MAKALA MAALUM: Afueni kwa wazalishaji mahindi huku bei ya mbolea ikishushwa
BARNABAS BII na ONYANGO K’ONYANGO
WAZALISHAJI mahindi katika eneo la North Rift wana kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali kutangaza mpango mahsusi wa kutoa mbolea ya bei nafuu wakati huu wanapojiandaa kwa msimu wa upanzi.
Chini ya mpango huo, serikali itanunua mbolea moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji. Kisha mbolea hiyo aina ya DAP itauziwa wakulima kupitia maghala ya Halmashauri ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) na yake ya Shirika la Kitaifa la Wafanyabiashara (KNTC) kwa bei ya Sh2,300 kwa gunia moja la kilo 50.
Wafanyabiashara wa reja reja wamekuwa wakiwauzia wakulima mbolea hii ya kupanda kwa Sh3,200, bei ambayo wakulima wamelalaka wakisema ni ya juu mno.
“Kuanzia msimu ujao, wakulima watanunua mbolea kutoka kwa maghala ya NCPB na KNTC kwa kutumia mfumo wa “E-Vouchers” ili kuwakinga dhidi ya wafanyabiashara wanaowapunja,” Waziri wa Kilimo Peter Munya akasema.
Alisema vocha hizo zitatolewa kupitia vyama vya ushirika vilivyosajiliwa ili kuwawezesha wakulima wadogo kunufaika kutokana na mpango huu.
“Mfumo huu umeanza kufanyiwa majaribio katika baadhi ya kaunti na lengo letu ni kuwafikia wakulima wenye mahitaji zaidi kupitia vyama vya ushirika vilivyosajiliwa,” Bw Munya alisema wiki jana alipokutana na wakulima kutoka eneo la North Rift mjini Eldoret.
Lakini wakulima waliiomba Serikali kutekeleza Muafaka wa Maputo wa 2003, ambao Kenya ilitia sahihi, na na kutenga angalau asilimia 10 ya bajeti ya kitaifa kwa sekta ya kilimo.
“Muafaka wa Maputo uliungwa mkono na Mkataba wa Malabo wa 2014 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu na hivyo serikali inapasa kuutekeleza ili kupiga jeki sekta ya kilimo,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Wakulima Nchini (KFA) Kipkorir Arap Menjo.
Wakulima wa mahindi kutoka eneo, hilo hata hivyo, wamepata pigo kufuatia uvumazi wa nzige ambao huenda wakaathiri msimu huu wa upinzani.
Makundi kadha ya nzige yamevamia sehemu nyingi za kaunti za Trans Nzoia, Bungoma, Elgeyo Marakwet, Baringo, Pokot Magharibi na Turkana na kuharibu ekari kadhaa za mashamba ya mimea ya chakula na nyasi. Uvamizi huu ni tishio kuu kwa uzalishaji wa chakula na mali nyingine katika sehemu hizo.
Wakulima waliohojiwa walielezea hofu kwa nzige hao watakula mimea ya mahindi, wimbi, mtama na maharagwe wakati huu ambapo mvua imeanza kunyesha katika maeno hayo.
“Nzige hao wamezaa mayai ambayo huenda yakaanguliwa katika muda wa majuma machache yajayo na huenda wakala mimea yetu na kutusababishia hasara kubwa kwa kuwa tutalazimika kupanda tena,” akasema Bw Mathew Kosgei, mkulima kutoka eneo bunge la Moiben, kaunti ya Uasin Gishu ambako wadudu hao walitua juzi.
“Nzige hao watarudisha nyuma mafanikio ambayo yalipatikana katika sekta ya kilimo kupitia upanzi kwa wakati ambapo wakulima walitarajia kupata mavuno mazuri mwaka huu,” akaongeza Bw Kosgei.
Katika kaunti ya Trans Nzoia, wakulima wa mahindi wanapanga kuchelewa kupanda baada ya makundi ya nzige kuonekana katika maeneo ya Matumbei, Kapretwa na Mankhele.
“Nzige walionekana katika kaunti hii na inashukiwa huenda wametoka Uganda kupitia shamba la Shirika la Ustawishaji Kilimo (ADC) la Suam,” akasema Waziri wa Kilimo katika kaunti ya Trans Nzoia, Mary Nzoma.
Alisema wamewashauri wananchi kuwa waangalifu na wapige ripoti endapo watawaona wadudu hao popote. “Wao hula nyasi lakini huenda wakala mimea endapo hatua hazitachukuliwa haraka kuwaangamiza. Tumeanza mikakati ya kuwanyunyizia dawa,” akasema Bi Nzomo.
Katika kaunti za Uasin Gishu na Nandi, maafisa wa idara za Kilimo walisema wameweka mikakati ya kukabiliana na wadudu hao waharibifu walioonekana katika kaunti jirani.
Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Nandi, Dkt Kiplimo Lagat alisema, wamewaita maafisa wao walioenda likizoni ili wapige jeki juhudi za kupambana na nzige hao kote katika kaunti hiyo.
“Tumewaamuru maafisa wa kilimo wawe chonjo na wawasaidie wakulima katika maeneo yote ya kaunti hii endapo nzige watavamia,” akasema.
Katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, nzige wamevamia maeneo ya Soi Kusini, Tambach na Emsoo katika eneo bunge la Keiyo Kaskazini na kuibua hofu miongoni mwa wakulima.
“Nzige walitoka eneo la Chesongon katika kaunti ya Pokot Magharibi na wakatuvamia katika kijiji cha Liter. Walivamia nyanya na maembe kabla ya kuhamia maeneo ya Tiaty. Wakulima wameingiwa na hofu na wanaitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kuangamiza wadudu hao,” akasema Bi Zephaniah Kiptoo, mkazi wa kijiji hicho.
Kulingana na Katibu wa Wizara ya Kilimo Prof Hamadi Boga, serikali hutumia Sh200,000 kwa saa kunyunyizia nzige dawa kwa kutumia ndege.
“Nzige ni hatari kwa usalama wa chakula nchini na maisha ya wakulima kwa kuwa hula tani nyingi za chakula ambacho kingeliwa na familia za eneo husika,” akaeleza Prof Boga.
Wataalamu tuliowahoji walisema, uvamizi wa nzige katika eneo la Kaskazini mwa Kenya unaweza kuchangia kushuka kwa uzalishaji wa mahindi kwa kiwango kikubwa.
“Hali itakuwa mbaya zaidi kwani mwaka jana kiwango cha mavuno ya mahindi kilishuka kwa magunia milioni 11, kutoka magunia milioni 44 mnamo 2018 hadi magunia milioni 33,” akasema Mathew Langat ambaye ni mtaalamu wa kilimo mjini Eldoret.
“Kwa kuwa nzige wamekula mimea mingine eneo hilo majuzi, kuna hofu kwamba, huenda wakavamia mashamba ya mahindi na hivyo kuathiri uzalishaji wa chakula mwaka huu,” akaongeza.