Makala

Manusura wa shambulio la Al-Shabaab aapa kuhubiri amani hadi kifo

March 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

TUKIO la kigaidi la mwaka 2014 mjini Mpeketoni, Kaunti ya Lamu liliacha makovu mabaya kwenye maisha ya wengi eneo hilo.

Shambulio hilo la Al-Shabaab lililotekelezwa Juni 15, 2014, lilisababisha wanaume zaidi ya 90 kuuawa huku nayo makumi ya magari na nyumba zikiteketezwa kwa usiku mmoja.

Ni uvamizi ulioacha wengi wakiwa na hasira, kiwewe, majonzi na wengine wakisalia kushtuka hadi leo.

Aidha kuna wale ambao kumbukumbu ya madhila waliyoyaona iliwasukuma kubadilisha mwelekeo wa maisha yao.

Miongoni mwa watu hao ni mwalimu Ibrahim Shahibu Shekue.

Balozi wa amani Ibrahim Shahibu Shekue akisimama mbele ya mnara ulioorodhesha majina karibu 90 ha wanaume waliouawa na Al-Shabaab mjini Mpeketoni mnamo Juni 15, 2014. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Shekue,61, alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi ya Lake Kenyatta, iliyoko mjini Mpeketoni wakati shambulio la 2014 lilipotekelezwa.

Anakumbuka alivyodamka mapema kutoka mafichoni asubuhi baada ya mauaji ya usiku kucha, ambapo aliharakisha kuripoti shuleni, ikizingatiwa kuwa alikuwa ndiye mwalimu wa zamu wiki hiyo.

Bw Shekue anaeleza jinsi alivyopita mjini huku akijionea mandhari ya kutisha yaliyotapakaa damu na maiti kuenea kila mahali.

Sehemu mojawapo ya mji wa Mpeketoni ambao ulivamiwa na Al-Shabaab mnamo Juni 15, 2014. Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 90 usiku mmoja. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema aliupiga moyo konde na kuelekea shuleni akitetemeka huku kila alikopitia akisikia vilio. Yaani mji wa Mpeketoni ulikuwa umegeuzwa kuwa matangani.

“Nilifika shuleni saa kumi na mbili alfajiri na niliyokuwa nimeyapita njiani yalinitisha na kunimaliza nguvu. Damu na miili ya watu waliouawa kinyama na Al-Shabaab ilikuwa imelala kila mtaa na vibaraste vya mji wa Mpeketoni,” akaeleza Bw Shekue.

Anasema alipofika shuleni alikuta mazingira ya upweke kwani wanafunzi na walimu hawakufika.

Kutokana na hilo, Bw Shekue anasema aliafikia kurudi mjini Mpeketoni ili kuomboleza na jamaa na marafiki waliofikiwa na pepo hilo la mauti.

Mbali na ualimu, Bw Shekue kwa wakati huo pia alikuwa akishikilia wadhfa wa mwenyekiti wa Muungano wa jamii ya Waislamu wa taarafa ya Mpeketoni.

Anaeleza kuwa Al-Shabaab mbali na kutekeleza mauaji na uharibifu wa mali, pia waliacha ugonjwa mwingine hatari mjini Mpeketoni na Lamu kwa jumla.

Maradhi hayo ni chuki na migawanyiko ya kidini na kikabila.

Anaeleza masikitiko yake alipoona jinsi Wakristo na Waislamu wa Mpeketoni na viunga vyake walivyotofautiana waziwazi na kunyosheana vidole vya lawama, hasa kuhusiana na mauaji hayo ya kigaidi.

“Wakristo na Waislamu ambao awali waliishi kama mandugu walianza kuchukuliana kama maadui punde shambulio na mauaji ya Mpeketoni yalipotekelezwa. Al-Shabaab walitekeleza mauaji wakitumia misingi ya kidini kwani walilenga Wakristo na kuwaua kwa wingi. Tukio hilo lilisababisha kupandwa na kumea kwa mbegu chafu ya mgawanyiko wa kidini,” anaeleza Bw Shekue.

Ni kutokana na hilo ambapo Bw Shekue alijiita mkutano wa nafsi na kuibuka na mbinu ya kusuluhisha migongano iliyokuwepo kwani anasema hata yeye mwenyewe ilimuathiri kisaikolojia si haba.

