‘Manabii’ wanavyonyofua hela za maskini
NA BENSON MATHEKA
NI saa nane mchana katikati ya mtaa wa mabanda wa Kibra jijini Nairobi.
Ndani ya chumba cha udongo, kundi la watu waliovalia mavazi meupe wamezunguka mwanaume aliyeketi katikati yao huku akishika mgwisho na Biblia mkononi.
Kila mmoja anasonga mbele kwa zamu na kuinama mbele ya mtu huyo anayeaminika kuwa na nguvu za uponyaji.
Karibu na mlango wa chumba hicho, kuna kikapu kilichofunikwa kwa kitambaa cheupe.
Kila mmoja wao anatumbukiza pesa ndani ya kikapu hicho kabla ya kuondoka na kuelekea kwake nyumbani.
Mwanaume aliyeketi ni mhubiri maarufu anayeaminika kuwa na nguvu za ajabu kuponya maradhi sugu na kutatua matatizo ya wakazi wa mtaa huu.
Kibra ni makao ya watu milioni moja wanaoishi katika ufukara mkuu.
“Watu huja hapa niwahudumie. Ninawaponya na kusuluhisha matatizo yao kupitia maombi,” asema mhubiri huyo aliyejitambulisha kwa jina Nabii Wekesa huku akishika Biblia katika mkono mmoja na mgwisho katika mkono mwingine.
“Hivi ndivyo vifaa vyangu vya kazi,” asema.
Ajabu ni kwamba “nabii’ huyo hana kanisa analoongoza licha ya kuaminiwa na wengi.
Huwa anaendesha shughuli zake kutoka chumba hicho kinachojulikana na wakazi wa hapa kama nyumba ya maombi.
Tuligundua kuwa wakazi wengi wa mitaa ya mabanda wamekuwa wakiwaendea waponyaji wa kidini kupata suluhu ya matatizo yao, yakiwemo ya kiafya na kifamilia. Wahubiri hawa wamekuwa wakivuna pesa nyingi kutoka kwa watu wanaosaka huduma zao huku wengine wakiwapotosha wafuasi wao.
Maombi yanaweza kugharimu hadi Sh20, 000 kwa kutegemea mahitaji ya anayeombewa.
Tulibaini kwamba hali gumu ya maisha na huduma ghali za afya kumefanya wakazi kugeukia huduma za wahuburi hawa ambao wengi wao wanaongoza madhehebu yaliyo na mizizi ya jamii za Kiafrika.
“Wamekuwa wakiwasaidia wakazi wa hapa kwa kuwaombea wapone na kutimua mapepo wakitumia neno la Mungu,” asema Bw John Ogola mkazi wa Kibra Mashimoni.
Naye Bi Josphine Nasimiyu anataja nabii Wekesa kama mtu anayeongozwa na roho wa Mungu ambaye amekuwa msaada kwa wakazi wa mtaa huu.
Sawa na wakazi wengine, Ogola na Nasimiyu wanawavulia kofia manabii hawa na kuwataja kama waliojaaliwa nguvu na maono ya ajabu.
“Watu hutoka mbali kuja kwao wahudumiwe,” asema Ogola.
Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wakazi, mtaa huu una vituo vichache vya afya vinavyoendeshwa na mashirika tofauti na watu binafsi.
Wakazi wanasema vituo hivi havitoi huduma bora kama wafanyavyo wahubiri.
Uchuguzi wetu ulifichua kuwa wahubiri hawa wanatumia gharama ya juu ya matibabu na umaskini wa wakazi kuvuna pesa kupitia maombi ya uponyaji.
Wahubiri hawa huwa na wakati mwema kuvutia watu kwa sababu madhehebu yao yana misingi ya tamaduni za Kiafrika.
Wakenya wengi pia huamini ushirikina na hii huwapatia wahubiri fursa ya kutoa huduma za kutoa mapepo.
“Maradhi mengi yaliyo na watu yanasababishwa na mapepo na dawa ya mapepo ni maombi tu,” asema Wekesa aliyetukataza kumpiga picha akisema imani yake haimruhusu kutangaza huduma zake hadharani.
Baadhi ya wakazi wameshikilia kwa dhati imani ya madhehebu ya wahubiri wao hivi kwamba hawatafuti huduma za matibabu wanapoungua.
“Imani ya kanisa letu haitukubalii kutumia dawa za hospitali. Ninategemea maombi kutoka kwa kasisi wangu,” asema Bi Rhoda Akinyi mfuasi wa dhehebu linalojiita kanisa la Nabii lililoko Kibra Silanga.
Katika uchunguzi wetu wa wiki mbili, tulifichua kwamba watu wengi wamekuwa wakisaka huduma za wahubiri wanaoaminika kuwa na vipawa vya unabii.
Wanawaendea wahubiri hawa na kulipa pesa ili watabiriwe kuhusu hali ya maisha.
Wahubiri hawa wanaaminiwa hivi kwamba baadhi ya watu huwatembelea kila siku za Jumapili wawape mwongozo wa wiki inayofuata.
“Kabla ya kuanza wiki, mimi hufika kwa kasisi wangu ili anipe mwongozo. Kwa sababu sina kazi huwa ananitabiria hatua za kuchukua kabla ya kwenda kutafuta kazi,” asema Bw Michael Wanyama mkazi wa Kibra Silanga.
Kuongezeka kwa watu wanaohitaji maombi kumefanya wahubiri hawa kutoa huduma siku za kazi huku wakiandaa vikao vya kutoa mapepo na maombi kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi.
“Baada ya kuhudumu siku ya Jumapili mimi huandaa vikao vya maombi maalumu kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi,” asema Kasisi Milcah Simon wa kanisa linalojiita Roho wa Bwana.
Hata hivyo, kasisi huyu hana jengo la kanisa na watu humtembelea katika nyumba yake awahudumie.
Tulibaini kwamba wakazi wa mtaa huu wamegeukia wahubiri hawa kutatua shida za kijamii hasa matatizo ya ndoa, kazi na biashara na hata mapenzi.
Tulimpata Bi Philomena Auma akisubiri kuhudumiwa katika kanisa moja eneo la Kibra Lindi baada ya kutofautiana na mumewe.
“Nimefika hapa kumuona nabii. Nilikosana na mume wangu jana,” alisema.
Cha kustaajabisha ni kwamba licha ya wafuasi wao kusongwa na umaskini wa kupindukia, baadhi ya wahubiri wanaendelea kujilimbikizia utajiri mkubwa. Wapo wanaoendesha magari ya kifahari.
“Wafuasi shakiki wa wahubiri hawa ni kama watumwa na huwaletea bidhaa tofauti na pesa. Inasikitisha kuona watu wanaoakabiliwa na umaskini mkubwa kiasi hiki wakiongezewa mzigo kama huu,” asema mkazi Cornelius Karanja, muumini wa kanisa Katoliki.