalishwa kwa wingi na kusambazwa kwenye masoko na maduka ya Mpeketoni, Witu, Lamu mjini na kwingineko. Twajivunia kuwa wanaMajembeni,” akasema Bi Njoroge.

Mwanahistoria, diwani wa zamani na mkongwe zaidi eneo hilo, Bw Francis Chege, anakiri kuwa majembe yaliyoachwa na wazungu zamani ndio yaliyochangia eneo la Majembeni kubandikwa jina hilo hadi leo.

Shamba mojawapo Majembeni. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Chege alipongeza juhudi za serikali kuimarisha miundomisngi, hasa barabara kwenye eneo hilo la Majembeni na viunga vyake, hali ambayo imechangia mji huo kukua kwa kasi.

Anafafanua kuwa anayefika Majembeni kwa sasa atapata ni eneo lililokua kimaendeleo kwani utapata kuna kambi za kivyake za polisi wa kitengo cha kukabiliana na ghasia za dharura (RDU) wakijumuika au kushirikiana na Majeshi ya Ulinzi Kenya (KDF).

Pia utapata zahanati na shule kadhaa za msingi miongoni mwa masuala mengine ya kimsingi eneo hilo.

Bw Chege alishukuru kwamba Majembeni iliyoanza kama eneo dogo la majembe makuukuu yaliyoachwa tu kuharibika pale sasa imeendelea vilivyo.

“Biashara na kilimo vimenoga. Kuna maduka makubwa na vioski vingi. Tuko na usalama wa kutosha kwani polisi na KDF wamebuniwa kambi zao pale. Zahanati na shule ziko. Kujengwa kwa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen pia kumeletea mji wetu faida tele. Mji unazidi kupanuka kila kuchao,” akasema Bw Chege.