MALENGA WA WIKI: Jinsi hafla ya kumuenzi Maulidi Juma ilivyofana Rissea
Na HASSAN MUCHAI
ILIKUWA ni furaha kubwa kwa mkongwe wa nyimbo za Taarab, Maulidi Juma, baada ya “kuzikwa akiwa hai” mjini Mombasa juma lililopita.
Maulidi ambaye atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika uimbaji wa nyimbo za Taarab, amekuwa akiugua kwa muda. Baada ya habari zake kuangaziwa sana kupitia gazeti la ‘Taifa Leo’ na ‘Taifa Jumapili’, wafuasi wake waliamua kuungana pamoja ili kumtembelea na kumuenzi akiwa hai.
Si ajabu kwamba watu wengi humdhania Maulidi kuwa mwimbaji tu. La hasha! Maulidi ni mtunzi stadi wa mashairi na anaweza kutunga shairi moja kwa moja na kuliwasilisha bila kunukuu mahali popote.
Hili lilidhihirika mnamo Jumamosi iliyopita wakati mzee huyo anayetambuliwa kwa vibao vyake kama ‘Waringia Nini’, ‘Yule Hana Maumivu’, na ‘Vishindo Vya Mashua’ kutunga mishororo minne na kudai apewe chakula kwani alikuwa anahisi maumivu ya njaa!
Sherehe hiyo ya kufana iliwajumuisha waandishi wa haiba kubwa nchini mathalan Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Dkt Hamisi Babusa, Nuhu Bakari, Mzee Thomas Koskei, Juma Salim Makayamba, Lolani Kalu, Hassan Morowa miongoni mwa wengine.
Wengine walikuwa wanachama wa Chama cha WAKITA wakiongozwa na Mwenyekiti wao Abdul Noor, Naibu Mwenyekiti ndugu Kinyua King’ori, Wanto Warui na kadhalika. Pia walikuwepo wahadhiri kutoka vyuo vikuu ambao ni Henry Indindi, Andrew Watuha na Mohammed Khamis.
Sherehe za kumuenzi Mzee Maulidi zilifanyika katika ukumbi wa RISSEA ulioko ndani ya eneo la Fort Jesus. RISSEA ni kituo cha utafiti wa lugha ya Kiswahili na kimekuwa kikitumika sana kwa mikutano mbalimbali inayolenga kukuza lugha ya Kiswahili.
Aidha, wazo la kuwaenzi watu waliotoa michango yao katika kufanikisha ukuaji wa lugha ya Kiswahili lilianza mapema miaka ya ‘90 wakati wasanii na wanahabari walipoungana pamoja kumuenzi Hassan Mwalimu Mbega nyumbani kwake Kakuku, Ekalakala Machakos.
Waasisi wa wazo hili walikuwa Profesa Ken Walibora, Wallah Bin Wallah, aliyekuwa Naibu Gavana wa kaunti ya Mombasa Bi Hazel Katana, Hamisi Babusa, Nuhu Bakari na mwandishi wa makala haya, Bw Hassan Muchai miongoni mwa wengine.
Gazeti la ‘Taifa Leo’/’Taifa Jumapili’ lilidhamini kikao cha kwanza kwa kutoa mchango wa usafiri kwa wanachama mbali na kampuni ya Nation Media Group (NMG) kupitia idara yake ya masuala ya kijamii (Coporate Affairs) kufadhili kwa njia ya mchango wa mavazi miongoni mwa michango mingine.
Mghani wa mashairi Mzee Abdallah Mwasimba hakuachwa nyuma kwenye safari hii.
Ziara ya tatu ilifanyika miaka mitatu iliyopita kijijini Matondoni, Lamu.
Ziara hii ilikuwa ya kumuenzi mtaalamu wa masuala ya kiasili, Kiswahili na utamaduni wa Uswahilini, marehemu Sheikh Nabhany.
Ziara hii iliwajumuisha Andrew Watuha, Henry Indindi, Hezekiel Gikambi, Profesa Rayya Timammy, Mahmoud Mau, Wallah Bin Wallah, Alamin Siwa Somo na Hassan Muchai miongoni mwa wengine.
Ama kweli, sherehe ya juma lililopita ya kumuenzi Maulidi imefufua matumaini makubwa kwenye nyoyo za wapenzi wa mashairi.
Ni kupitia ushirikiano kama huu ambapo ushairi wa Kiswahili utaweza kudumishwa. Wasanii waliopata nafasi ya kuhutubia umati wa watu uliofika RISSEA walisifu wazo hili na kuitaka serikali kutwaa mfano huu wa kuwaenzi mashujaa wake na “kuwazika wakiwa bado hai’’.
Maulidi alikabidhiwa zawadi mbalimbali vikiwemo vyakula, nishani, vazi la kikoi na tarbushi miongoni mwa zawadi nyingine.Jambo lililojitoeza wazi siku hiyo ni kwamba, washairi wana ushirikiano wa kipekee na wako radhi kukutana na kusaidiana bila ya kuzingatia hadhi, kabila au tabaka la mtu.