• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Mama mshukiwa wa mauaji ya wanawe 2 Murang’a ‘asamehewa’

Mama mshukiwa wa mauaji ya wanawe 2 Murang’a ‘asamehewa’

NA MWANGI MUIRURI

MAMA wa miaka 39 kutoka Murang’a ambaye anashukiwa kuangamiza watoto wake wawili kwa shoka akilalamikia hatua ya familia yao kukataa atawazwe kuwa pasta katika kanisa la Repentance and Holiness lake Nabii David Owuor amesamehewa na serikali.

Hii ni baada ya maafisa wa kiusalama waliokuwa wakimchunguza kutoa taarifa rasmi ikionyesha kwamba mama huyo ni mwaathiriwa wa utumwa wa dini uliomwathiri akili.

Kaimu Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini, Bw Joshua Okello alithibitisha ripoti hiyo akidokeza kwamba Jennifer Njeri sasa atawasilishwa hospitalini wala sio mahakamani.

Hii ni baada ya kuua wanawe; Emmanuel Katitu wa miaka mitano na Jayden Muiruri, 3, katika Kijiji cha Kangangu eneobunge la Maragua Desemba 23, 2023.

Bw Okello alisema kwamba “kwa sasa tunafanya mipango ya kumwasilisha mwanamke huyo hospitalini baada ya kubaini kisa hicho kilikuwa mkasa usio wa kisheria.

“Ishara zote zinaonyesha mwingilio wa itikadi za dini uliomkoroga mshukiwa hadi kurukwa na akili na kwa sasa ni bayana hata hajielewi na hana udhibiti wa matendo na maongezi akihitaji usaidizi badala ya adhabu,” akasema Bw Okello.

Awali, Bw Okello alikuwa amefichua kwamba mshukiwa huyo alikuwa ameandika waraka wa mauti akielezea kwamba alikuwa akilenga kuangamiza watoto wake na pia ajitie kitanzi kwa kuwa familia yake ilipinga atawazwe kuwa pasta wa Nabii Owuor.

Nayo taarifa kwa maafisa wa kiusalama kutoka kanisa hilo ambalo serikali imependekeza lipigwe marufuku, ilisema linamjua mama huyo kama mshirika mtiifu aliyeacha kuhudhuria ibada miezi minne iliyopita akiishi wakati huo katika Kaunti ya Kiambu.

“Alikuwa ameandika waraka wa karatasi nne akielezea jinsi familia yake ilikataa atawazwe kuwa pasta katika kanisa la Dkt Owuor na ndipo aliamua kujimaliza na aue watoto wake,” Bw Okello akasema.

Afisa huyo wa serikali aliongeza, “mshukiwa anaonekana dhahiri shahiri kwamba hayuko katika fahamu zake za ulainifu na ametatizwa sana na mwingilio wa imani ya kidini kiasi cha kugeuka kuwa pepo kwake”.

Bw Okello alisema kwamba “mwanamke huyo ndiye alijisalimisha kwa maafisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Kabati kilichoko takriban kilomita 40 kutoka alikoshambulia watoto wake”.

“Maafisa wa polisi Kabati walitupigia simu na tukafika kwa nia ya kumkamata lakini baada ya kumhoji na kumsikiliza kwa makini, tuliona anapaswa kwanza kufikishwa hospitalini atibiwe kwa kuwa waziwazi hana akili timamu,” akasema Bw Okello.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Gavana Wavinya apiga marufuku maiti za ‘wageni’...

Wetang’ula kuwakilisha Afrika katika Jumuiya ya Madola

T L