Makala

Maktaba ya kipekee Tharaka Nithi iliyoleta teknolojia ya mawasiliano mashinani

Na FRIDAH OKACHI October 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ZAIDI ya wakazi 10,000 kutoka eneo la Gatunga, Kaunti ya Tharaka Nithi watafaidika na huduma za maktaba ya kipekee baada ya kukamilika kwa ujenzi uliofadhiliwa na kaunti pamoja na serikali ya Amerika.

Maktaba hiyo ya kipekee iliyo na huduma za Mawasiliano na Teknolojia (ICT) inatoa fursa kwa wakubwa na wadogo kujifunza yanayojiri kote duniani na kuongeza maarifa.

Kulingana na Gavana wa Tharaka Nithi, Bw Muthomi Njuki, wanafunzi kutoka shule za msingi 63 watapata uwezo wa kusoma vitabu vya historia yao na mataifa mengine.

Bw Njuki alisema wakazi ambao ni wakulima watafaulu kufahamu mambo yanayojiri kuhusiana na kilimo.

“Tumewapa watoto wetu nafasi ya kusoma zaidi kando na mafunzo wanayopata pale shuleni. Serikali ya kaunti itawekeza pakubwa kuhakikisha milango yake haitafungwa na kutoa fursa murwa kwa wakazi kujifunza mbinu za kisasa za biashara,” alisema Bw Njuki.

Mkurugenzi wa Misheni ya USAID Bw David Gosner pamoja na gavana wa Tharaka Nithi Bw Muthomi Njuki wakati wa ufunguzi wa maktaba spesheli eneo la Gatunga. Picha|Fridah Okachi

Ndani ya maktaba hiyo, yapo maeneo tofauti muhimu kwa watu wote. Sehemu ya watoto ikitengwa na vitabu pamoja na vipakatalishi ambavyo viliwekwa masomo maalum.

Mkazi wa Gatunga Bw Onesmus Mutembei, alisema upande mwingine umetengwa kituo cha ICT ambacho kinatoa huduma za mtandao kwa wakazi ambao ni wakulima.

“Wakati tulitembelea maktaba hii ya kidijitali, tulioana aina ya mimea mbalimbali ambayo inastahili kupandwa kwa wakati huu. Pia, inatuwezesha kufahamu kiwango cha mvua ambayo itanyesha wakati huu.”

“Bw Mutembei alisema kuwa maktaba hiyo ya jamii inawakaribisha wafadhili wa vitabu vya kisasa na historia, huku wazee wa jamii ya Tharaka wakipata nafasi ya kuweka historia ya jamii hiyo katika vitabu na kuwezesha vizazi vijavyo kupata mafunzo ya walikotoka.

Maktaba ya kijamii ya teknolojia ya mawasiliano katika Kaunti ya Tharaka Nithi. Picha|Fridah Okachi

Kadhalika, wanawake wanapata fursa maalum ya kupata mafunzo ya kipekee, haswa dhidi ya vita vya kijinsia na mafunzo ya kibiashara.

Kiongozi wa Muungano wa wanawake Tharaka Bi Aniceta Kiriga alisema wanawake wanaoshona watatumia maktaba hiyo kusambaza kazi zao mitandaoni.

“Kwa sasa biashara ya ushonaji inatoa fursa kwa wanawake hawa kuuza bidhaa zao katika nje ya nchi na kote duniani bila kutegemea wakazi wa eneo hilo pekee,” alisema Bi Kiriga.