Mama aliyejitolea kukinga jamii dhidi ya maambukizi ya corona
Na SAMMY WAWERU
Huku virusi vya corona nchini vikionekana kupungua, historia ya wazalendo waliokuwa mstari wa mbele katika oparesheni kusaidia kudhibiti msambao ikiandikwa hii leo, Peris Wakarura hatakosa kujumuishwa kwenye listi.
Ni Mkenya mzalendo anayeendelea kuridhisha nyoyo za watu kutokana na ukarimu wake kujiunga katika vita dhidi ya janga la corona.
Kisa cha mgonjwa wa kwanza kilipotangazwa nchini, mwezi Machi 2020, sawa na wananchi wengine, Peris alipokea taarifa hiyo kwa mshangao.
Ugonjwa wa Covid-19, ambao kwa sasa ni janga la kimataifa, uliripotiwa mara ya kwanza Wuhan, nchini China, Novemba 2019, na maswali yaliyokosa majibu yalitawala mawazo ya Peris, “Ikiwa kweli Kenya inaweza kuwa mwenyeji wa gonjwa aliloliskia kwenye vyombo vya habari?”
Mnamo Machi 13, haikuwa siri tena, haikuwa habari za kimataifa kuhusu virusi hatari vya corona, kwani Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe alithibitisha taarifa ‘chungu’ Kenya ni mwenyeji wa Covid-19.
Peris ambaye ni Pasta Mmishonari, anasema alisali kwa muda wa siku tatu, kuombea taifa.
Eneo la Maguo, mtaa wa Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi, mama huyo ni mmiliki wa ploti, na siku chache kabla kisa cha kwanza cha corona kutangazwa nchini, alikuwa ameanza kuimarisha nyumba zake.
“Mimi hutegemea vibarua vya hapa na pale kusukuma gurudumu la maisha na kukimu familia yangu mahitaji muhimu ya kimsingi. Sijaweza kukamilisha kutengeneza nyumba za ploti ninayoishi na wanangu,” Peris ambaye ni singo matha wa watoto sita anaelezea.
Vyumba vya ploti yake ambavyo vingali mahame, vinahitaji kuimarishwa, kuwekwa mabati, kupiga kuta plasta, pamoja na kuweka madirisha na milango, kati ya mengine kukamilisha ujenzi.
Anafichua kwamba katika Kaunti ya Lamu, ni mkulima wa miti, baadhi ikiwa tayari kuvunwa. Siku moja baada ya mgonjwa wa Covid-19 kutangazwa nchini, Peris alipata mteja aliyeahidi kununua magogo ya miti yenye thamani ya Sh160, 000.
“Nilifahamisha wanangu, ndoto ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vyetu ilikuwa imetimia. Wote waliridhia habari hizo njema, na kufurahia hawataendelea kuhisi baridi tena,” Peris anadokeza.
Machi 16, mpango wa malipo ya miti ukaingiana, akapata kima cha Sh160, 000 pesa taslimu.
Mama huyo anasimulia kwamba alitenga Sh10, 000 pekee kufanya ununuzi wa bidhaa za matumizi ya nyumbani, nyingi zikiwa za kula.
Peris ambaye pia ni mwashi, akaweka mikakati namna ya kukamilisha ujenzi wa nyumba zake, ambazo zimekawia kuimarishwa.
Subiri, yaskie haya makuu. Mpango huo hata hivyo, Machi 17, ukachukua mkondo tofauti. “Usiku, niliskia sauti ya Mungu ikinihimiza niamke nianze kuokoa watu wake (Wa Mwenyezi Mungu) corona ni roho mbaya,” anakumbuka.
“Kwenye hotuba yake akithibitisha mgonjwa wa kwanza wa Covid-19, Waziri wa Afya alihimiza umma kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni, kupulizia kwa kemikali maeneo ya umma na kuvalia maski kila wakati. Kuokoa watu wa Mungu kunajumuisha vita dhidi ya adui huyu, na nikaamua kutumia mali yangu kutekeleza shughuli hiyo,” Peris akaambia ‘Taifa Leo’ wakati wa mahojiano.
Alifafanua kuwa, asubuhi ya Machi 17, alishauriana na mmoja wa wazee wa kanisa, Johnson Ngaruiya ambaye pia alishangazwa na uamuzi wake. “Nilisisitiza kujua kwa nini alijishughulisha sana na jamii, kiasi cha kuonekana kuasi familia yake. Aliniambia ndani yake alihisi kuokoa watu dhidi ya Covid-19 na kwamba Mola atakimu familia yake,” Ngaruiya akasema.
Mapato ya miti yaliyosalia, yote akaelekeza katika vita dhidi ya corona, hatua anayosema ilizua tumbojoto kati yake na baadhi ya wanawe. “Baada ya mashauriano na maafisa kadha wa Idara ya Afya, nilishauriwa kemikali bora kupulizia maeneo ya umma, na eneo nitakaponunua, Viwandani, Nairobi. Mapato ya miti yaliyosalia, Sh150, 000 nikayaelekeza kwenye misheni ya kupambana na corona,” anaelezea.
Kiasi cha pesa hizo, Sh130, 000 alitumia kununua dawa-kemikali, aina ya Sodium Hypochlorite (NaOCl·5H2O).
Aidha, fedha zilizosalia alinunua vitakasa mikono, sabuni ya majimaji, na maski za hospitali zilizopendekezwa na Wizara ya Afya.
