Mama aliyeshindwa kunyonyesha pacha wake watatu aletewa msaada
NA OSCAR KAKAI
NI saa nane mchana Ijumaa na Vivian Chepkite ameketi ndani ya nyumba yake ya msonge akiwa amewashika wanawe wawili kati ya pacha watatu ambao wanashindana kunyonya.
Kila mtoto mvulana ameshikilia titi la mamake. Mtoto wa tatu ambaye ni msichana ameshikwa na jirani akingojea nafasi yake kunyonya, lakini hakuna maziwa kwake.
Mama huyo mwenye umri wa miaka 30 katika kijiji cha Kapsimatia, kata ya Psurum, Pokot Magharibi ambaye alijifungua pacha watatu katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kapenguria kupitia upasuaji sasa anasema kuwa ameshindwa kuwanyonyesha kutokana na uhaba wa chakula na kukosa uwezo wa kuwalea.
“Nilipata mimba na baada ya miezi mitano nikawa mgonjwa na kuenda hospitalini. Miguu zangu zilifura na uzito ukaongezeka. Nilifikiria kuwa ilikuwa ugonjwa wa kawaida,” anaeleza.
Familia hiyo hata hivyo ilijawa na furaha wakati msanii wa nyimbo za injili kutoka Pokot, Christine Loyeye alipofika ghafla kwenye boma hilo na kutoa msaada cha chakula na bidhaa za matumizi ya nyumbani.
Akihadithia masaibu yake kabla ya msaada huo, Chepkite anasema kuwa aliuza kuku ndiposa akafika kwenye hospitali ya rufaa ya Kapenguria umbali wa kilomita 100.
“Nilianza kuumwa na nikaenda katika hospitali ya kaunti ndogo ya Chepareria lakini niliambiwa niende katika hospitali ya kaunti ya Kapenguria. Nilijifungua Aprili 11, 2024 kupitia upasuaji. Nilifikiri ilikuwa mtoto mmoja lakini nikaonyeshwa watatu,” anasema.
Bi Chepkite anasema kuwa wiki mbili baada ya kurudi nyumbani alianza kukumbana na changamoto.
“Hakuna maziwa kwenye matiti. Watoto wangu wanalia kila wakati wakishindana kunyonya. Ndio niliomba wasamaria wema na serikali kunisaidia,” anasema.
Mama huyo wa watoto wanne anasema kuwa mumewe hana ajira na hufanya vibarua ambavyo mapato yake ni duni.
“Hatukutarajia pacha watatu. Ni vigumu jambo hili kufanyika na lazima tujikaze ili wakue na afya hadi ukubwani,” Bi Chepkite anasema.
Anasema kuwa kuna uhaba wa maji kwenye kijiji hicho na wakazi hutembea zaidi ya kilomita 20 kupata bidhaa hiyo.
“Sisi huamka saa kumi na mbili asubuhi na kufika saa tano mtoni. Ukituma mwana boda boda anachelewa kuleta maji. Ni hali ngumu na mimi hushinda na njaa na watoto wananyonya kila saa. Tunafaa kuletewa maji hapa karibu,” anasema.
Mumewe Johnston Losharipo mwenye umri wa miaka 32 anasema kuwa hali si hali kwa sasa.
“Sikujua tutapata pacha watatu. Nilifikiria ni mtoto mmoja. Tukiwe kwenye chumba cha upasuaji, niliambiwa nilete nguo nikaleta za mtoto mmoja, wakaniambia nilete nyingine, nikaleta lakini nikarejeshwa kuleta nyingine za mtoto wa tatu. Nilishangaa na nikapigwa na butwaa sababu sina chochote. Nitalisha aje watoto hao ilihali mimi ni maskini hohehahe?”anauliza.
Anasema kuwa safari ya kulea wanawe haijakuwa rahisi kutokana na uchumi mbaya lakini wamejaribu kupata usaidizi kuyoka kwa familia, marafiki na majirani.
“Sina ng’ombe wala mbuzi. Tuko na shida nyingi eneo hili. Mwaka jana hatukuvuna sababu ya kiangazi. Marafiki wamenisaidia na chakula. Mimi hufanya vibarua nipate shilingi 50 ama 100 ya kununua kikombe cha maziwa. Majirani hunipa mahindi lakini wakati mwingine tunalala njaa,” anasema Bw Losharipo.
Mwimbaji Loyeye anasema kuwa alipokea habari kupitia mtandao wa kijamii ambapo picha za mama huyo zilikuwa zikisambazwa kisha akaanza kukusanya vyakula kutoka kwa wasamaria wema.
Anasema kuwa gharama ya kulea watoto hao iko juu sababu wanahitaji vitambaa vya kuwafunga na maziwa zaidi sababu maziwa ya mama mzazi hayatoshi watoto hao watatu.
“Madaktari walipeana ushauri kuwa wanunue maziwa zaidi. Watoto wanahitaji maziwa maalum ya dukani. Imekuwa vigumu kulea watoto hao,” anasema.
Anasema kuwa waliwakaribisha watoto hao licha ya suala hilo kuwa lisilo la kawaida kwa jamii ya Pokot.
“Sio jambo la kawaida na tunaomba wasamaria wema kuingia kati na kusaidia familia. Mama hawezi kuwanyonyesha watoto vyema sababu ya kula vibaya. Ninaomba mtu awasaidie tu na ng’ombe wa maziwa,”anasema Bi Loyeye.
Alitoa wito kwa maafisa wa lishe bora kupeana ushauri kuhusu jinsi ya kulisha watoto hao.