Manda yageuka maskani ya mapumziko kwa simba, chui na nyoka
NA KALUME KAZUNGU
MANDA ni miongoni mwa zaidi ya visiwa 35 vya Lamu ambapo tangu jadi simba, chui na nyoka hupendelea kuzurura.
Kisiwa hicho ni makazi ya watu karibu 3,000 ambapo wengi wao wanafanya kazi za kilimo na kuchimba changarawe na matofali ya kujengea.
Kisiwa hiki hakina gari hata angalau moja kutokana na kwamba kimezingirwa na Bahari Hindi ilhali barabara zake zikiwa zile za mchanga na mawe mawe.
Isitoshe, barabara zenyewe zimezingira na vichaka na magugu, hali ambayo huzifanya kuonekana pweke kila unapozitumia.
Mbinu ya uchukuzi ipatikanayo kwenye kisiwa cha Manda ni ile ya pikipiki, punda na wanaotembea kwa miguu.
Sifa kuu zinazotambulisha Manda, hasa kwa yule mja anayefika kaunti ya Lamu kwa mara ya kwanza, ni jinsi kisiwa hicho kilivyosheheni visanga kuhusu simba, chui na nyoka wanaorandaranda mara kwa mara mitaani, vijijini na vitongojini.
Ni kwenye kisiwa cha Manda, ambapo utasikia punda au mbuzi wakiwa wamevamiwa na kuuliwa na simba au chui kinyume na maeneo mengine ya Lamu ambapo ni nadra kusikia wanyama hao wakidhuru mifugo.
Mnyama wa pekee aliyeripotiwa kuua punda, mbuzi na kondoo kwenye sehemu zingine za Lamu ni fisi.
Ni Manda ambapo pia utasikia ripoti ya jinsi nyoka wakubwa kwa wadogo wanavyotawala ovyo ovyo, kuvamia makazi ya binadamu na kukera wenyeji si haba.
Wengi wa nyoka hao wanatambuliwa kwa sifa ya kuwa na sumu kali, hasa moma, bafe, swila na wengineo.
Je, kisiwa hiki cha Manda ni mbuga au kinapakana na chochote kinachokaribiana na hifadhi ya wanyama pori?
Maafisa wa Utawala na Wazee wa Kisiwa cha Manda wanasema msitu uliozingira kisiwa hicho, hasa ule wa mikoko na vichaka vingine vimechangia pakubwa kuwavutia wanyama hatari kama simba na chuo kutafuta makazi Manda.
Kadhalika, Manda ni eneo lililopakana na Mradi wa Bandari ya Lamu ulioko eneo la Kililana, Lamu Magharibi. Maeneo hayo mawili yametenganishwa na mkondo wa Bahari Hindi au kivuko maarufu kijulikanacho kama Mkanda.
Kulingana na Chifu wa Manda Mohamed Yusuf Suleiman, simba, chui na wanyamapori wengine walianza kutafuta hifadhi kisiwa cha Manda baada ya msitu waliokuwa wakitumia kama makazi yao kufyekwa kupisha ujenzi wa Bandari ya Lamu.
Bw Suleiman anasema upo msimu ambapo simba na chui huogelea na kuvuka kuingia kisiwa cha Manda kupitia eneo hilo la Mkanda.
“Manda ni kisiwa kilichoanza kufanywa makazi ya binadamu miaka ya 1960. Wengi wa wanaoishi hapa ni Waswahili wa asili ya jamii ya Wabajuni. Ni waliokuwa wakimbizi wa vita vya Shifta vya mwaka 1964 eneo la Kiunga lililoko mpakani mwa Kenya na Somalia. Hawa simba na chui wanaorandaranda mitaani hapa tumewazoea. Hifadhi yao ya Kililana ilipoharibiwa waliishia kukimbilia hapa. Tunatangamana nao hapa,” akasema Bw Suleiman.
Bw Joseph Onyango, mzee wa kisiwa cha Manda, anasema cha kutia moyo ni kwamba licha ya wanyamapori hao kuvamia makazi yao mara kwa mara, hakujakuwa na kisa hata kimoja cha simba au chui kuripotiwa kumvamia au kumuua mtu.
Anasema ni kama wanyama hao wanajua fika kuwa ili kuendelea kuishi kisiwani humo lazima waheshimu binadamu.
“Mahangaiko wanayotupitishia hawa simba na chui ni kuvamia na kuua wanyama wetu, hasa punda, mbuzi na kondoo. Hawajawahi kuua binadamu. Ombi letu kwa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini ni kufikiria jinsi watawadhibiti hawa wanyamapori kwani hali ikiendelea hivi huenda waanze kulenga watu hapa. Mara nyingi tumekutana na hawa wanyama njiani na huwa ni inatisha,” akasema Bw Onyango.
Kwa upande wake, Mary Oduor alieleza kutoridhishwa kwake na jinsi wanyama kama vile nyoka wanavyoonekana kila mara wakitambaa, iwe ni mashambani, kwenye machimbo ya mawe au hata nyumbani mwao.
Kisiwa cha Manda kimekuwa na visa vya watu kuumwa na nyoka ilhali wengine wakiishia kufariki au kupoteza viungo vyao vya mwili, ikiwemo mikono na miguu.
“Twapenda wanyama kweli lakini hii ya nyoka kutambaa kila mara nayo inasinya. KWS iibuke na mbinu ya kuwahamisha hawa nyoka na wanyama wengine hadi maeneo yanayofaa wao kuishi,” akasema Bi Oduor.
Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa KWS Kaunti ya Lamu, Ahmed Ibrahim amekiri kupokea visa kadhaa vya wanyamapori kuonekana kwenye makazi ya binadamu, hasa kisiwani Manda, Pangani na kwingineko.
Bw Ibrahim aidha aliwashauri wakazi kupiga ripoti mara moja endapo wataona wanyama wakivamia sehemu zao.
Pia aliwashauri wale wanaoathiriwa kwa kuumizwa au kuuawa na wanyama pori au mali yao kuharibiwa, ikiwemo mifugo kuuawa kuhakikisha wanaripoti matukio hayo ili uchunguzi ufanywe na kufidiwa.
“Tatizo kubwa hapa ni binadamu kuvamia na kukaa kwenye misitu au njia za wanyama. Ningewasihi waepuke hilo ili kupunguza hizi presha za migogoro kati ya binadamu na wanyamapori,” akasema Bw Ibrahim.