• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Makanga mbioni kufuta nambari za simu kwenye magari kwa hofu ya kusemwa na abiria

Makanga mbioni kufuta nambari za simu kwenye magari kwa hofu ya kusemwa na abiria

NA LABAAN SHABAAN

UKIABIRI matatu mojawapo ya Kampuni ya ByBuss Trans Sacco na ukose kufurahia huduma zao, utapanda mlima sana kuwasilisha malalamishi kwa usimamizi wa shirika hilo.  

Hii ni kwa sababu ya hulka ya makondakta kufuta namba za mawasiliano zilizobandikwa ndani ya magari.

Yamkini tabia hii inalenga kuficha utovu wao wa maadili kwa wamiliki wa mabasi ya usafiri.

Taifa Leo imebaini haya katika basi la ByBuss Trans Sacco ambalo huhudumu kati ya Thika na Nairobi.

Katika matatu moja, nambari za mawasiliano zimefutwa.

Hii itamuwia vigumu kwa abiria kupata nambari za simu ili kulalama ama hata kuwapa mjibizo wa sifa na mapendekezo mengine.

Katika basi hilo kuna bango lenye notisi kwa abiria kuripoti matukio ndani ya chombo cha usafiri.

Wateja wanatakiwa kutoa ripoti kuhusu kutofikishwa mwisho wa safari, lugha ya matusi, muziki wa sauti ya juu na visa vingine vya utovu wa maadili vinavyohusisha wahudumu wa matatu.

Mnamo Desemba 2023, tukio la ‘kondakta’ wa kampuni hii kumpiga kofi abiria lilisambaa mitandaoni na kuibua hisia mseto.

Dhuluma, lugha ya matusi, na kutozwa nauli ya juu ni baadhi ya matatizo ambayo wasafiri wa vyombo vya uchukuzi wa umma hupitia mikononi mwa wahudumu wa matatu.

Kulingana na kanuni ya uendeshaji wa Magari ya Usafiri wa Umma (PSV), matatu zote zinafaa kuweka wazi nambari za simu ili abiria wawasiliane na dawati la wahudumu wa wateja.

Kanuni hii kadhalika inamhitaji msafiri kutuma mjibizo wa suala ibuka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) ili kufanikisha utatuzi wa mgogoro.

Endapo mzozo kati ya shirika la usafiri na mteja halitasuluhishwa ipasavyo, NTSA hubatilisha leseni ya operesheni ya usafiri.

  • Tags

You can share this post!

Wanaume wa SDA si washerati, asema mhubiri na kuvutia rundo...

Mgawanyiko Mlimani: Hofu matukio ya 1992, 1997 yanajirudia

T L