MAKALA MAALUM: Elimu ya ngumbaru yarudisha maelfu katika masomo Nakuru
Na SAMUEL BAYA
WANAFUNZI wenye umri mkubwa wasiopungua 20 hivi walikuwa makini wakimsikiliza mwalimu wao darasani katika chuo cha elimu ya ngumbaru cha Nakuru.
Kituo hicho kiko katikati ya mji wa Nakuru mkabala na afisi za muungano wa wakulima, kwenye barabara kuu ya Nakuru kuelekea Kabarak.
Utulivu wa wanafunzi hawa wazee wakiendelea kutafuta elimu iliyowaponyoka ujanani ni tofauti kabisa na taswira iliyopo nje ya afisi hizo ambayo ni kelele za magari na shughuli tele za boda boda wanoita abiria.
Hata kuingia kwangu katika darasa hilo hakukuwasimamisha katika utulivu wao na walikuwa makini wakihakikisha kwamba hakuna neno hata moja ambalo linawapita masikioni mwao.
Nilivutiwa na umakini wao ila nikataka kufahamu ni mambo gani ambayo yaliwafanya wakakosa elimu hii ujanani.
Watoto sita
Mmoja wa wanafunzi hapa ni Bi Juliana Chepkoech mwenye umri wa miaka 39 na mama wa watoto sita. Ingawa aliingia kuchelewa darasani na kuketi akihema, alikuwa mtu wa kwanza kunijia kwa mahojiano nilipotaka kujua ujio wake hapa.
“Nimechelewa kidogo. Unajua tena kuchanganya masuala ya kinyumbani na masomo kwa mpigo sio kazi rahisi. Hata hivyo ari yangu ya kutafuta elimu niliyoiacha miaka mingi iliyopita ilinichochea nikarudi masomoni,” akasema katika mahojiano na Taifa Leo.
Bi Chepkoech aliambia Taifa Leo kwamba tayari watoto watatu kati ya hao sita wamemaliza masomo ya sekondari huku wanne wakiwa watahiniwa wa KCSE inayokamilika.
“Watoto wangu watatu walimaliza shule za sekondari halafu mimi mwenyewe ninamaliza mwaka ujao. Mara nyengine ninapotoka nyumbani watoto wananibeza kwa uchu wangu wa elimu ila ninafurahi kwa sababu ninataka kusoma na kupata ufahamu zaidi kuhusu maisha,” akasema.
Mama huyo alisema kuwa kurudi kwake shuleni kuliwashtua wengi hasa katika mtaa anaoishi mjini Nakuru ila aliendelea kuchapa masomo bila uoga.
“Niko pazuri katika somo la Kiingereza ila ninapata changamoto katika masomo ya sayansi. Ni magumu kweli kweli lakini nakaza moyo,” akasema katika mahojiano yetu.
Kando yake alikuwa ni Bi Monica Ngemwa mwenye umri wa miaka 32 na mama ya watoto watatu. Yeye alikuwa nje kimasomo kwa miaka saba hadi mapema mwaka huu alipoamua kurudi tena darasani kusoma.
Wakati yeye akitarajia kumaliza masomo yake ya sekondari ndani ya miaka mitatu ijayo, mtoto wake wa kwanza alimaliza mtihani wa KCPE mwaka huu.
“Nilifanya mtihani wangu wa KCPE mwaka wa 2002 lakini nikakosa karo ya kuendelea na masomo. Hata hivyo baada ya kuwa nje kwa miaka 17, mwaka huu niliamua kurudi kusoma kwa sababu hiyo ndiyo ambayo imekuwa ndoto yangu ya miaka mingi.
“Wakati fulani nilijikataa kwa sababu watu waliniona mimi nimesoma lakiniukweli ni kuwa hata kuandika taratibu za mikutano zilikuwa shida tele. Lakini sasa mambo ni tofauti na ninahisi kwamba ninaelekea vyema,” akasema.
Na ili kuhakikisha kwamba anapata elimu na kujisukuma kimaisha, Bi Ngemwa alisema kuwa mumewe amekuwa katika msitari wa mbele kumuunga mkono.
“Mume wangu hata ni yeye ambaye ananilipia karo ya masomo. Ameniamini na anatia moyo pamoja na wanangu,” akasema.
Kwa ajuza Bi Joyce Njoroge wa umri wa miaka 62, hatua ya wanawe na wajukuu zake kuongea Kiingereza mfululizo kila wanapomtembelea kulimfanya arudi masomoni, ikiwa ni miaka 40 baada ya kuwa darasani.
