Mama aomba msaada kusafiri Vietnam kumuona bintiye kabla anyongwe kwa kosa la ulanguzi
MAMA Purity Wangui, mkazi wa kijiji cha Weithaga, Murang’a ni mwenye machungu anapotafakari kuwa bintiye atauawa nchini Vietnam baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa mihadarati.
Hii ni baada ya Margaret Nduta, 37, mnamo Machi 6, 2025, kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo mbili ya dawa aina ya kokeni kupitia Vietnam.
Alipewa adhabu hiyo ya kuuawa katika nchi hiyo, yenye sheria kali ya kupambana na ulanguzi wa mihadarati, licha ya taifa hilo kuwa ngome ya uovu huo.
Bi Nduta alikamatwa mnamo Julai 2023 akiwa safarini kuelekea Laos akibeba kokeni ndani ya mizigo yake.
Katika kijiji cha Weithaga, Kaunti ya Murang’a mama Wangui anatamani kusafiri hadi jiji la Chi Minh ili angaa aonane na binti yake ana kwa ana.
Lakini mama huyo anajiuliza ni kwa nini binti yake alijiingiza katika ulanguzi wa mihadarati katika nchi ya kigeni, kosa ambalo sasa huenda likachangia kuuawa kwake.
“Nawasubiri watu kadhaa wa familia yangu wajitokeze waandamane nami katika safari ya kwenda huko. Sharti nimwone kabla ya siku ya kuuawa kwake,” Wangui anasema, akifahamu fika kwamba hana fedha za kulipia nauli hadi Vietnam.
Baada ya kujulishwa na jirani mmoja kwamba kutoka Murang’a hadi Vietnam ni umbali wa karibu kilomita 8,100, anajibu: “Huo umbali hauwezi kulinganishwa na miaka hii yote ambayo nimekuwa mamake.”
Wakati wa mahojiano, Mama Wangui alisema anaweza kuamua kutembea kwa miguu hadi jijini Ho Chi Minh.
Anaonekana mwenye wasiwasi na machungu akikumbuka kuwa bintiye atauawa katika nchi za kigeni.
Mama Wangui anasema Bi Nduta alikuwa amemkubali Yesu kama mwokozi wa maisha yake na ni mcha Mungu.
“Huenda aliwekelewa kosa hilo au aliungana na watu wabaya. Nimemlea ndani ya maadili ya Kikristo……….. naomba msamaha kwa niaba yake. Namwomba Rais William Ruto kupitia mbunge wangu Ndindi Nyoro kulifuatilia suala hilo. Serikali ihakikishe kuwa binti yangu amerejeshwa nyumbani na afungwe gerezani nchini Kenya,” Wangui anasema huku akiwa mwingi wa machungu.
Vietnam ni kitovu cha ulaguzi wa dawa za kulevya katika eneo zima za Golden Triangle, eneo la makutano ya mipaka ya China, Laos, Thailand na Myanmar.
Walanguzi hutumia jiji la Ho Chi Minh kwa sababu linakaribiana na Cambodia, ambayo ni soko kubwa la mihadarati.
Alex Murumba aliyejitambua kama mmoja wa watu wa familia hiyo alimwomba Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi kutumia mbinu za kidiplomasia kuwezesha kurejeshwa nyumbani kwa Bi Nduta.
“Kama familia, tumejawa na wasiwazi. Hatuna uhakika kama Bi Nduta ambaye aliondaka nchini 2023 kusaka ajira ng’ambo aliishia kuwa mlanguzi wa dawa za kulevya,” Bw Murumba anasema.
Anasema familia hiyo imeingiwa na hofu kwamba endapo Nduta hatakata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa Machi 6, 2025, atauawa.
Nchini Vietnam, yeyote anayepatikana na hatia ya kupatikana au kusafirisha zaidi ya gramu 600 ya dawa aina za heroine au cocaine au zaidi ya kilo 2.5 ya “methamphetamine” adhabu yake ni kifo.
IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA