• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
MAKALA MAALUM – Prof Oniang’o: Wanaume Gen Z wawache uzembe

MAKALA MAALUM – Prof Oniang’o: Wanaume Gen Z wawache uzembe

NA SAMMY WAWERU

AKITAMBULIKA kwa uweledi wake katika masuala ya lishe, mifumo ya chakula na kilimo, Prof Ruth Oniang’o hana hofu kuzungumza yaliyo moyoni mwake.

Akiwa amehudumu katika nyanja mbalimbali sekta ya kibinafsi na umma, nyadhifa za juu, Msomi huyu anasema kamwe hana furaha na wanaume wa kizazi cha kileo.

Hata ingawa si wote, akiwalinganisha na wa enzi za zamani anaona tofauti kubwa sana kimalezi na kimaadili.

Kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza, Prof Oniang’o anataja uwajibikaji kimajukumu hususan kwenye familia kama gapu inayozidi kuwa pana.

Kuanzia Jeneresheni ya Zama za Zama na ya Alpha, mtaalamu huyu atakayetinga miaka 78 baadaye mwaka huu (2024), anasema gapu kimaadili ni kubwa kiasi cha kumtia hofu.

Prof Ruth Oniang’o, mtaalamu wa masuala ya Lishe Bora, Kilimo na Mifumo ya Chakula. PICHA|SAMMY WAWERU

Anakosoa Jeneresheni ya Milenia, Z na Alpha, anazohoji zimekwama kwa wazazi kutekelezewa majukumu ambayo wao wenyewe wanaweza kuyamudu.

Zilizowatangulia zikiwa ziliwajibika kukithi familia zao mahitaji muhimu ya kimsingi, za sasa Prof Oniang’o anasema mwelekeo wa dira yao umepotoka na kupotea.

“Awali, wanawake walikuwa wakisalia nyumbani kulinda watoto na maboma, ili wanaume wakirejea wanapata kila kitu kikiwa shwari. Sasa, mambo yamebadilika,” anasema.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Dijitali, Prof Oniang’o alielezea wasiwasi wake kuhusu wanaume wa kizazi cha kisasa wanaotegemea wazazi wao au waliotwikwa jukumu kuwalea wakiwa wachanga, akisema tabia wanazoonyesha zinaelekezwa kwa familia zao; watoto.

“Tunawaona wakikaa bila kufanya kazi, wanachothamini zaidi ni kupiga siasa na kuchangia kiduchu sana katika malezi ya familia. Hayo yanawashushia hadhi yao kama ‘vichwa’ kwenye familia,” akasema msomi huyo.

Huku kizazi cha Jeneneresheni Z wengi wakiwa chuoni na wengine wamefuzu, Prof Oniang’o anasema umewadia wakati kuwarejesha kwenye laini.

Prof Ruth Oniang’o, mtaalamu wa masuala ya Lishe Bora, Kilimo na Mifumo ya Chakula wakati wa mahojiano na Taifa Dijitali Jijini Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU 

“Tunapaswa kuwakumbusha kuhusu majukumu yao kama wanaume, na tuwashauri wasiige mfano mbaya wa waliowazidi kimiaka,” anasisitiza.

Mwanafilosofia huyu Mstaafu wa Masuala ya Sayansi ya, Chakula na Lishe Bora, hutetea vijana na anasema haja ipo kuwajuza mila, tamaduni na itikadi za Kiafrika.

Muacha mila ni mtumwa, tujivunie itikadi zetu kama Waafrika, Prof Oniang’o anaamini.

“Tunapaswa kuithamini mizizi chanya ya utamaduni wa Kiafrika. Wanaume, ni wakati wa kujitokeza, kutunza familia zenu, kuchangia katika maendeleo, na kusaidia kuimarisha wanawake wetu,” anasisitiza.

Akirejelea majukumu ya wanaume na wanawake wakati wa ujana wake, anaona umuhimu wa jinsia zote mbili kutimiza majukumu yao.

“Wanawake wanatekeleza jukumu muhimu katika mfumo wa chakula. Tunahitaji kuwathamini kwa sababu bila chakula, hatuwezi kuishi. Zamani, ilikuwa wanaume ndio wanatafuta chakula, japo sasa wanawake ndio wametwikwa majukumu hayo. Ni kinaya! Wanaume, haswa kizazi cha kileo waamke,” anashauri.

Katika kauli yake, anaainisha majukumu ya wanawake kupikia familia na waume kusaka na kuleta chakula.

Prof Ruth Khadaya Oniang’o alizaliwa Septemba 9, 1946, na alihudumu kama Mbunge Maalum kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kati ya mwaka 2003 na 2007.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua aapa kuadhibu wanasiasa watundu Rift Valley

Mti wa kitamaduni ulioanguka unavyozua hofu  

T L