“Unaonaje wewe upite njiani kisha mtu anakutupia cheche za maneno kwamba ni gaidi na muuaji. Wakristo na Waislamu hawakutaka kuonana ana kwa ana. Hapo ndipo nikaafikia kuchukua jukumu zito la kuwapigia viongozi wa dini zote Mpeketoni, ikiwemo Waislamu na Wakristo ili kujadiliana na kuweka mambo sawasawa,” akasema Bw Shekue.

Anasema ni kupitia juhudi hizo, ambazo awali zilikumbwa na pingamizi za pande hizo mbili zilizopandiwa mbegu ya uadui na chuki, ambapo mwishowe alifaulu kuleta uwiano na utangamano wa makabila na dini zote za Lamu, hasa kupitia kuundwa kwa vuguvugu la amani kwa jina Lamu Interfaith Peace Initiative.

Vuguvugu hilo lilimteua Bw Shekue kuwa mwenyekiti wake hadi leo.

Anasema ni kupitia juhudi za Lamu Interfaith Peace Initiative ambapo migawanyiko, iwe ya kidini au ya kikabila iliyokuwa imepandwa na adui Al-Shabaab waliweza kuishinda.

“Vuguvugu letu lilituwezesha sisi viongozi wa Kiislamu na Kikristo kushikana na kuzunguka kila kona ya Mpeketoni na Lamu, miji, vijijini na vitongojini tukihubiri amani, uwiano na utangamano wa makabila na dini zote. Twashukuru kwamba leo Waislamu na Wakristo wa Lamu wanashirikiana, wakikaa meza moja kula na kunywa kinyume na awali ambapo uadui ulikuwa umekita mizizi,” akasema Bw Shekue.

Anasema ni kupitia kile alichokiona wakati wa shambulio la Al-Shabaab mjini Mpeketoni, ambapo fikra na mtazamo wake kuhusu maisha ulibadilika.

“Tangu mwaka huo hadi sasa mimi ni balozi wa amani. Ninafanya hivyo ima nikifundisha shuleni kama mwalimu, nikiwa kama kiongozi wa dini misikitini na vilevile kuenda makanisani au kwenye mikutano ya kijamii kama mzee. Nilikuwa nikiishi Mpeketoni wakati Al-Shabaab walitekeleza mauaji usiku huo, hivyo mimi pia ni manusura wa shambulio la Al-Shabaab. Na ndio sababu nikaapa kuhubiri amani hadi kifo,” akasema Bw Shekue.

Kwa wanaomjua Bw Shekue wanamtaja kuwa rafiki, mpenda amani, mpole, mlezi na mcheshi.

Bw Ibrahim Shahibu Shekue wakati wa mahojiano na Taifa Leo mjini Mpeketoni, Lamu. Yeye ni manusura wa shambulio la Al-Shabaab ambaye ameapa kuhubiri amani hadi kifo. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Alex Mugo, mkazi wa Mpeketoni, alisema ni kupitia juhudi za Bw Sekue ambapo umoja wa dini na makabila yote umedumishwa, sio Mpeketoni tu bali pia Lamu yote.

“Sio rahisi kumpata Muislamu kukaa mahali kama kanisani akisikiliza ibada toka mwanzo hadi mwisho na kisha baadaye kutangamana na waumini bila ubaguzi. Huyo Bw Sekue ni mwadilifu, mpenda amani, mcheshi, mwenye kuelewa na asiye na ubaguzi. Ni kielelezo tosha cha mja anayejiita balozi wa amani Lamu, Kenya na ulimwengu,” akasema Bw Mugo.

Bi Lucy Kimani aliomba wananci wote na vionozi kuia mfano wa Bw Sekue ili upendo, umoja, uwiano na utanamano wa makabila na dini ufaulu hata zaidi.

Bw Shekue alizaliwa kijiji cha Kizingitini kilichoko Faza, Kaunti ndogo ya Lamu Mashariki mwaka 1963.

Alisomea shule ya msingi ya Kizingitini kabla ya kujiunga na Shule ya upili ya Mpeketoni iliyoko Lamu Magharibi na kisha ile ya wavulana ya Malindi High alikohitimisha masomo yake ya sekondari.

Baadaye alijiunga na Taasisi ya Mafunzo ya Walimu ya Egoji iliyoko Kaunti ya Meru alikosomea na kuhitimu kozi ya ualimu.

Yeye ni baba wa watoto watatu – wavulana wawili na msichana mmoja.