MALEZI: Chuja habari unazoweka mtandaoni kuhusu watoto wako
WAZAZI wengi siku hizi huwa wanafuatilia waliko watoto wao na shughuli zao za mtandaoni ili kuhakikisha wako salama.
Baadhi ya watoto hawana tatizo na hili kwa kuwa linawafanya wajihisi salama.
Lakini wengine wanahisi wazazi wao wanawadhibiti kupita kiasi jambo ambalo linaathiri maisha yao ya kijamii na ya shuleni.
Baadhi ya vijana hutafuta njia za kuhepa vidhibiti hivi, ambavyo vinaweza kufanya mambo kuwa mabaya zaidi.
Wataalamu wa malezi dijitali wanasema kwamba wazazi wanapokuwa wakali sana, watoto wanaweza kuasi na kuvunja sheria.
Ni bora kuzungumza na watoto kwa uwazi kuhusu teknolojia na kuwafundisha kuchagua kwa uangalifu kile wanachofanya.
Watoto wanapokuwa wakubwa, wanapaswa kujifunza kuwajibika mtandaoni, na wazazi wanapaswa kuacha kuwafuatilia. Baadhi ya vijana wanafikiri kwamba wanapaswa kuachiwa uhuru wao wakitimiza umri wa miaka 16.
Ingawa hii inawezesha wazazi kufuatilia maisha ya familia, teknolojia mpya huleta changamoto mpya kwa wazazi kama vile kutegemea intaneti na programu za malezi kwa ushauri.
Wataalamu wanasema ingawa mtandao unaweza kuwapa wazazi fursa ya kubadilishana habari kuhusu mbinu na mazoea ya ulezi, ni muhimu mzazi afanye hivyo kwa kiasi ili asianike habari zinazoweza kuhatarisha maisha ya watoto wake.
“Mzazi hafai kuanika habari nyingi kuhusu familia yake katika mitandao ya kijamii. Hapa tunazungumzia picha na maelezo ya kibinafsi ya mtoto,” asema mtaalamu wa malezi Cristina Ponte.
Anasema kutegemea mtandao na apu zinazotoa ushauri wa malezi kunafaa kuwa kwa kiasi huku mzazi akizingatia usalama wa mtoto na familia yake kwa jumla.
“Hii ni kwa sababu data za watoto zinaweza kufuatiliwa na kudakuliwa ili kutumiwa kwa malengo ya uhalifu au kwa manufaa ya kifedha ya watu na kuweka maisha yao kwenye hatari,” aeleza Ponte.