MAKALA MAALUM: Eneo ambapo wanawake wanaishi kivyao mbali na wanaume
Na MARY WANGARI
UMEWAHI kufikiria kuhusu eneo ambapo wanawake wanaishi kivyao mbali na wanaume katika mazingira tofauti?
Iwapo la, basi hujasikia kuhusu kijiji cha Umoja Uaso, ambacho ni eneo maalum wanakoishi wanawake pekee na ni marufuku kwa wanaume kuingia huko.
Umoja Uaso, iliyo karibu na Mto Uaso Nyiro, mjini Archers Post, katika Kaunti ya Samburu, ni kijiji cha aina yake kinachoweza tu kuelezwa kama hifadhi na himaya ya wanawake ambapo wanaume ni wageni wasiohitajika asilani.
Wazo la kuanzisha jamii ya wanawake pekee lilimjia mwasisi Rebeca Lolosoli takriban miaka 30 iliyopita alipokuwa akiuguza majeraha na kupata nafuu kitandani katika hospitali aliyolazwa.
Hata hivyo, wakati huo hakutarajia kuwa wazo hilo lingegeuka mwanga wa tumaini na kimbilio kwa mamia ya watoto na wanawake katika Kaunti ya Samburu.
Lolosoli alijipata amelazwa hospitalini baada ya kupokea kichapo cha mbwa kwa kuamua kuwahamasisha wanawake katika kijiji chake kuhusu haki zao, lakini hilo halikumvunja moyo.
Badala ya kuingiwa na woga na kujificha, mwanamke huyo jasiri aliamua kuleta mabadiliko na hapo ndipo alipoungana na kundi la wanawake 15 na kuanzisha Kijiji cha Umoja mnamo 1990.
Wanawake hao walikuwa manusura wa ubakaji uliotekelezwa na wanajeshi wa Uingereza na walijipata hawana pa kwenda baada ya waume wao kuwadhulumu na kuwatema.
Jamii pia iliwatenga kwa madai kuwa walikuwa wameletea jamii aibu, na hapo ndipo wazo la kuanzisha makao ya wanawake pekee lilipochipuka.
“Nilibakwa na wanajeshi wa Uingereza. Nisingeweza kuolewa kutokana na uovu walionitendea wanajeshi hao. Nilisikia kuhusu kijiji hiki kupitia uvumi kijijini. Nilijawa na raha tangu nilipowasili. Walinipa mbuzi na maji. Nikaanza kujihisi salama,” anasimulia Seita anayemtunza mjukuu wake.
Kadri mpito wa wakati ulivyojifumbua, ndivyo kijiji hicho kinavyopanuka na kuwa kimbilio kwa idadi kubwa ya wanawake na wasichana wanaotoroka ukeketaji, ndoa za mapema, dhuluma katika ndoa, ubakaji na mambo mengine ambayo ni kawaida katika utamaduni wa Samburu unaotawaliwa pakubwa na taasubi ya kiume.
Kituo hicho sasa kimegeuka kivutio mojawapo cha watalii nchini na kimataifa na kujitwalia umaarufu tele.
Hata hivyo, haijawa safari rahisi kwa Lolosoli ambaye amejipata mara kwa mara akikabiliwa na uhasama kutoka kwa wanaume wenye ghadhabu ambao wamemshambulia mara kadhaa, kama anavyosimulia katika mtandao wa kijamii wa YouTube wa shirika la kimataifa la CBS.
Judy Lelumba alikuwa na umri wa miaka 24 alipoozwa kwa mumewe aliyekuwa na umri wa miaka 54. Maji yalizidi unga kutokana na tabia ya mumewe kumpiga kila mara jinsi anavyosimulia.
“Alianza kunipiga nikatoroka. Niliporudi akaendelea kunipiga na hapo ndipo nikaamua kutoroka na kuapa sitawahi kurudi kwake tena,” anasema mama huyo mjamzito aliye na watoto wawili .
Wanawake na wasichana wanaotoroka masaibu yanayowakumba, hukimbilia kijiji hicho ambapo hujifunza jinsi ya kulea watoto wao, kufanya biashara na kujitegemea kimapato pasipo hofu kuhusu dhuluma na ubaguzi kutoka kwa wanaume.
Wanawake hao pia hushirikiana katika majukumu yote kuanzia ujenzi wa nyumba hadi shughuli za kujichumia riziki kwa kutengeneza mapambo mbalimbali yanayouziwa watalii.
“Huwa tunagawana kwa usawa mapato tunayopata huku yanayosalia tukiweka katika hazina ya pamoja na kuyatumia tu dharura inapotokea kama vile ugonjwa,” anasema Venusi Lalapol ambaye ni mama wa mtoto wa mwaka mmoja.
Kinyume na inavyotarajiwa kwa kijiji kama hiki ambacho wanaume hawaruhusiwi, kuna idadi kubwa ya watoto wachanga, jambo ambalo hawachelei kufafanua.
