Manusura wa janga la maji kusomba kijiji Mai Mahiu walia kupuuzwa na serikali
MNAMO Jumatatu, Aprili 29, 2024, mwendo wa alfajiri, maji yaliyokusanyika katika shimo chini ya reli huko Kijabe, Kaunti ya Kiambu yalielekea kwa kasi vijiji vya Kamuchira, Jerusalem, Ruiru, Githioro na Georges vilivyoko Mai Mahiu, Kaunti ya Nakuru.
Maji hayo yaliyotoka vilima vya Kijabe na Kinare yalikuwa yamekwama kwa muda kwa kuwa njia ya kutokea ilikuwa imeziba, kabla ya kuta za shimo kupasuka takriban saa tisa usiku.
Yalitiririka kwa nguvu yakisomba mawe, kung’oa miti na uchafu mzito.
Maji hayo yalifika vijiji hivyo vitano kwa kasi ya kutisha, yakaua zaidi ya watu 60 na kuharibu mali ya thamani ya mamilioni ya pesa.
Wengine walinusurika wakiwa na majeraha, lakini wengi walipoteza makazi, mifugo na mashamba yao ya kilimo.
Watu 38 waliorodheshwa kuwa hawajulikani waliko wakati timu za uokoaji za mashirika mbalimbali zilipositisha shughuli za kuwatafuta.
Ingawa mvua kubwa katika maeneo ya vilima vya Kijabe na Kinare ilitajwa kama chanzo cha mkasa huo, baadhi ya manusura wanaamini ulitokana na makosa ya kibinadamu.
Takriban miezi 20 baadaye, manusura wa mkasa wa Maai Mahiu bado wanasumbuliwa na athari za mafuriko hayo.
Kamera za runinga na wageni mashuhuri waliondoka kitambo; misaada ya kibinadamu sasa inatolewa mara chache tu kupitia mashirika ya wahisani na wasamaria wema wanaojitolea kuwasaidia kujenga upya maisha yao.
Miongoni mwa manusura hao ni Bernard Kamau, mwalimu wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 40, ambaye alipoteza wanawe wawili, Maxwel na Rowan, katika mkasa huo huku akinusurika.
“Ilikuwa hali ya kutisha. Niliwasikia wanangu wakilia lakini sikuweza kuwaokoa. Hakuna uchungu mkubwa kama kujua huwezi hata kuwaokoa watoto wako,” alikumbuka kwa masikitiko.
Bw Kamau aliyekuwa mmiliki wa nyumba kumi, sasa anaishi ya kupanga mjini Maai Mahiu na anahangaika kuanza maisha upya. “Serikali ilitusahau kabisa baada ya ahadi nyingi. Familia nyingi bado hazijapona kutokana na mkasa huu,” alisema.
Kwa upande wake, Mary Muthoni, 61, alipoteza watu wanane wa familia na sasa anaishi katika kijiji cha Memo, Murungaru, Kaunti ya Nyandarua.
Usiku wa mkasa, alikuwa amewaalika watoto na wajukuu wake nyumbani kwake Ngeya karibu na kituo cha biashara cha Maai Mahiu kusaidia kuchangisha pesa kupata dhamana ya mwanawe Isaac Mwangi aliyekuwa amezuiliwa na polisi kwa mwaka mmoja.
Kati ya watu 12 waliokuwa nyumbani humo, ni wanne pekee walionusurika; wanane waliangamia. Miongoni mwa waliokufa ni binti yake kitinda mimba aliyekuwa mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza, mkwe wake na wajukuu sita.
Bi Muthoni, ambaye pia aliwahi kuwa mkimbizi wa mapigano ya kikabila mwaka 1988 Londiani na 1992 Narok, alisema alipoteza nyumba aliyokuwa amepanga, mali yote na ardhi yake yenye rutuba ambayo sasa imefunikwa na mawe na tope.
“Tuliahidiwa makazi mapya na serikali lakini hakuna chochote kimefanyika. Tunaishi kwa shida,” alisema.
Wahisani walimchangia Sh1 milioni, akatumia Sh750,000 kununua nusu ekari na kuanza kujenga nyumba, lakini ujenzi huo umekwama kwa kukosa fedha.
Bw Alex Kimani, manusura mwingine, alipoteza familia yake yote na bado anateseka kisaikolojia kufuatia kutopatikana kwa miili ya binti zake.
Msamaria mwema kutoka Amerika alimjengea nyumba, hatua iliyopunguza mzigo wa kodi. Ingawa ameoa tena, maisha bado ni magumu.
“Siwezi kufanya kazi kwa sababu ya jeraha la mkono na kifua. Nilikuwa nauza matunda sokoni Maai Mahiu. Serikali ilitoa ahadi nyingi lakini ilituacha baada ya miezi michache,” alisema.
Rais William Ruto alipotembelea eneo hilo Aprili 30, 2024, aliahidi serikali ingewatafutia waathiriwa ardhi wajenge makazi mapya.
Zaidi ya mwaka mmoja baadaye, wengi bado hawana ardhi wala makazi. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki hivi majuzi alisema bei ya juu ya ardhi imechelewesha mpango huo licha ya Sh250 milioni kutengwa.
Wakati huo huo, wahisani kama Rotary International na Scann Foundation wamejenga nyumba 18 za vyumba viwili kwa baadhi ya familia zilizoathirika.
Hata hivyo, manusura wengi bado wako njia panda, wakiwa na majeraha ya mwili na akili, na wakihisi kusahauliwa. Bado wanatumaini serikali itatimiza ahadi zake, iwape makazi na kurejesha ardhi yenye rutuba iliyopotea katika mkasa huo.