• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 1:12 PM
Mama mkwe ameniibia mtoto wangu mchanga, msichana, 24, alia

Mama mkwe ameniibia mtoto wangu mchanga, msichana, 24, alia

Na FLORA KOECH

MWANAMKE wa umri wa miaka 24 katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet analilia mwanawe ambaye anadaiwa kuchukuliwa na mama mkwe bila idhini yake, na hajaweza kumpata miezi miwili baadaye.

Yote yalianza Januari 5, 2024, wakati Sheila Jepchirchir aliacha mtoto wake wa umri wa miezi 20 chini ya uangalizi wa mamake ili kwenda kuchukua stakabadhi zake katika afisi ya mumewe, mjini Serem, kwenye mpaka wa Nandi na Vihiga.

Katika siku mbili akiwa mbali, mama mkwe wake anadaiwa kutembelea nyumbani kwao katika kijiji cha Chebokogwa katika viunga vya mji wa Iten, akidai kwamba alikuwa karibu na eneo hilo baada ya kuhudhuria mazishi eneo jirani hivyo akaonelea afike mle ‘kuwajulia hali’.

Sheila Jepchirchir akiwa na mamake Bendina Kiplagat wakihadithia jinsi mama mkwe alitoroka na mtoto. Picha| Florah Koech

Mamake Jepchirchir, Bendina Kiplagat, aliambia Taifa Leo kwamba alikuwa akiendelea na shughuli zake za kila siku Januari 7, ambapo mwanamke huyo, ambaye familia ilimfahamu, alifika karibu saa kumi jioni. Alikaribishwa vizuri na kupewa chakula.

Karibu dakika 30 baadaye, mgeni huyo ambaye muda huu wote alikuwa amemshikilia mjukuu wake, anadaiwa aliomba aende kwenye duka lililo karibu akanunue soda kwa ajili la watoto wengine wawili waliokuwa mle nyumbani, jambo ambalo alikubaliwa, na wakaenda.

Kulingana na nyanya huyo aliyejawa na majonzi, mgeni huyo alikawia mno kurejea na akaanza kuwa na wasiwasi.

Baada ya saa moja, watoto ambao waliandamana na mgeni walirejea peke yao.

Walimwambia kwamba mama huyo alipanda bodaboda akiwa na mtoto na wakaelekea upande wa Iten mjini.

“Tulimpigia simu mara moja na akadai kwamba alikuwa ameenda kununua nyama na kwamba atarudi na mtoto muda usiokuwa mrefu,” akahadithia mamake Jepchirchir, akisema kwamba haijawahi kutokea, na kuifanya familia hiyo iliyojawa na majonzi kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha Iten baada ya simu walizompigia kukosa kujibiwa tena.

Ripoti iliyonakiliwa katika Kituo cha Polisi cha Iten. Picha|Florah Koech

Imekuwa karibu miezi miwili sasa tangu mtoto huyo apotee.

“Mgeni huyo tunamfahamu kwa sababu alikuwa anafanya biashara eneo jirani kwa zaidi ya miaka 10. Japokuwa hakuwa amemwona mtoto huyo tangu azaliwe, sikuona lolote baya kwa sababu alienda dukani akiwa na watoto wengine wawili,” akasema Bi Kiplagat ambaye alikuwa akilea mtoto huyo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Anadai kwamba mwanamke huyo ambaye ni nyanya ya mtoto huyo amezima simu na hafikiki kufikia sasa.

“Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa mtoto wetu. Serikali itusaidie kumtafuta mtoto kwa sababu hatujui mwanamke huyo alikuwa na nia gani,” akaambia Taifa Leo.

Sheila Jepchirchir akihadithia jinsi mama mkwe wake alikuja kwao akiwa hayuko na kuondoka na mtoto wake mchanga wa miezi 20. Picha|Florah Koech

Kulingana na familia ya Jepchirchir, makazi ya mama mkwe huyo hayafahamiki na kuzima simu kwake kumeongezea wasiwasi wao.

Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet Peter Mulinge alisema kwamba kulingana na wapelelezi wa DCI, hilo suala ni la kifamilia na kwamba wahusika wanafaa kulitatua.

“Kisa hiki hakikuripotiwa kwangu binafsi, lakini habari nilizonazo ni kwamba mtoto huyo alichukuliwa na nyanyake na familia hizo mbili zinafaa kusuluhisha baina yao, kulingana na DCI. Ikiwa kesi ilichukuliwa kuwa uhalifu ningekuwa nimeanza kuishughulikia, lakini nimeambiwa ni suala la kifamilia,” akasema Bw Mulinge akiahidi kuangalia tena.

  • Tags

You can share this post!

Mmiliki wa kiwanda cha gesi ya janga aachiliwa kwa dhamana

Wakenya sasa wanachukua mikopo kununua chakula nyumbani

T L