Pia anasema alinunua vifaa vya kusaidia kutakasa mikono, pampu ya kupulizia maeneo ya umma kemikali, pampu ndogo kadhaa na stika za kampeni kuhamasisha kuangamiza virusi vya corona.
Oparesheni dhidi ya Covid-19 maeneo ya umma ikang’oa nanga. “Niliolenga katika utangulizi ni wahudumu wa bodaboda eneobunge la Ruiru (linalojumuisha Githurai na viunga vyake). Waziri Kagwe alieleza wasiwasi wake kuhusu wendesha bodaboda kuwa mtandao hatari kueneza corona kwani huhudumia watu wengi. Siku za kwanza watu walihofia sana,” akafafanua.
Kulingana na Peris, wanabodaboda waliridhishwa na jitihada zake, na kila walipomuona walimkaribisha kuwahudumia.
Mama huyo mkwasi wa utu, mkarimu na mcheshi anasema alihisi anafanya jambo linalofaa, na kupanua oparesheni yake kuhudumia jamii bila malipo.
Mbali na wahudumu wa bodaboda, alijituma kupulizia maeneo ya umma kama vile; masoko, vibanda vya kina mama mboga, milango ya majengo ya kupangisha na yale binafsi, matatu na magari ya kibinafsi, tuktuk, vituo vya afya – hospitali na zahanati, makanisa, vituo vya polisi, wanakolala watoto wa mitaa maarufu kama ‘chokoraa’, miongoni mwa maeneo mengine yanayotembelewa na watu kutafuta huduma.
“Kwa mfano, nina rekodi ya mabasi yote yanayohudumu kati ya mtaa wa Githurai na jiji la Nairobi. Ratiba yangu, siku sita kwa juma, huwa katika misheni kuokoa watu. Tangu nianze kutoa huduma, hakuna siku nimewahi kukosa, ila Jumapili pekee ambayo hupumzika. Ni wajibu alionipa Mwenyezi Mungu,” kwa furaha na tabasamu anaelezea.
Kabla kuanza oparesheni, huongoza kikosi chake kwa maombi, akisema sala kwa Mungu ni muhimu katika kila jambo, kabla kulitekeleza.
Ni uzalendo kwa taifa, ambao unaendelea kumvunia kongole, sifa na umaarufu chungu nzima. “Ikiwa kuna mama ambaye anapaswa kutambuliwa na serikali, muite huyu Peris. Kwa hakika mambo anayoendelea kufanya yametushangaza kama walinda usalama. Ameonyesha utu na uzalendo,” akasema afisa mmoja wa polisi, Kituo cha Polisi cha Kimbo kilichoko kilomita chache kutoka Thika Super Highway, akidokeza kwamba amekuwa akipulizia kila kona ya kituo hicho, ikiwamo afisi, seli, malango, sehemu hizo zikiwa chache tu kuorodhesha.
Hata hivyo, oparesheni hiyo haijakuwa rahisi. Mwaka wa 2007, Peris anafichua kwamba alihusika katika ajali mbaya na punda, wakati akisafirisha mizigo.
Anadokeza kwamba uti wake wa mgongo uliathirika kwa kiasi kikubwa, ajali iliyomlazimu kutumia kiti chenye magurudumu kinachotumiwa na watu wenye matatizo ya kutembea. Hali hiyo, aliendelea nayo kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.
Isitoshe, ni majeraha mabaya yaliyomuacha akiwa singo matha, mumewe alipomtoroka baada ya kuona ameshindwa kutembea.
“Watu walinisimanga, kuwa nitasalia kuwa kiwete, ila Mungu akaniponya. Huhudumia jamii, na kutembea nikiwa nimebeba pampu yenye lita 20 za kemikali si rahisi. Uzito huo hufufua matatizo ya mgongo kufuatia ajali niliyopata. Pia, nimeanza kushuhudia maumivu ya jointi za mikono,” anafafanua, akiongeza kwamba atasitisha oparesheni yake Kenya itakapotangaza na kuthibitisha kuwa huru dhidi ya Covid-19.
Alipoulizwa anavyofanikisha kufadhili oparesheni hiyo, alisema alikuwa amenunua kemikali, sabuni ya majimaji na maski, zitakazomsukuma miezi kadhaa.
Hata hivyo, alisema bidhaa hizo zinakaribia kuisha, na anahimiza Wakenya wasamaria wema kumpiga jeki.
Peris Wakarura ni mchungaji, na wahubiri wengi wanafahamika kutegemea kufadhiliwa na wafuasi wao.
Mama huyo, Pasta Mmishonari anafanya kinyume, ambapo anahudumia umma na jamii bila usaidizi wa anaolisha chakula cha kiroho.
Peris anasema makanisa na misikiti ilipofungwa, yake ‘haikifungwa’. Iliingia kwenye nyoyo za watu, kuwafikia, kuwafariji na kuwapa matumaini janga la corona ni la muda tu na litaisha.
“Kipindi cha corona, kimekuwa na nyakati ngumu. Kama watumishi wa Mungu, tunapaswa kuonyesha utu na kusaidia watu wanapotuhitaji, na huu ndio wakati wanatuhitaji zaidi, na si kuwalisha cha kiroho pekee, ila kuwasaidia kwa hali na mali,” anashauri.
Kando na kuonyesha utu na ukarimu kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19, Peris anafichua kwamba kwa muda wa miaka kadhaa amekuwa katika daraja la mbele kusaidia mayatima na watoto wa mitaa.