• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
MAKALA MAALUM: Baada ya kutema mihadarati sasa amegeuka baraka kuu kwa watoto

MAKALA MAALUM: Baada ya kutema mihadarati sasa amegeuka baraka kuu kwa watoto

Na PHYLLIS MUSASIA

AKIWA mzaliwa wa Othaya, Kaunti ya Nyeri, Bw Alex Maina alikuwa mwanafunzi mwerevu shuleni ambaye alitazamia kupata alama za juu.

Hata hivyo, hilo halikutimia kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Akiwa na umri wa miaka 16 hivi, wazazi wake tayari walikuwa wameshaona kijana mwenye maadili ambaye angekuwa nguzo ya familia na mfano mwema kwa wadogo wake wanne.

Lakini licha ya kuwa na maono na matarajio makuu, Bw Maina ambaye kwa wakati huo alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Upili ya Chinga mjini Nyeri, hakuepuka ushawishi wa marafiki.

“Wakati mwingi ningewaona wenzangu wakijishughulisha na matumizi ya dawa za kulevya. Kila nilipowaangalia wakifanya mambo yao, wangenishawishi nionje kidogo lakini nilikumbuka sana ushauri wa mama na baba kuhusu nidhamu na maadili katika jamii,” akasema Bw Maina.

Bw Maina alisema kuwa ilifika wakati ambao hakuweza kujizuia licha ya kutaka kuwa tofauti.

“Maisha yaligeuka kabisa pindi tu nilipovuta bangi kwa mara ya kwanza. Nilihisi kana kwamba nilikuwa katika hali tofauti na kila mtu, nilianza kuwaza tofauti nilipojiunga na wenzangu na kuanza kuvuta sigara, kunywa pombe pamoja na kuvuta bangi mara kwa mara,” akasema.

Maina alianza kujitenga na familia yake huku muda mwingi akikaa na marafiki. Hali ilibadilika na kugeuka kuwa mbaya hata zaidi jambo ambalo lilipelekea wazazi wake kugundua mabadiliko kwenye tabia yake.

“Nilijitenga sana na kuhakikisha kuwa sihudhurii maombi ya kila siku ya familia. Sikuogopa kuvuta bangi hata nilipokuwa shuleni jambo ambalo lilitatiza sana masomo yangu na uhusiano wangu na walimu,” akaeleza Maina.

Muda ulipozidi kuyoyoma, Maina alisema hakuweza kukaa zaidi ya saa tatu kabla ya kutumia marijuana, sigara na pombe.

“Uzoefu wa madawa ya kulevya ulinikosesha amani. Sikuweza kutulia zaidi ya masaa matatu kabla ya kuyatumia madawa hayo,” akaeleza.

Wakati wa usiku, Maina alisema alitumia bangi ili ‘kujizawadi’ kwa yale yote aliyopoteza wakati wa mchana. Aliibadili marijuana kuwa rafiki wa pekee na wakaribu.

Mambo yalianza kwenda murama Maina alipokamilisha masomo yake ya kidato cha nne. Marafiki wote walimkimbia na akabaki upweke. Alihama nyumbani kwao na akajipata akitangatanga kwenye mitaa ya jiji ya Nairobi.

Kule, Maina alisema alipata marafiki wa tajiriba yake. ‘Sikumbuki ikiwa kunacho chochote kibaya ambacho sikufanya. Nikiwa Nairobi niliongoza genge zote za kila uovu. Nilihisi kana kwamba maisha yalikuwa mazuri kwa sababu ya marafiki wapya niliokutana nao,” akasema.

Hata hivyo, licha ya mamabo hayo yote baba yake Maina hakuchoka kujaribu kumsaidia Maina arekebike.

Kama vile mzazi yeyote yule angefanya hima kuona kwamba mwanawe aliyepotoka anarejea katika njia bora, babaye Maina alimzungumzia na kisha kumlipia karo katika chuo kimoja cha ufundi.

“Nilishindwa kusawazisha masomo na utumizi wa madawa ya kulevya. Cha kushangaza ni kwamba licha ya baba kulipa hela nyingi shuleni kwa ajili ya kozi yangu, nilisitisha masomo baada ya muda wa miezi miwili tu,” akaeleza Maina.