Bi Njorogoe ni miongoni mwa watahiniwa waliofanya mtihani wao wa KCPE 2019. Awali tulipompata akiendelea na masomo alikuwa mwingi wa matumaini ya kufaulu.
Muda wa miaka 40
“Nilikaa nje kwa miaka 40 na kisha baada ya tafakari ya muda mrefu, niliamua kurudi nyumbani kuendelea na masomo. Ninafanya mtihani wa darasa la nane mwaka huu na walimu wametufunza vyema,” akasema.
Aliongeza “Watoto wangu watatu na wajukuu ni wasomi. Sasa kila mara wanaponitembelea huwa wanaongea Kiingereza. Hii ilitokea kuwa changamoto kwa hivyo nikaamua ni kwa nini nisisome ili mimi name niwe msomi. Ndio maana niko hapa,” akasema Bi Njoroge.
Tulipoongea na Bi Linda Nyaboanzu, wa umri wa miaka 23 na mama ya mtoto mmoja, binti huyu alisema alikatiza masomo yake ya kawaida baada ya kupata ujauzito ila akasema kuwa hatarudi nyuma kamwe.
“Nilijiunga na elimu ya ngumbaru mwaka wa 2017 na nimekuwa hapa kwa miaka mitatu sasa. Ninafanya mtihani mwaka ujao na lengo langu ni kuwa daktari siku za usoni.
Aidha alisema kuwa alipata ujazuzito mwaka wa 2010 na hivyo basi akalazimika kuacha masomo na kutafuta mbinu za kumlisha mwanawe.
“Kila kitu kilionekana kuwa shwari hadi mwaka wa 2010 nilipopata ujauzito. Nililazimika kuacha masomo ili nimtafutie mwanangu ila ndani ya moyo wangu, nilikuwa naomba lazima nimalize masomo yangu,” akasema.
Kulingana na Bw Patrick Moi mwenye umri wa miaka 35, kurudi kwake masomoni kuliwashangaza wazazi wake ambao mwanzoni hawakuamini kama ataweza kusoma.
“Nilipowaambia wazazi wangu kwamba ninataka kusoma na kuendelea mbele na masomo, walishtuka na wakanikejeli kwamba kwa vile sikuweza kusoma ujanani, itakuwa vigumu sana kwangu kusoma miaka ya uzeeni. Lakini nilishapiga moyo konde na kuamua kwamba lazima niendelee na masomo,” akasema kwenye mahojiano yetu.
Ngumbaru
Mmoja wa walimu wa wanafunzi hawa Bi Esther Macharia aliambia Taifa Leo kwamba alianza kufundisha kituoni hapo mwaka wa 2012, pindi tu serikali ilipoanzisha mradi huo wa elimu ya ngumbaru kwa wote.
“Nimekutana na watu wengi hapa ambao wengine kwa kutokana na changamoto za kimaisha hawakuweza kuendelea na masomo ujanani. Tumeona wengi wamekuja hapa na kufanya vyema katika mitihani ya kitaifa,” akasema Bi Macharia.
Afisa mkuu wa elimu ya watu wazima katika kaunti ndogo ya Nakuru Magharibi Dkt Samuel Muthee alisema kiu cha kutafuta elimu kimewafanya zaidi ya watu wazima 2,000 kurudi madarasani na kusoma katika kaunti hiyo.
Akiongea na Taifa Leo, Dkt Muthee alisema kuwa wengi bado wanaendelea kuitikia mwito wa kurudi darasani kusoma.
“Katika mpango huu kuna darasa la wale ambao hawajawahi kabisa kujua kusoma na kuandika. Wao wako na kitengo chao.
Kisha kuna kitengo cha wale ambao walifanya elimu ya msingi lakini bado hawajafaulu kwenda sekondari halafu kuna kitengo cha vijana ambao aidha waliamua kuacha masomo lakini baadaye wakaamua kurudi shuleni,” akasema afisa huyo.
Mwaka huu jumla ya wanafunzi wakongwe 75 ambao wanafanya mtihani wa KCSE kutoka kituo hicho ilihali wanafunzi 48 walifanya KCPE.
“Tunaomba serikali iangalie hili suala na kuhakikisha kwamba elimu hii inatiliwap pondo kwa sababu licha ya kuwa muhimu serikali bado haijawekeza vya kutosha kuimarisha elimu hii ya watu wazima,” akasema Dkt Muthee.