• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
MAKALA MAALUM: Mandhry, msikiti ambao umedumu kwa zaidi ya karne nne

MAKALA MAALUM: Mandhry, msikiti ambao umedumu kwa zaidi ya karne nne

Na FARHIYA HUSSEIN

KUNA mandhari mengi ya kupendeza katika Pwani ambayo yatabakia kuwa historia daima.

Msikiti wa Mandhry ni miongoni mwa majengo maarufu ya kihistoria katika eneo la Mji wa Kale mjini Mombasa, ambako kuna mambo mengi ya kihistoria.

Mji wa Kale ni eneo linalojulikana katika historia ya nchi hii tangu enzi za Waarabu kutoka Omani walipofika kwa ajili ya kuwasaidia Waswahili kupambana na Wareno.

Waumini wengi wa dini ya Kiislamu wanaoishi mtaa wa Kibokoni ulioko eneo hilo la Mji wa Kale, wanaendelea kufanya ibada zao katika msikiti huo wa Mandhry, mmojawapo ya misikiti ya kale zaidi mkoani Pwani.

Msikiti huo uliojengwa mnamo mwaka 1570 na kurekodiwa kuwa wa tatu maarufu hapa nchini, ungali uko imara hata baada ya kuwako kwa kipindi cha miaka 449 iliyopita. Waumini wanaoishi mtaa huo wa Kibokoni na sehemu za jirani wanaendelea kuutumia kwa sala na ibada zao.

Viongozi wa Omani waliamrisha ujenzi wa msikiti huo kwa ajili ya Waarabu kuendeleza sala na maombi yao na pia kusambaza dini ya Kiislamu katika sehemu nyingine za Pwani.

Kulingana na baadhi ya watu wa eneo hilo waliohojiwa, jina la ‘Mandhry’ limetokana na familia iliyoishi mtaa huo wa Kibokoni wanaofahamika kama Wa-Mandhry, ukoo ambao ulitoka huko Oman zama za kale.

Waislamu kutoka sehemu mbalimbali za Kenya huwa wanafika kuzuru na kusali katika msikiti huo na hilo ni jambo linalosaidia pakubwa kueneza na kuhakikisha historia yake inadumishwa.

Kando ya msikiti huo, kuna kisima kinachojulikana kwa jina maarufu la ‘Kisima cha Mandhry’ ambacho kinaaminika kilianza kutumiwa tangu enzi za Waarabu kwa ajili ya kutawadha kabla ya kusali.

Mskiti huo ulioko barabara ya Sir Mbarak mjini Mombasa una rangi ya manjano tofauti na majengo mengineyo yaliyoko katikati ya mji huo ambayo yana rangi samawati. Hii ni kutofautisha rangi za majengo mengine na rangi iliyopakwa msikiti huo.

Juu ya jengo hilo la msikiti huo, kuna nguzo ndefu ambayo hutumiwa na mtu anayeadhini; anayewaita waumini wafike kuswali.

Sehemu hiyo ilikuwa ikitumiwa hapo kale lakini wakati huu, imebakia kuwa waumini washuhudie historia ya msikiti huo, kwani wanatumia chombo cha kupaaza sauti kuita waumini msikitini.

Mwaka 1990

Ilikuwa mwaka wa 1990, wakazi wa eneo hilo waliamua kujenga Madrassa kando kidogo na mskiti huo kwa ajili ya kuwafanya wakazi wa sehemu hiyo ya Kibokoni waweze kupata mafunzo ya dini pamoja na kusoma Kurani.

Kitabu kitakatifu cha Kuran pamoja na vya mafunzo ya dini ni baadhi ya vitu ambavyo vilitumiwa wakati wa enzi za Waomani walipokuwako na ziko hadi wakati huu. Majengo ya kihistoria yameendelea kubakishwa huku yakifanyiwa marekebisho machache tu.

Baadhi ya watu wa Pwani ambao babu zao waliwasimulia historia ya jinsi Mombasa ilivyokuwa, wanasema kuwa mabaharia wakiongozwa na Vasco Da Gama walijaribu kuuteketeza mtaa huo wa kihistoria na kuuchoma, lakini msikiti ulibakia.

Hata hivyo, wakazi wa Pwani wameweza kufaidika kwani tafrija za utamaduni zinazofanyika mara kwa mara na kujulikana kama ‘Swahili Culture’, zinasaidia pakubwa kuhakikisha majengo ya kihistoria pamoja na vyakula yanabakia kuwa vivutio kwa watalii wa hapa nchini na ng’ambo.

Ngome ya Fort Jesus na hoteli ya kwanza ya Africa Hotel, kituo cha kwanza cha polisi Mombasa na duka lililokuwa maarufu la Ali’s Curio Shop ni miongoni mwa majengo ambayo yanabakia kuwa ya kihistoria hapa nchini.

You can share this post!

Serikali sasa yaahirisha kufunguliwa kwa shule

TAHARIRI: Tuzishangilie Gor, Bandari katika CAF

adminleo