Kilichomfanya Maina arekebishe tabia ni bidii ambayo wenzake waliosoma naye walionyesha kila walipokutana naye.

“Kila mmoja alionekana mwenye kufaulu sana maishani. Nilijiona kuwa pekee ambaye niliitisha usaidizi wa kifedha na hata chakula cha siku kutoka kwao,” akasema Maina huku akiongeza kuwa binamuye waliokuwa wakisoma pamoja alikuwa yatari keshamaliza masomo yake na kupata kazi nzuri jijini Nairobi.

Mnamo 1999, Maina anasema aliamua kubadilika ka kurudi nyumbani ambapo aliomba kurejesha uhusiano na wazazi wake.

Baadaye mwaka uliofuata, alihama kutoka Nyeri hadi Nakuru ambapo mwanzo mpya wa maisha yake ulionekana.

“Niligundua kuwa upendo na hamu ya kukaa karibu na watoto ilikuwa inajitokeza ndani yangu. Nilianza kuwatembelea watoto katika mitaa ya mabanda na kuwapa soda na tosti ya mikate kila nilipokutana nao,” akasema Maina huku akiongeza kuwa alihisi vyema kila wakati alipowaona watoto hao wakifurahikia chakula hicho.

Kwa ushirikiano na mkewe Patricia, Maina alisema idadi ya watoto waliokuwa tayari ameunda uhusiano wa karibu nao iliongezeka na akawaza kuanzisha makao ya kuwachunga watoto wa mitaa ya mabanda.

Taka na makapi

Ndani ya chumba chake kimoja walipoishi na mkewe, Maina alishiriki chakula japo kidogo pamoja na watoto kutoka mtaa wa mabanda wa Hilton ambako kunayo sehemu kubwa, Gioto ambako hutupwa makapi yote ya mji wa Nakuru.

Mwaka wa 2005 Maina alisema kazi aliyokuwa akifanya ya juakali ilimsaidia kuanzisha shule ndogo ili kuwasaidia watoto hao kwa ajili ya masomo.

“Maina alitufikia sisi kama wazazi wa watoto hawa na kutuomba ikiwa tungemruhusu kuwezesha kupata masomo. Tulikubali kwa sababu hatukuwa na namna pale kijijini,” akasema mmoja wa wazazi, Bi Lorna Ambezi ambaye alifafamua wengi wao hutegemea kazi ya kuokota chupa za plastiki na chuma kutoka kwenye taka ili kupata riziki ya siku.

Kwa makubaliano hayo, Maina hatimaye alitimiza ndoto yake na kuipa shule hiyo jina la ‘The Walk Community Centre’ na kisha kuibadili kuwa ‘The Walk Academy’ wakati wizara ya elimu ilipohitaji kusajiliwa kwa shule hiyo.

Wakati huu, shule hiyo ina zaidi ya watoto 400 ambao wote wanatoka katika mitaa duni ya Nakuru na familia ambazo hazina uwezo wa kifedha.

‘The Walk Academy’ inatoa masomo ya bure, sare, chakula na vitabu kwa watoto wote.

Chini ya usimamizi wa Bw Maina, shule hiyo imeweza kuajiri jumla ya wafanyakazi 15 wakiwemo walimu na wapishi miongoni mwa wafanyikazi wengine.

Kulingana na mtaalamu wa kutoa ushauri kwa masuala ya matumizi ya dawa za kulenya, Dkt Philip Kisia, matumizi hayo yanaweza kudhibitiwa iwapo iliyeathirika atazungumziwa kwa njia maalum na kupata mafunzo kwa muda.

Aidha, Dkt Kisia anasema kuwa inahitaji uvumilivu na mapenzi kutoka kwa familia ya aliyeathirika ili kuhakikisha kuwa mwanao anawezeshwa kurekebika kikamilifu.

Bw Maina kwa sasa amehitimu kama mtaalamu wa kutoa mawaidha kwa wale walioathirika. Ana shahada katika taaluma ya Saikolojia.

“Nimehitimu pia kama mhubiri na nina shahada ya pili katika theolojia na Ukristo,” akasema Bw Maina ambaye anahubiri katika kanisa moja la Deliverance mtaani Kiamunyi, Nakuru

  • Tags

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya mtindo, sajili na...

Gor Mahia yajikwaa Homeboyz, KCB wakiimarika

adminleo