• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Majonzi mwanafunzi akizama majini akijipiga selfie

Majonzi mwanafunzi akizama majini akijipiga selfie

NA MWANGI MUIRURIĀ 

FAMILIA ya mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyezama Mto Chania akijipiga selfie Januari 10, 2023 imeitaka serikali kutoa wapiga mbizi kusaidia katika harakati za kumsaka.

Rose Njeri kutoka Kijiji cha Gwa Kumunyu-Gakui, eneobunge la Gatundu Kusini anasemwa kwamba aliandamana na marafiki wawili kujipiga selfie kabla ya kurejea shuleni katika Kaunti ya Machakos.

Kamanda wa polisi Gatundu Kusini Bi Wanjiku Gakurui alisema juhudi za kusaka mwili wa mwaathiriwa zimezinduliwa.

Alisema kwamba eneo alipozama ni hatari na ambapo maji hupita chini ya mawe makubwa ambapo huenda ndipo mwaathiriwa alikwama.

“Tunaomba subira huku tukifanya bidii kusaka msichana huyo ndani ya mto huo hatari na ambao unazidi kuwa na mafuriko kutokana na mvua inayozidi kunyesha. Hatuwezi kwa sasa kuongea kuhusu hali yake kwa kuwa ya Mungu ni mengi. Tunaamini kuwa bado kuna matumaini ya kupatikana akiwa hai,” akasema.

Hata hivyo, Bi Gakurui alionya wenyeji dhidi ya mzaha wao katika kingo za mito, madimbwi na pia matimbo.

Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bw Elijah Kururia alisema “tunaungana na familia ya mwaathiriwa kumtumainia Mungu katika shughuli ya kumsaka ndani ya maji”.

Alisema atatembelea familia hiyo na pia kushiriki kikamilifu katika harakati za sasa za dharura za kumtafuta msichana huyo.

Bi Gakurui alisema uchunguzi pia umezinduliwa kuhusu mazingara halisi ya msichana huyo kuishia ndani ya mto huo.

“Tunataka kubaini kwa uhakika kiini cha msichana huyo kuwa katika kingo hizo, alikuwa akipiga selfie akitumia simu ya nani kwa kuwa kwa kawaida wanafunzi huwa hawana simu na pia waliokuwa naye katika muda wa mkasa huo,” akasema.

Afisa huyo alisema kwamba ripoti za kuanguka kwake zilitolewa na marafiki wake wawili “lakini tutarekodi taarifa rasmi baada ya kuwahoji kwa kina”.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Jinsi Tanzania imejipanga AFCON mara hii kuepuka fedheha ya...

Eugene Wamalwa: Nitakuwa debeni 2027 kuwania urais

T L