“Kulingana na mila yetu si vyema kwa mwanamke kukosa watoto. Watoto ni muhimu na ndio utajiri wa mwanamke hata kama hajaolewa. Ingawa tunaishi kando na wanaume, tungali tunavutiwa nao.
“Si vyema kuwa na watoto bila mume kulingana na utamaduni wetu. Lakini ni vibaya hata zaidi kukosa watoto kwa kuwa bila watoto wewe si chochote,” anafunguka mwanamke mmoja mchanga mwenye watoto watano wenye baba tofauti.
Kama anavyoeleza Judith, 19, aliyekimbilia kijiji hicho kutafuta usalama baada ya ‘kuuzwa’ kwenye ndoa akiwa na umri wa miaka 13 kwa mzee wa miaka 57, wanawake wachanga, wanaruhusiwa kwenda kwa wapenzi wao lakini hawaruhusiwi kuwaleta wanaume kijijini humo.
Wanawake hao hufurahia fursa ya kipekee ya kufanya mambo ambayo kwa kawaida hawangeweza kuyafanya hapo mbeleni.
“Nimejifunza kufanya mambo hapa ambayo kwa kawaida ni marufuku kufanya katika jamii. Ninaruhusiwa kujitafutia hela na mimi hujivunia mno wakati watalii wanaponuna mapambo yangu,” anasimulia Leila Nagusi, mwanamke wa umri wa makamo, ambaye ni mama wa watoto watano.
Kwa sasa kijiji hiki kimegeuka kivutio cha watalii kutoka humu nchini na wale wa kimataifa. Wanawake wanaoishi humo hutoza ada fulani ya kiingilio kwa watalii wanaowatembelea huku wakitumai kwamba wageni hao watanunua mapambo wanayotengeza.
Hela wanazopata hutumika kununua chakula, mavazi na kuwezesha makao kwa wote wanaoishi kijijini humo.
Kwa sasa wanawake hao hawana budi kutazama mbele na kusahau masaibu yaliyowakumba baadhi yao mikononi mwa wanajeshi wa Uingereza waliokuwa wakifanya mazoezi eneo la Samburu.
“Wanajeshi wa Uingereza walinipata nilipokuwa nikichanja kuni. Walikuwa watatu. Walinibwaga chini. Tangu siku hiyo huwa ninazidiwa na uchungu moyoni kila ninapokumbuka,” anasimulia Ntipayo ambaye ameishi kijijini humo kwa takriban miaka 20.
Kundi la wanawake kutoka kijiji cha Umoja liligonga vichwa vya habari mnamo 2003 lilipokutana na mawakili kutoka shirika la Uingereza la Leigh Day. Mawakili hao walikuwa wamezuru Archers Post kwa lengo la kutoa usaidizi kwa wakazi wa eneo hilo waliokuwa wamejeruhiwa na mabomu yaliyokuwa yameachwa na jeshi la Uingereza.
Hapo ndipo wanawake hao walipopata fursa ya kufungua nyoyo zao kuhusu makovu ya machukizi waliyotendewa hadi miaka 30 iliyopita. Idadi kubwa ya wanawake hao walisimulia kuhusu kuvamiwa na kubakwa na magenge ya wanajeshi walipokuwa wakichanja kuni au kuchota maji.
Martin Day, mmojawapo wa mawakili walioombwa kutoa usaidizi kwa wanawake hao, alikusanya ushahidi ikiwemo stakabadhi asilia za ripoti za polisi na ripoti za matibabu ikiwemo watoto suriama kutokana na Wasamburu na Waingereza.
Licha ya wakili huyo kuwasilisha matokeo yake, Idara ya Kifalme ya Jeshi na Polisi Uingereza (RMP) ilihitimisha kwamba stakabadhi zote hizo zilikuwa ghushi ikiwemo ushahidi thabiti wa watoto chotara ambao ulikuwa dhahiri.
“Hawakufanya uchunguzi wowote wa DNA kuhusiana na watoto suriama kwa kuwa inakadiriwa wanajeshi kati ya 65,000 na 100,000 huenda walikuwa nchini Kenya wakati wa kipindi hicho cha miaka 30,” alisema Day akinukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa.
Iwapo hilo linakustaajabisha, hakuna kilichomwandaa Day kwa mshtuko uliomsubiri alipouliza kuhusu takriban nakala 500 za ushahidi aliokuwa amekusanya baada ya RMP kukamilisha uchunguzi wake.
Alielezwa kwamba nakala zote hizo zilikuwa zimetoweka na hadi leo ushahidi huo haujawahi kupatikana.
Japo kesi hiyo bado haijatamatishwa, ni muhali mno kuiendeleza bila stakabadhi hizo asilia jinsi alivyofafanua Day.
“Tulikusudia kuitisha fidia kwa wanawake na wasichana walioteseka mikononi mwa wanajeshi. Maisha yao yaliharibiwa kabisa,” alisema wakili huyo.