Mama asimulia alivyotupwa jela kwa kujiondoa kwa mwajiri katili Saudi Arabia
MNAMO 2021, Susan Njeri aliwapa busu la kwaheri watoto wake wawili na kuabiri ndege kuelekea Saudi Arabia kutafuta riziki.
Akiwa amebeba mkoba mdogo na ndoto kubwa, alitumai kupata kipato nafuu na kuinyanyua familia yake katika uchochole ikiwemo kuwakikishia watoto wake siku njema za usoni.
Licha ya ripoti chungu nzima kuhusu wajakazi wa Kenya wanavyodhulumiwa na kunyanyaswa katika nchi za Mashariki ya Kati, Bi Njeri alipania kustahimili changamoto hizo na kuibuka imara zaidi.
Lakini badala ya malipo bora na nafasi alizotarajia, safari yake iligeuka kuwa ya kuvunja moyo na kubadilisha maisha.
Kabla ya kusafiri, hakuwa na hela za kuandaa stakabadhi zake, hivyo alilazimika kuitisha usaidizi kutoka kwa wakala wa Nairobi, ambaye, kwa kuelewa hali yake, hakumtoza ada yoyote.
Hakujua wakati huo kuwa safari iliyonuiwa kuokoa familia yake kutoka kwenye magumu, ingemtumbukiza katika mojawapo ya sehemu zenye masaibu zaidi maishani mwake.
Nyumbani, nafasi za ajira ziliadimika na kidogo alichopata kutokana na kazi za vibarua hakingeweza kulisha wala kuwatunza watoto wake – waliokuwa Gredi 9 na Gredi 5 – shuleni.
Wiki za kwanza mbili nchini Saudi Arabia zilimtamausha na kusambaratisha upesi ahadi ya maisha bora aliyosifiwa na mawakala wa ajira.
Anasema alipelekwa katika familia ambapo alifanya kazi saa nyingi bila kupumzika.
Pasipoti yake ilitwaliwa alipowasili, akazuiwa kuwasiliana na familia yake na alipolipwa mshahara wake, ulichelewa.
Punde si punde, ilikuwa wazi hatima yake ilikuwa mikononi mwa mwajiri katika taifa ambalo hakuelewa lugha wala utamaduni wake.
“Nilimfahamisha mama yangu tu kuwa nasafiri Saudi Arabia ili niwalishe watoto wangu, aliokubali kuwatunza nilipoondoka.
“Nilijawa na matumaini, lakini maisha huko yakageuka kuwa mabaya zaidi. Kama mjakazi, niliamka kabla ya kila mtu na kulala usiku wa manane. Kandarasi ilisema saa nane za kazi, lakini sikuwa na siku za kupumzika. Wakati mwingine nilitukanwa na kutishiwa na nikahisi nimenaswa,” alisimulia Njeri katika mahojiano na Taifa Leo.
Baada ya kustahimili hali hiyo kwa miezi saba, alifanya uamuzi ambao ungebadilisha mkondo wa maisha yake.
Alimwacha mwajiri wake na kuanza kwenda nyumba hadi nyingine akisaka malipo bora na mazingira yenye utu.
Sawa tu na wafanyakazi wengi wa kigeni, alitegemea mitandao isiyo rasmi na masimulizi bila kujua kumwacha mwajiri wake bila kibali rasmi ni hatia chini ya sheria za leba na uhamiaji Saudia.
Kwa karibu miaka mitatu, alifanya kazi huku akiandamwa na mamlaka.
Kisha bahati yake ikafika kikomo, akakamatwa, tukio lililoashiria mwanzo wa masaibu yake ya miezi sita yanayomtaabisha hadi sasa.
Bila mtafsiri wala wakili, Njeri alizuiliwa korokoroni kisha akarushwa jela ya Dhahban kwa kuwa Saudi Arabia kinyume cha sheria – licha ya stakabadhi zake za usafiri kushikiliwa na mwajiri wa zamani.
Anaeleza maisha katika jela hiyo kuwa ya kikatili. Seli zilifurika, hazikuwa na vijisehemu vya kupitishia hewa wala usafi.
Anasema chakula kiliadimika na kilikuwa duni, hakukuwa na huduma za afya za kutosha huku wafungwa wakishindwa kuwasiliana na familia zao.
“Wengi wetu, Wakenya na wengine, hatukuzungumza Kiarabu. Hakukuwa na watafsiri. Hatukuelewa mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yetu au jinsi ya kuitisha mahitaji ya kimsingi. Niligundua mamia ya Wakenya wanateseka jela pasipo familia zao nyumbani kufahamu. Tulilala sakafuni, wakati mwingine bila magodoro au blanketi. Ungeugua na kukaa siku kadhaa bila kuona daktari,” alisema.
Alilemewa kihisia hasa kwa sababu ya kuwa mbali na watoto wake akihofia kwamba huenda hatawaona tena milele.
Aliachiliwa huru kupitia njia asiyotarajia baada ya mwajiri wake wa mwisho kulipa faini na gharama za usafiri zilizohitajika, na kumwezesha kurejeshwa Kenya.
“Nilibahatika. Bila usaidizi wake, labda bado ningekuwa jela.”
Alirejea Kenya wiki tatu zilizopita akiwa mchovu kupindukia, matatizo ya kisaikolojia na bila chochote cha kuonyesha alikuwa ughaibuni kwa miaka aliyoishi nje ya nchi akisema imekuwa vigumu kutangamana upya kwa sababu unyanyapaa na makovu yaliyosalia kisaikolojia yanaendelea kumhangaisha.